Search This Blog

Wednesday, December 21, 2022

Ukupigao Ndio Ukufunzao


      Alikuwepo mtu mmoja ambaye alikuwa mvivu kupita kiasi, alikuwa akipenda kulala tu na pengine hupita mikahawani na kupiga masoga. Mtu huyo, vile vile, alikuwa na tabia ya uchafu wa kiwiliwili chake na nguo pia. Hakupenda kufua nguo, kukoga, kukata makucha wala kusafisha meno yake. Alikuwa mtu yeyote hapendi kumtupia macho kwa hali ya uchafu wake. Watu wa hapo kwao wakifanya kazi za kulima chakula chao na pesa za matumizi ya mambo mengine pia zilikuwa zikitoka humo humo katika vipando vyao. Mtu huyo mvivu alikuwa na tabia ya kupita katika vijumba vya wenziwe na kudusa. Alikuwa akijuwa wakati wa kila mtu anapokunywa chai au anapokula chakula cha mchana au kijio. Akijua kuwa, sasa mtu fulani yu tayari kula, huko kwake, basi atakwenda ajidai kutoa masoga mpaka akaribishwe kula. Hii ndiyo iliyokuwa tabia yake na hivi ndivyo alivyokuwa akiishi. Watu wa hapo kwao walianza kukirihika kwa tabia yake hii mbaya na kila mtu alikuwa akimsema na kumdharau. Yeye mwenyewe alitambua kuwa watu wanaudhika naye, sababu baadhi ya watu, wale machope machope, walikuwa wakimwambia, 'Eh, baba wee, kazi yako ni kupita majumbani na kudusa tu, hufanyi kazi!!' Yule mtu hakuwacha tabia yake kwani alipokuwa akienda kule majumbani kwa watu mahashumu yaani watu wenye haya na tabia nzuri, walikuwa wakisema naye vizuri, na kuchekacheka naye, basi aliona haudhi mtu. Lakini juu ya hivyo hata wale watu mahashumu hawakupenda tabia yake. Kwa muda kupita ulianza mnong'ono mjini, watu wote pamoja walifanya shauri kuwa mtu huyo akomeshwe tabia hii ya uvivu, ya kupita majumbani mwa watu na kudusa. Katika mkutano huo wa watu palikubaliwa na watu wote kuwa wamwendee watu wawili wamwambie kuwa watu wote hawaipendi tabia yake mbaya hii, na ya kuwa ni lazima afanye kazi kama watu wengine na asipofanya hivyo watu wote wa hapo kwao hawatamsaidia kwa chakula. Walimwendea watu wawili wasiokuwa na muhali yaani wasiokuwa na haya. Walimkuta mkahawani anapiga soga na huku ana kipande cha andazi mkononi anakinyofoa nyofoa. Kiandazi hicho alikiomba kwa mtu aliyekuja hapo mkahawani na kununua kikombe cha tangawizi na andazi moja. Wale watu wawili walimwita siri na walianza kumwambia kuwa watu wa hapo kwao wamewatuma wamwambie aache tabia ya uvivu aende akalime kama watu wengine na aache kupita vijumbani akidusa na ya kuwa tokea siku ile hatapewa chakula na mtu yeyote. Alipoambiwa maneno haya yule mvivu, alipuuza, akajichekesha na kurudi hapo mkahawani na kuendelea na sogalake. Wakati wa chakula cha mchana ulipofika, alianza kazi yake ya kuranda. Alikwenda kwa mtu wa kwanza akakuta watu wanapakuwa. Hapo alikaa na kujikuna kuna kichwa na huko yumo katika kutoa porojo lake la desturi. Mwenye nyumba alimwambia, 'Jana tulikutumia fulani na fulani, hawakukwambia maneno ya watu wa mji?' Hapo alinyamaza kimya, hakujibu. Hapo yule mwenye nyumba alifunga mlango wake na huku anamwambia, 'Haya baba, kwa heri.' Lile vivu lilikwenda zake na akaona, hakika mambo yamemharibikia. Alijaribu tena kwenda nyumba nyingine, alipofika huko watu wanakosha mikono ili wapate kula, naye alinyoosha mkono wake atiliwe maji ya kunawa, lakini mtia maji hakumtilia na aliona haya sana. Hapo hakuambiwa neno wala hakukaribishwa bali watu waliinama na kuendelea kula tu. Hapo vivu lilinyerereka likaenda zake na huku analia kwa njaa. Watu wa nchi hiyo walikuwa wakarimu sana lakini walifanya hivyo kwa kutaka kumuelimisha mwendo mzuri wa kibinadamu. Njaa ilipomshika barabara, lile vivu ilimjia fikira aende kwa mtu yeyote akamuombe kazi apate chakula badala ya kuomba chakula. Basi alikwenda kwa Mwarabu mmoja wa Maskati aliyekuwa akiweka duka hapo kwao na kumwambia ampe kazi. Yule Mwarabu alikuwa hajui kusema Kiswahili vizuri, basi alimjibu, 'Kama nataka kazi, tasafisha haba mbele ya nyumba wangu, khalafu tashkuwa ndoo na kwenda kwa mtoni nashkuwa maji naleta, taumba senti khamsini.' Yule mvivu alijikaza na akaifanya ile kazi ya kusafisha mbele ya nyumba ya yule Mwarabu na kwenda mtoni kuchukua maji akapewa, senti khamsini. Hapo alijinunulia nusu kibaba cha mchele na nguru wa senti kumi akaenda akajipikia akala akashiba. Alipokwisha kula, ilimjia ari na fikira ya maisha yake mabaya, alisema moyoni mwake kuwa ni lazima ajisaidie kwa kufanya kazi, hataki tena kudusa wala kutamania mtu yeyote. Hapo alifanya kazi ndogo ndogo hapo mjini kwao na huku anadunduliza vipesa hata akapata shilingi nne akazinunulia jembe la kulimia. Basi aliacha tabia ya uvivu na alianza kufanya kazi. Alikwenda kwenye kisitu alichokirithi kwa mama yake, akaanza kukifyeka na kupanda kila namna ya vitu. Alipanda mtama, mahindi, mboga, matango na vyenginevyo. Mungu alimbarikia akavuna vitu vingi sana akavijaza ndani ya kibanda chake na ikawa hahitaji kitu cho chote cha mtu. Siku zote alikuwa yakimjia majuto ya maisha yake ya nyuma na akijilaumu sana kuishi maisha yale ya kivivu na fedheha. Mavuno yake yalipokuwa makubwa, yaani yalipomzidi hata ikawa hawezi kuyala peke yake, alichukuwa baadhi ya vitu kama vile mahindi na mboga na kuvipeleka sokoni kuviuza. Watu walipomuona huko sokoni, hawakupenda kununua vitu vyake kabisa kwa sababu ile tabia yake ya uchafu hakuiacha bali alizidi kuwa mchafu tokea alipoanza kujishughulisha kwa kazi za kulima. Huko sokoni alipambana na mtu mmoja aliyependa sana mboga zake lakini alipomuona mwenye mboga alisema, 'Oh, sipendi mboga zako, sababu wewe u mchafu. Nenda kakoge, ufue nguo zako na ukate makucha yako, halafu unaweza kuja kuuza vitu vyako na watu wanaweza kuvinunua.' Yule mtu alijilaumu sana kwa kujiweka mchafu. Kwa hivyo alianza kujinadhifisha na kujiweka katika hali nzuri. Mara ya pili alipeleka tena vitu vyake sokoni, watu walipomuona huko walimfurahikia sana kwa unadhifu wake na vitu vyake vizuri. Aliuza vitu vyake kwa bei nzuri sana na alirudi kwake na pesa chungu nzima. Huyo mtu alitanukiwa na maisha yake haya mapya. Aliendelea kufanya kazi na kuuza vitu sokoni hata akawa na pesa nyingi sana. Hapo alijenga nyumba nzuri na kununua nguo nzuri. Basi aliishi maisha ya raha na furaha kama wenziwe au zaidi. Mtu huyo asingelipata raha hiyo lakini alipopigwa na njaa alifundishika, akaanza kufanya kazi na vitu vyake vilipokataliwa huko sokoni, vile vile, alifundishika akaacha tabia ya uchafu. Kwa hivyo ni kweli wanayosema watu kuwa ukupigao ndio ukufunzao.

0 comments:

Post a Comment

BLOG