Alikuwepo mtoto
akisoma shule pamoja na wenziwe waliokuwa na umri mmoja, mtoto huyo akipenda
kwenda shuleni na akiyapenda aliyokuwa akisomeshwa, lakini alikuwa na ila mbaya
sana. Ila zake alikuwa akisinzia wakati mwalimu anaposomesha na mengi yaliyokuwa
muhimu yakimpita. Ila ya pili alikuwa akifikiri nje wakati wa darasa, ama
akifikiri kucheza mpira au kwenda sinema usiku au kwenda pwani kuogelea au
kwenda kununua vitu vya kula akitoka nje. Akipewa kazi za nyumbani alikuwa
akifanya nusu tu na nusu nyingine akifanya huko huko shuleni kwa kutazamia
vitabuni au kwenye madaftari ya wanafunzi wenziwe. Akili yake haikuwa mbaya
lakini ila hizi zilimsabibisha kuwa nyuma sana katika masomo yake kuliko
wenziwe. Mara kwa mara mtihani ukija, yaani kutazamwa wanafunzi waliofahamu
masomo yao barabara na walio bora kuliko wengine, alikuwa akipitwa sana na
wenziwe na pengine akianguka, yaani akikaa pahali pate pale pasipo na kwenda
madara ya juu. Mara moja alianguka katika chumba cha sita kwenda cha saba. Siku
hiyo alilia sana, akaenda mpaka kwao na kilio, akaulizwa analolilia akasema kuwa
amefeli, hakupasi, yaani hakwenda chumba cha juu.
Baba yake alimwambia,
'Ndio siku zote ninakunasihi uache mchezo mwingi na ujitahidi katika darasa zako
husikii, basi hiyo ndiyo faida ya mchezo. Huwezi kupasi ila ujitaabishe kweli
kweli,
hukusikia watu wanasema mtaka cha mvunguni
sharti ainame? Basi usipoinama hukipati cha mvunguni, mwanangu, na kuinama ni
kujikaza kwa kila njia. Njia zenyewe ni: Kwanza ni kumsikiliza mwalimu barabara
wakati anaposomesha, pili usilolifahamu umuulize pale pale kabla hajaendelea na
kusomesha jingine, tatu uache kufikiri cho chote kingine wakati wa masomo. Jambo
jingine ukiondoka shuleni ufanye kazi zote nyumbani ulizopewa shule, na
usizifanye ovyo ovyo, uwe na hakika kuwa unavyofanya ndivyo. Usilolifahamu
tazama maelezo zaidi katika madaftari yako, na kazi utakayoikosa, kama vile
hesabu na nyinginezo, lazima ufanye tena mpaka uzijue. Ukifanya hivi, mwanangu,
lazima utapasi kama wenzio.' Yule mtoto aliwacha mchezo wote aliokuwa nao na
akafuata maneno aliyoambiwa na baba yake. Kwa kufanya hivyo alitokea kuwa mtoto
hodari kuliko wote humo katika darasa, kwa hivyo mtihani ulipokuja alitokea wa
kwanza. Alipata karibu alama tisini katika alama mia kwa kila fundisho
lililotolewa katika mtihani. Walimu walifurahi sana na uhodari wa mtoto huyo.
Baba yake pia alifurahi kwa kuona mtoto wake alisikiliza mawaidha yake. Badala
ya mtoto huyo kwenda darasa la saba (kwani alikuwa katika darasa la sita) walimu
wake walimrukiza na kumpeleka darasa la nane kwa uhodari alioufanya wakati wa
mtihani. Walimu wake walijua kuwa sababu ya uhodari huo, yule mtoto aligombezwa
na baba yake kwa kutokupasi na kwa kufeli, basi kwa hivyo yule mtoto alijitahidi
sana hata akapata aliyokuwa akiyataka. Hapo yule mtoto alijua maana ya fumbo
mtaka cha mvunguni sharti ainame. Yaani alijua kuwa kuinama ni kutaabikia kila
jambo unalolitaka, ukikataa kuinama, yaani kujitaabisha, utakalo hulipati.
0 comments:
Post a Comment