Search This Blog

Wednesday, December 21, 2022

UA JEKUNDU

 





    SIMULIZI FUPI: UA JEKUNDU!!!

    __TUTAMBUE MAANA YA UPENDO___

    NA: George Iron Mosenya



    Mvua ilikuwa inanyesha katika jiji la Mwanza na kuwafanya wakazi wake kujikinga katika vibanda mbalimbali ili wasikumbwe na madhara ya ile mvua.

    Mvua iliendelea kumwagika kwa kasi na kama masihara vile mvua ile ikaleta balaa. Mitaro ikaanza kujaa maji.

    Nikajitazama mavazi niliyokuwa nimevaa, suti nyeusi na mkononi nikiwa na bahasha ya kaki ndani yake pakiwa na ua jekundu na na kadi kwa ajili ya mpenzi wangu!!

    Watu kadhaa waliokuwa wamejikinga pale walikuwa wamevaa nguo nyekundu.

    Naam! Ilikuwa siku ya wapendanao!!

    Nilijua kuwa muda ule mpenzi wangu Matha alikuwa akinisubiri kwa hamu kubwa lakini nisingeweza kwenda kwa sababu mvua ilikuwa kali sana.

    Mara maji yakazidi na sasa yakaanza kupita huku yakisafirisha kwa kasi vitu kama masufuria, mabeseni na ndoo za maji.

    Mungu wangu yalikuwa ni mafuriko!!!

    Mafuriko jijini Mwanza!!

    Mvua iliendelea kupiga kwa kasi, sasa zilipita redio pamoja na vifaa vingine vya ndani kama redio na luninga!!

    Pale tulipokuwa kila mmoja aliingiwa na mashaka, watu wakajaribu kutumia simu za mikononi lakini mara tukapeana maonyo kuwa palikuwa na dalili mbaya ya kuweza kupigwa na radi kwa kutumia simu katika mvua ile.

    Hakuna aliyekuwa anatabasamu tena, sasa kila mmoja akawa na mashaka!!

    Tukiwa bado katika hali ile mara katika maji yale aliibuka mtoto mdogo akapiga kelele kidogo na maji yakaendelea kuondoka naye.

    Jicho langu lilimuona nisingeweza kujifanya sijamuona, nilijitahidi kusahau na kujifanya sijamuona lakini nafsi ilinisuta. Nikamfikiria kuwa yule ni mtoto, sikujua wazazi wake ama wakubwa zake walifanya jitihada gani katika kumuokoa.

    Nilipowaza kuhusu wakubwa wake nikakumbuka kuwa hata mimi ni mkubwa wake. Je ni jitihada gani ambazo nimefanya ili kumuokoa.

    Na hapo nikakumbuka kuwa ile ilikuwa ni siku ya wapendanao!!

    Hivi ni kweli kuwa upendo wangu nilitakiwa kumuonyesha matha tu tena kwa kumpa maua na kadi?

    La! Sidhani kama ni upendo ule ambao nilitakiwa kuuonyesha… hivi ina maana mdogo wangu kule kijijini yakitokea mafuriko ama janga lolote lile ni nani atamsaidia wakati mimi nipo mbali.

    “Mungu unayeishi naenda kuazimisha siku ya wapendanao nishike mkono baba…” nilisema kwa sauti ya chini kisha upesi nikakimbia na kuingia katika mkondo ule wa maji, ebwana eeh! Maji yana nguvu sana jama.

    Yalinichukua na kunitupa mbali, nikatapatapa huku na kule nikajaribu kuweka ujuzi wangu wa kuogelea lakini haikuwa kama ambavyo inakuwa nikiwa naogelea katika mito ama nikiwa katika sweeming pool. Yale maji yalikuwa na kasi sana. Ndani ya sekunde chache tu yalikuwa yameniingia puani na mdomoni.

    Sasa maji yalianza kunisukuma kuelekea mbele. Nikapata muda wa kujiuliza kuwa kama mimi mtu mzima yale maji yamenichukua namna ile vipi kuhusu yule mtoto si yawezekana yamemuua tayari.

    Lakini wazo lile ni kama kuna mtu nisiyemuona aliniambia nilifute na kuendelea mbele.

    Kwa wakati ule sikuamini kama ingeweza kuwa ni sauti kutoka kwa yule Mungu mkuu niliyemuomba kabla ya kuingia ndani ya ule mkondo mkubwa wa maji.

    Ni baadaye sana ndipo nilitambua vile.

    Nilizidi kusukumwa na maji, hatimaye nikawa napambana ili niosipoteze uhai, hali ilikuwa mbaya sana. Nilijaribu kukata maji kwa kutumia mikono na miguu lakini haikuwezekana kila nilipojaribu maji yalinizidi na kunitupa upande mwingine.

    Nikiwa katika kukata tamaa katika ile siku ya wapendanao nikafanikiwa kumuona yule mtoto akiwa amenasa katika tawi la mti, nilijaribu kuogelea lakini maji yalinizuia, nikajaribu zaidi na zaidi lakini bado haikuwa sawa.

    Ni hapo nikakumbuka kumuita yule ambaye nilimuaga kuwa naenda kwenye maji!!

    “Mungu… nikiendelea kutumia nguvu na akili zangu za kibinadamu najua nitakufa, siwezi kupambana na maji haya baba. Siwezi hata kidogo, mtazame yule mtoto usinitazame mimi baba. Mtazame yle mtoto yule yule katika tawi….” Nilizungumza huku nikijaribu kurusha miguu huku na kule.

    Kama hujawahi kupata ajali ya kusombwa na maji usije kuiweka katika orodha ya vifo vizuri!! Maji ni mabaya sana, endelea kuyanywa, endelea kuyaoga na kuyatumia uwezavyo lakini usiombe maji yakiamua kukumeza.

    Nikiwa nahangaika bado, mbele yangu ilipita miili ya akina mama na watoto ikiwa imepoteza uhai kwa kuitazama tu!!

    Ni kitu gani hiki jamani? Nilijiuliza huku akili yangu ikikumbuka kujuta kwa nini niliamua kuingia katika maji yale. Lakini ule haukuwa wakati wa majuto!!

    Nilifanya tena jitihada, sasa nilivua suti yangu, nikabaki na pensi. Aisee kwenye maji hata kitambaa tu cha mkononi ni kizito sana na kinaweza kukuzamisha.

    Nilipovua nguo zile nikajisikia kuwa mwepesi sana, na hapo nikajaribu kupambana na yale maji. Nikajaribu hadi nikamkaribia yule mtoto ambaye sikujua kama yu mzima ama amekufa!!

    Nilipomgusa tu mara lile tawi likakatika, maji yakamchukua.

    Nikamng’ang’ania kwa nguvu zote asiweze kuniponyoka ilikuwa kazi ngumu, sikutaka yeye anywe maji na wakati huohuo nilitakiwa kukwepa kuendelea kunywa maji!!

    Nikiwa katika kuhangaika kule mara maji yaliongezeka kasi na kunizidi nguvu kiujumla.

    Sikumuachia yule mtoto!!

    Maji yakatusomba na sikukumbuka kitu kingine tena giza nene likatanda……



    ____



    Fahamu zilikuja kurejea nikiwa sijui hata mahali nilipokuwa…. Nilipofumbua macho na kuyafikicha nilikutana na rangi nyekundu.

    “Mama anko ameamka!!” sauti ya kitoto ilisikika.

    Na mara kitanda kikazungukwa na na wanawake wawili, wakasaidiana kunipa pole nikashindwa cha kujibu, wakanieleza kwa kifupi kilichotokea na kubwa zaidi wakanishukuru kwa kumuokoa mtoto yule. Ambaye walielezea kuwa baba yake alisombwa na mafuriko na kukutwa akiwa mfu lakini mtoto alikutwa yu mikononi mwangu akiwa anapumua!!

    Mtoto yule aliona harakati zangu zote za kumsaidia!!

    Alisimulia vyema hata nilivyokuwa nimevisahau.

    Baada ya hayo yule mtoto alinipatia UA JEKUNDU kisha akanibusu katika paji la uso, na hapo nikakumbuka kuwa ile siku ya tukio ilikuwa ni siku ya wapendanao!!!

    Naam licha ya kuvunjikia mguu, licha ya kupasuka kichwani. Nilikuwa nimemuonyesha upendo mtoto yule!!!!

    Lile UA JEKUNDU nimelihifadhi hadi siku hii ya leo, kila nikilitazama linanikumbusha kuwa upendo una thamani kubwa kuliko kitu chochote.

    Ikiwa mtu anasema anazo nguvu za kuipiga duniani mwambie kuwa upendo unazo nguvu zaidi ya hizo!!!



    JIFUNZE!! DUNIA inahitaji upendo kuliko kitu chochote kile, tafadhali ukipata dakika kadhaa za kufikiri basi fikiri juu ya upendo kwa yule ambaye uliyejiandaa kumchukia.

    Ukifanikiwa kuibadili chuki na kuwa upendo basi baada ya miaka kadhaa dunia itakuwa sehemu sahihi sana kuishi tofauti na sasa.

0 comments:

Post a Comment

BLOG