Walikuwepo
ndugu wawili wanaume, ambao, baba yao alipokufa walirithi shilingi mia sita.
Mmoja alifanya biashara ya kuuza samaki sokoni na yule wa pili alifikiri kwanza
jambo bora la kufanza kwa shilingi zake mia tatu. lkamjia fikira ya kuondoka
hapo kwao na kwenda nchi za mbali kutembea. Katika hayo matembezi yake alimkuta
mtu yumo ndani ya ofisi yake iliyojaa viti na meza. Aliuliza habari za ofisi
ile, na aliambiwa kuwa ofisi ile ni ya mtu ambaye kazi yake ni kuuza maneno, na
ya kuwa bei ya kila neno ni shilingi mia. Yule mtoto alifikiri na ilimfahamikia
kuwa hapana shaka kuwa maneno hayo yanayouzwa ni yenye manufaa makubwa. Hapo
alikwenda kwa huyo anayeuza maneno na akamwambia kuwa anataka kununua maneno.
Yule mtu alimwambia atoe shilingi mia kwanza, ndipo amuuzie neno moja, yaani
habari moja ya maneno. Yule mtoto alitoa shilingi mia. Hapo aliambiwa na yule
mtu, 'Mungu akikupa kitu kidogo bora upokee na ushukuru.' Yule kijana
alimwambia, 'Nambie tena jambo jengine.' Alijibiwa kuwa hawezi kuambiwa jambo
jengine mpaka atoe shilingi mia. Aliomba apunguziwe lakini hakukubaliwa. Kwa
hivyo alitoa shilingi mia nyingine. Yule mtu alimwambia, 'Ukipita pahali
ukakaribishwa bora ukae kidogo.' Sasa yule kijana kabakia na shilingi mia tu.
Lakini juu ya hivyo akataka aambiwe jambo jengine. Basi alizitoa zile shilingi
mia zilizobaki na akaambiwa, 'Ukiaminiwa jiaminishe.' Hapo yule kijana alipigana
pigana akapata nauli ya kurudi kwao. Alipofika huko kwao ndugu yake mwenye
biashara ya samaki alimwuliza namna alivyo tumia shilingi zake mia tatu.
Alimjibu kuwa alizinunulia maneno. Ndugu yake aliruka na kumwambia, 'Ebo!!
Sijapata kuona mtu mpumbavu kama wewe, umezitupa shilingi mia tatu bure!! Bora
tukufunge kamba tukuweke hapa kwanza, bila ya shaka, umeingiliwa na wazimu.'
Yule muuza samaki hakutaka kumsaidia nduguye kwa chakula, basi huyo nduguye
alikuwa akizubaa zubaa tu na kula anachokipata. Yeye huyo aliyepoteza pesa zake
alikuwa hodari kwa kuandika Kiswahili. Kwani aliwahi kujifundisha kuandika hapo
zamani kidogo. Mara moja alimjia mtu amuandikie barua ya kuomba kazi kwa Mfalme.
Hapo yule kijana aliiandika barua nzuri sana, ya kupendeza na ya kufurahisha.
Yule mwenye kuandikiwa ile barua alitoa senti ishirini na kumpa huyo muandikaji.
Yule kijana alitaka kuzikataa kwani zilikuwa kidogo sana ukilinganisha na
jitihada aliyofanya katika kuiandika barua hiyo. Alipofikiri lile neno
alilonunua kwa shilingi mia, kuwa Mungu atakachokupa bora upokee, zile senti
ishirini alizipokea akaenda akajinunulia mkate. Barua hiyo ilifika kwa Mfalme
naye aliipenda sana, na akataka amuone aliyeiandika. Kwa hivyo yule muandikaji
alitafutwa na kupelekwa mbele ya Mfalme. Alipofika huko Mfalme alimpenda sana.
Mfalme alimuuliza kazi anayofanya na alisema kuwa hana kazi. Alimuuliza kuwa ana
wazee na alijibu kuwa ana ndugu yake mmoja tu anayefanya kazi ya kuuza samaki.
Mfalme alimwambia kuwa atamuweka hapo kwake awe mtu wake wa kuandika mambo yake.
Yule kijana alifurahi sana. Basi alikaa huko na alipewa kila namna ya raha.
Alipewa mshahara mzuri, nyumba nzuri na aliozwa mke mzuri pia. Alipofikiri hali
ya nduguye, muuza samaki, alitamani ampatie kazi bora huko kwa mfalme. Kwa hivyo
alimwambia mfalme kuwa angependa nduguye apewe kazi hapo alipo yeye. Mfalme
alikubali na hapo aliitwa akafika mbele ya mfalme. Alipoitwa huko kwa mfalme
alidhani anakwenda kuadhibiwa. Kwani alifikiri kuwa yule nduguye aliyekataa
kumsaidia, anayefanya kazi huko kwa mfalme, amemtilia fitina. Hapo alikwenda
huko kwa mfalme shingo begani kwa ajili ya khofu aliyokuwa nayo. Alipofika huko,
mfalme alimwambia kuwa ndugu yake anapenda naye afanye kazi hapo pake ikiwa
atapenda. Yule kijana alijibu, 'Napenda sana, Bwana.' Aliulizwa kazi apendayo na
alijibu kuwa anapenda kazi ya kuuza duka. Hapo alipewa pesa nyingi na alifungua
duka kubwa sana mjini. Kwani mfalme aliona bora amsaidie kwa pesa ili afungue
duka lake mwenyewe kuliko kumweka hapo pake kwa kumfanyia kazi zake. Kijana huyo
alijilaumu sana kwa kumfukuza yule ndugu yake hapo zamani na alistaajabu kwa
msaada alioupata kwa nduguye aliyemfukuza. Basi aliendelea na kazi za duka na
muda si muda alikuwa mmoja katika matajiri wa hapo. Mfalme alimpenda sana yule
kijana mwandishi na alimfanya kuwa waziri wake. Mke wa yule mfalme alimpenda
sana yule waziri mpya na alitamani kila wakati amuone. Mara moja mfalme alitaka
kusafiri pamoja na mkewe kwa muda wa siku chache. Basi kwa jinsi ya kumpenda
huyo kijana yaani waziri mpya, alimwacha hapo kwake awe naibu wake na atazame
kila jambo. Mke wa mfalme alikataa kumfuata mumewe huko safarini alipojua kuwa
yule kijana anayempenda atasalia pale nyumbani. Kwa hivyo alimuomba mfalme
amuache hapo nyumbani. Mfalme alimwacha mkewe hapo nyumbani na akaenda kwenye
safari yake. Mfalme alipoondoka, yule mkewe afimpeleka mtu kwa yule naibu
kuitwa. Yule naibu alikwenda kwa haraka kusikiliza amri ya Malkia. Naibu
alipofika kwa Malkia, alimkuta amejipamba sana na alionekana kuwa mzuri kuliko
mwanamke yeyote mjini. Hapo Naibu alimwuliza Malkia haja yake. Malkia alimjibu,
'Tokea ulipofika hapa petu nalianza kukupenda sana basi napenda uwe rafiki yangu
tokea leo usiku na unifanyie kama nitakalokuambia.' Hapo, yule naibu wa Mfalme,
lilimjia lile neno alilolinunua kwa shilingi mia, nalo ni kuwa akiaminiwa
ajiaminishe. Basi, pasipo na kupoteza wakati alimjibu, 'Mimi sipendi urafiki
nawe kabisa kwani siwezi kuvunja uaminifu wangu.' Malkia alikasirika sana na
alimtisha yule kijana kuwa atamfanya mambo ya kumpatisha adhabu asipokubali
urafiki naye. Yule kijana alifungua mlango na akaenda zake mbio. Malkia
alijaribu kumfukuza kidogo, lakini hakumpata. Malkia alipokuwa akisema maneno
hayo alikuwepo askari nyuma ya mlango na alisikia maneno yote. Malkia alipokata
tamaa kuwa anayoyataka kwa yule naibu hatayapata, alitengeneza chumba kidogo
kilichokuwepo mbali na vyumba vyengine vya nyumba yake. Huko alitia kijigodoro
na kijito. Aliposikia kuwa mumewe, mfalme, karibu atarudi alidai kuwa ni mgonjwa
na alijiweka katika hali ya unyonge. Mfalme aliporudi alishtuka sana alipoona
hali dhaifu ya mkewe. Hapo mfalme alipotaka kujua jambo lililomfika mkewe,
Malkia alijibu, 'Tokea ulipoondoka nilikuwa nikiadhibiwa na yule naibu wako
uliyemuacha hapa, alikuwa ananitaka kwa urafiki na mimi sikupenda jambo hilo.
Kwa hivyo adhabu ilipokuwa kubwa nilihamia kule kwenye chumba kidogo. Nashukuru
bwana umefika leo, angalao nishushe puma." Mfalme alipokitazama. kile chumba
alichodai kuwa ndiko alikokuwa akilala, alihamaki hata yule bibi mwenyewe
alimuogopa. Hapo mfalme alifikiri lazima amuue yule naibu lakini hakupenda
kumuua watu wakajua, maana watu wakijua watataka wajue sababu ya kifo cha naibu,
na wakijua sababu
ya kifo chake basi itakuwa ni aibu juu ya nyumba yake. Basi Mfalme alimuagizia naibu wake wa shamba aje mjini, nokoa alipofika aliambiwa na mfalme, 'Nenda shamba kachimbe shimo la kiasi ya futi ishirini na liwe tayari kesho asubuhi. Akija mtu yeyote, ijapo mtoto wangu, akikuuliza, "Kazi ya bwana imekwisha?" hapo mtumbukize humo shimoni. Ukitoa siri hii, nokoa, nitakuua.' Nokoa alifanya kama alivyoambiwa huko shamba. Asubuhi mfalme alimwita naibu na akamwambia apande farasi aende huko shamba kwa nokoa akamuulize kuwa kazi imekwisha. Yule naibu alipanda farasi akaandama njia ya kwendea kwa nokoa. Alipofika kati ya njia alikuta watu wamekaa nyumbani, watu wote walisimama na kumkaribisha kahawa. Yule naibu hakutaka kukaa lakini alipofikiri lile neno alilolinunua kwa Shilingi mia nalo ni kuwa akikaribishwa ni bora akae, alikaa na kungojea kahawa. Mfalme alifanya wasiwasi na alitaka kujua kama naibu wake amekwisha tumbukizwa shimoni au bado kwa hivyo alimpeleka mwanawe aende kwa nokoa akamuulize kama kazi imekwisha. Mfalme alisahau kufikiri habari ya kumtuma mwanawe huko. Yule mtoto alikwenda upesi sana na alifika kwa nokoa kabla ya yule aliyetumwa kwanza hajafika, nokoa alipomuona mtoto wa mfalme, alihuzunika sana kwa ajali iliyomkabili. Yule mtoto alimuuliza nokoa, 'Kazi ya bwana imekwisha?' Nokoa alijibu, 'Naam, twende nikakuonyeshe.' Hapo yule mtoto wa mfalme alifuatana na nokoa mpaka huko kwenye shimo na kufika hapo pembezoni mwa shimo, hapo, nokoa alimtumbukiza na kumfukia. Yule naibu alipokwisha kunywa kahawa kule alikokaribishwa alikimbilia kwa nokoa, naye akamwuliza, 'Kazi ya bwana imekwisha?' Nokoa alimjibu, 'Naam, imekwisha.' Hapo alirudi kwa mfalme. Mfalme na mkewe walikuwa roshanini kumngojea mtoto wao aje kutoa habari. Mara walimuona yule naibu anarudi. Hapo mfalme na mkewe walilia sana kwani walijua kuwa mtoto wao amekufa. Naibu alimjibu mfalme kuwa kazi imekwisha Mfalme alimwita yule naibu na kumwambia amtolee hadithi ya maisha yake na amwambie kama lililokuwa alipoondoka. Kwani aliona kuwa Mungu anampenda sana kijana yule, kwa hivyo lazima liko jambo linalomsaidia. Yule kijana aliitoa hadithi ya maisha yake tokea mwanzo wa kurithi shilingi mia tatu mpaka akanunua maneno. Vile vile alimwambia mambo yaliyojiri baina yake na mkewe alipokuwa safarini. Yule bibi aliyakanusha yale aliyoyataka kwa naibu, lakini naibu alimwita yule askari aliyekuwa akisikiliza maneno aliyoyasema Malkia kumwambia yeye. Askari aliyasema maneno yote. Hapo mfalme alimwambia Malkia kuwa yeye ndiye aliyesabibisha mauti ya mwanawe na ya kuwa yeye ni mwanamke mbaya sana. Mfalme alimwambia yule naibu wake kuwa lazima amuue mkewe kwa ubaya wake na alimweleza namna alivyosalimika na mauti ya shimo na akaingia mwanawe. Yule naibu mwenye akili alimuomba mfalme asimuue mkewe lakini ampe adabu tu. Basi mfalme alikubali. Adabu ya kwanza aliyompa, alimuacha, tena akamfunga miaka kumi. Basi kwa hiyo taabu aliyoipata alikufa kabla ya muda wa kufunguliwa haukufika. Mfalme naye hakuishi sana akafa. Basi yule waziri ndiye aliyetawala. Ufalme alioupata yule naibu ulisabibishwa na yale maneno aliyoyanunua kwa shilingi mia tatu. Basi yule mke wa mfalme aliyetaka kumtia huyu naibu matatani aliingia matatani mwenyewe na kusabibisha kifo cha mwanawe. Ndipo watu wakasema, 'Mchimba kisima huingia mwenyewe.

0 comments:
Post a Comment