Gari aina ya Pick Up iliyochakaa ilikuwa ikiendeshwa kwa kasi kubwa kuelekea katika Zahanati ya Kijiji cha Nanyamba kilichokuwa katika Wilaya ya Mvumero mkoani Mtwara.
Mzee Munki ambaye aliyekuwa dereva hakuonekana kujali mashimo kadhaa yaliyokuwa katika barabara hiyo mbovu iliyojaa madimbwi kadhaa ya maji yaliyosababishwa na mvua za mara kwa mara ambazo zilikuwa zikiendelea kunyesha, kitu alichokuwa akikijali kwa wakati huo ni kumfikisha Zubeda katika zahanati hiyo na kisha kujifungua.
Nyuma ya gari, Zubeda alikuwa akipiga kelele kwa maumivu makali, dalili zilionyesha alikuwa katika uchungu wa kujifungua. Wanawake wawili waliokuwa nyuma ya gari lile na Zubeda waligundua kwamba muda wowote ule kuanzia kipindi hicho Zubeda angeweza kujifungua, hivyo wakajiandaa vilivyo.
Mzee Munki hakupunguza mwendo, bado aliendelea kuendesha gari kwa kasi kubwa mpaka pale wanawake wale walipomtaka kulisimamisha gari lile. Mzee huyo akafunga breki, akateremka na mzee mwenzake aliyekuwa katika siti ya mbele pamoja naye, mzee Chanyenje ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Nanguruwe .
Safari haikutakiwa kuendelea zaidi ya hapo, walichokifanya ni kumuandaa Zubeda kujifungua tu. Kelele zake za uchungu zikawafanya wanawake wale kumwangalia kwa wasiwasi mkubwa. Baada ya sekunde kadhaa, wakamtaka kuipanua miguu yake na bi Asha kuanza kumtoa mtoto huku akimtaka Zubeda kumsukuma mtoto.
Kazi haikuwa rahisi hata kidogo, muda wote Zubeda aliendelea kupiga kelele huku akishika vyuma vya pembeni ya gari lile, alisikia maumivu makali. Bi Asha na mwanamke mwenzake wakaendelea kumzalisha.
Mtoto alianza kutoka, bado Zubeda alitakiwa kusukuma zaidi na hatimaye mtoto kutolewa. Kila mmoja akaanza kumwangalia mtoto yule, japokuwa alikuwa mdogo sana lakini tayari kuna kitu cha tofauti kikaanza kuonekana katika mwili wake, ubaya wa sura yake kiasi ambacho wote wakaanza kuangaliana kwa macho ya mshangao.
Damu zilikuwa zimetapakaa garini huku zikichuruzika mpaka chini. Zubeda hakuwa akipiga kelele tena, alikuwa kimya huku akihema kwa nguvu kama mtu ambaye alikuwa akitaka kukata roho.
Bi Asha na bi Fatuma wakamuandaa mtoto yule vizuri na kisha kumpatia Zubeda huduma ya kwanza na ya haraka sana mahali pale na kuendelea na safari ya kuelekea zahanati.
Kuanzia hapo, safari ile iliwachukua takribani dakika ishirini, wakawa wamekwishafika katika Zahanati ya Namkuku iliyokuwa katika Kijiji cha Nanyamba, kilometa sita kutoka Nanguruwe.
Mzee Munki na mzee Chanyenje wakambeba Zubeda kisha kumpeleka ndani ya zahanati ile. Bado alikuwa kwenye hali mbaya, alikuwa akiendelea kwa nguvu huku jasho jinsi likiwa linamtoka.
Manesi wa zahanati ile wakaamrisha Zubeda apakizwe kwenye machela ‘iliyochoka’ ambayo mataili yake yalionekana kama yanataka kuchomoka na kuanza kusukumwa. Baada ya kumfikisha ndani ya chumba husika, nesi mmoja akamfuata bi Asha na kisha kumtaka kumpa mtoto yule.
“Mmmh!” yule nesi alitoa mguno mara baada ya macho yake kutua usoni mwa mtoto yule.
“Vipi tena?” aliuliza bi Asha japokuwa aliijua fika sababu iliyompelekea nesi kutoa mguno wa namna ile.
“Hakuna kitu,” Nesi alijibu na kisha kumpeleka mtoto yule katika kitanda kimoja kidogo na kumlaza.
Kila nesi aliyeingia ndani ya chumba kile na kumwangalia mtoto yule alipigwa na mshangao, alionekana kuwa wa tofauti usoni mwake, alikuwa na sura mbaya mno jambo lililowashangaza hata manesi wenyewe walimwangalia.
Zahanati ile ilikuwa imewahudumia watoto wengi na tofautitofauti kutoka sehemu mbalimbali lakini kwa mtoto aliyeletwa siku hiyo alionekana kuwa tofauti kabisa. Sura yake ilikuwa mbaya mno.
“Zainabu njoo,” nesi mmoja alimuita nesi mwenzake ambaye alikuwa akipita kuelekea ofisini kwa dokta mkuu.
“Mbona umeniita kwa sauti ya chini? Kuna nini?” Zainabu aliuliza mara baada ya kumfikia nesi mwenzake.
“Umemuona yule mtoto aliyeletwa hapa?”
“Yupi?” Zainabu aliuliza.
“Aliyeletwa na watu waliokuwa hapo kwenye benchi.”
“Hapana. Amefanya nini?”
“Mmmh!”
“Mbona hauzungumzi Esta?”
“Mtoto mbaya huyo sijawahi kuona. Yaani bora amekuwa mwanaume, kwani kama angekuwa mwanamke, hata mume asingepata,” Esta alimwambia Zainabu huku uso wake ukionyesha mshangao.
“Mtoto mwenyewe yupo wapi?” aliuliza Zainabu.
“Chumba namba mbili,” alijibu Esta.
Nesi Zainabu hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuanza kuondoka na kuanza kuelekea katika chumba kile alichoambiwa huku lengo lake likiwa ni kutaka kumuona mtoto huyo aliyeelezwa kuwa na sura mbaya.
Mara baada ya kufika ndani ya chumba kile, moja kwa moja Zainabu akaanza kupiga hatua kukifuata kitanda alichokuwa amelazwa mtoto yule na kisha kumwangalia. Akapigwa na mshtuko mkubwa, mwili wake ukaanza kumsisimka kupita kawaida, hakuamini kama duniani kulikuwa na mtoto mwenye sura mbaya kama ile aliyokuwa nayo mtoto yule.
Zainabu hakutaka kuendelea kubaki ndani ya chumba kile kwani kadiri alivyomwangalia mtoto yule na ndivyo alivyozidi kuogopa, alichokifanya ni kuondoka ndani ya chumba kile. Alipofika koridoni, akakutana na Esta ambaye alikuwa akimwangalia katika mtazamo uliomaanisha kwamba alitaka kusikia kile alichokuwa amekiona.
“Mmmh!” aliguna Zainabu.
“Vipi?”
“Nimetishika sana,”
Hali ndivyo ambavyo ilivyokuwa katika kipindi hicho, taarifa za sura mbaya za mtoto yule zikaanza kutapakaa katika zahanati yote hasa kwa manesi wale ambao nao hawakuonekana kuridhika, wakaanza kuwaambia hata baadhi ya watu waliokuwa wakifika ndani ya hospitali ile. Kila mtu aliyepata nafasi ya kumuona mtoto yule alishtuka kutokana na ubaya wa sura yake.
Hata katika kipindi ambacho Zubeda alipopata nafuu na kuweza kuzungumza na kukaa kitako, alionekana kutokuamini mara baada ya kumwangalia mtoto wake usoni, hakuamini kama alikuwa amepata mtoto aliyekuwa na sura mbaya kama yule.
Ghafla, Zubeda akajikuta akianza kutokwa na machozi, kila alipokuwa akimwangalia mtoto wake, alishindwa kufahamu ni mahali gani ambapo mtoto yule alikuwa ameitoa sura ile, hakufanana na mtu yeyote katika familia au hata ukoo wao.
Japokuwa mtoto alikuwa na sura mbaya lakini mwisho wa siku Zubeda akakubaliana na kila kitu, akaukubali ukweli kwamba yule alikuwa mtoto wake, mtoto ambaye alitakiwa kumthamini, mtoto ambaye alitakiwa kumpa mapenzi ya dhati bila kujali ubaya wa sura kwa kuamini kwamba kila siku kazi ya Mungu huwa haina makosa.
Bado Zubeda aliendelea kukaa ndani ya zahanati ile, manesi walikuwa wakipokezana kuingia ndani ya chumba alichokuwepo. Japokuwa wengine walikuwa wakiingia kwa ajili ya kumpa matibabu lakini asilimia kubwa ya manesi waliokuwa wakiingia walitaka kumuona mtoto aliyezaliwa.
Mtoto yule akaonekana kituko, sura mbaya aliyokuwa nayo iliwafanya manesi wale wazidi kumshangaa huku wengi wakihisi kwamba mtoto yule alikuwa kiumbe cha ajabu kuwahi kutokea katika kijiji hicho.
Hayo yalikuwa madhara ya pombe. Kitendo cha mume wa Zubeda, Mtungulu kunywa sana pombe za kienyeji ndiyo ilikuwa sababu iliyompelekea kumharibu mtoto yule. Homoni zake zilizokuwa zikitoka ziliathiriwa kwa kiasi kikubwa na pombe hizo zilizokuwa kali.
Japokuwa manesi wengine walimcheka na kumdhihaki lakini Zubeda hakutaka kumtenga mtoto wake, kila siku asubuhi alikuwa akimbeba na kumnyonyesha bila kujali maneno ya watu waliokuwa wakiongea.
Kwake, sura ya mtoto wake ilikuwa nzuri, alimpenda kwa mapenzi yote, alimthamini huku akimshukuru Mungu kwa kumpa mtoto mzuri kama alivyokuwa mtoto huyo wa kiume.
“Issa,” alisema Zubeda.
Hilo ndilo lilikuwa jina la mtoto wake. Kila alipokuwa akimwangalia, aliuhisi moyo wake kuwa katika mapenzi mazito ya mtoto wake, ubaya wa sura yake haukuonekana machoni mwake, kila alipokuwa akimwangalia, alimuona mtoto kuwa ‘handsome’ zaidi ya watoto wote.
Sifa za ubaya wa sura ya mtoto Issa zikaanza kusambazwa vijijini, kila aliyesikia taarifa kuhusiana na sura ya mtoto huyo alitamani kwenda katika zahanati hiyo na kujionea kwa macho yake mwenyewe.
Hilo ndilo lililotokea, baada ya siku mbili, watu wengi walikusanyika nje ya zahanati hiyo kwa ajili ya kumuona mtoto huyo. Issa alikuwa akitisha lakini hilo wala halikumfanya mama yake, bi Zubeda kupunguza mapenzi aliyokuwa nayo juu yake, bado alimpenda na kumthamini kama mtoto wake.
Mpaka Zubeda anaruhusiwa kurudi nyumbani, tayari kijiji kizima cha Nanguruwe kilishapata taarifa kuhusu Issa.
Kitendo cha Zubeda kuteremka kutoka katika gari la mzee Munki, tayari wanakijiji walikuwa wamemzunguka huku kila mmoja akitaka kumuona Issa. Ni kweli, Issa alikuwa na sura mbaya kiasi ambacho watu waliendelea kumshangaa zaidi kwani hakukuwahi kuzaliwa mtoto aliyekuwa na sura mbaya kama aliyokuwa nayo Issa.
Bado taarifa za Issa ziliendelea kusambazwa kama upepo. Ndani ya siku tano tu, mkoa mzima wa Mtwara walikuwa wakifahamu kwamba kulikuwa na mtoto mwenye sura mbaya aliyezaliwa katika Kijiji cha Nanguruwe.
“Nimesikiasikia tu kuna mtoto mbaya, hivi ni kweli?” aliuliza jamaa mmoja aliyetoka Mtwara Mjini, alikuwa mahali hapo kwa ajili ya kumuona mtoto Issa.
“Yeah! Yupo. Huyo mtoto ni mbaya mno, ukimuona tu unaweza kukimbia,” alisema jamaa mwingine, alikuwa mwenyeji wa kijiji hicho.
“Naweza kumuona wapi?”
“Katika nyumba ile kule.”
“Ipi?”
“Ile iliyozungukwa na watu wengi” aliuliza mwenyeji huyo.
“Kumbe ndiyo ile?”
“Hiyohiyo.”
Jamaa huyo akaondoka na kwenda katika nyumba ile. Bado watu walikusanyika, kila siku ilikuwa ni lazima watu wafike ndani ya nyumba hiyo kwa ajili ya kumuona Issa.
Kile alichokiona ndicho alichokisikia kutoka kwa watu mbalimbali. Hakukuwa na uhitaji wa mtoto Issa kufikisha siku arobaini ndiyo watu waanze kumuona, ndani ya siku chache tu tayari kila mtu alikuwa amemuona Issa.
Maneno ya wanakijiji yaliuchoma moyo wa Zubeda, kitendo cha watu kusema kwamba alikuwa amezaa mtoto aliyefanana na nyani kilimuumiza mno mpaka kufikia hatua ya kutaka kuhama kijiji hicho.
Mtungulu hakuonekana kujali, pombe ndicho kitu kilichoonekana kuwa cha maana sana katika maisha yake. Ujio wa mtoto wake wala haukuweza kubadilisha ratiba yoyote ile, kila siku alikuwa akiamka na kuelekea katika klabu cha pombe kwa ajili ya kuiburudisha nafsi yake.
Jukumu la kumlea Issa lilikuwa kwa Zubeda, yeye ndiye alikuwa kila kitu kwa mtoto huyo. Kila siku alikuwa akihakikisha kwamba anamnyonyesha na kumfanyia mambo mengine kama mtoto.
Kila siku usiku Zubeda alikuwa na kazi ya kumbembeleza Issa. Alikuwa akilia usiku mzima hali iliyogeuza kuwa kero kwa wanakijiji wengine waliokuwa wakikaa karibu na nyumba aliyokuwa akiishi.
“Mbona umezaa nyani?” lilikuwa ni swali alilouliza Mtungulu kila alipokuwa akimuona Issa.
Maneno hayo yalimuumiza mno Zubeda, hakuamini kama mume wake, Mtungulu angeweza kumuita mtoto aliyezaa naye kwamba alikuwa nyani. Zubeda hakusema kitu, kwa sababu mtoto wake alikuwa amedharauliwa na kufananishwa na mnyama, aliacha maneno hayo yaendelee kutamkwa midomoni mwa watu.
Siku zikaendelea kukatika, mtoto Issa aliendelea kukua huku maneno yakizidi kusikika kwamba kulikuwa na uwezekano kuwa mtoto huyo alitoka katika sayari nyingine, alikuwa kiumbe kingine kilichojulikana kama ‘alien.’
Miezi miwili ilipokatika, kijiji cha Nanguruwe kikawa kama sehemu ya maonyesho, mara kwa mara watalii walikuwa wakifika mahali hapo kwa ajili ya kumuona mtoto huyo. Sifa zake zilizokuwa zikisikika ndizo zilizowapelekea watu wengine kutoka katika mikoa mbalimbali na hata nchi nyingine kufika mahali hapo kwa ajili ya kumuona Issa tu.
Baada ya miezi mitatu kukatika, kuna watu zaidi ya ishirini kutoka Botswana walikuwa wamefika jijini Dar es Salaam na kuulizia mahali alipokuwa akiishi Issa.
Kundi hilo la watu likawavutia waandishi wa habari wa magazeti ya Ijumaa na Uwazi kuanza kufuatilia kuona ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea kwani hiyo haikuwa hali ya kawaida watu kutoka nchini Botswana kuja Tanzania kwa lengo la kutaka kumuona mtoto huyo.
Waandishi waliwaambia kwamba mtoto huyo hakuwa akipatikana jijini Dar es Salaambali Mtwara ambapo pia wakataka kwenda huko kwani hakukuwa na kitu walichotamani kwa wakati huo zaidi ya kumuona mtoto huyo ambaye kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo alivyovuma zaidi mkoa hadi mkoa.
Walichukua saa kadhaa kufika Mtwara, siku hiyo hawakuhangaika kwenda kijijini Nanguruwe, wakalala mjini mpaka asubuhi ya kesho yake kuelekea huko huku waandishi wa habari wakiongozana pamoja nao.
Kutokana na ubovu wa barabara walitumia saa tatu kufika kijijini hapo. Wanakijiji walionekana kushtuka kwani haikuwa hali ya kawaida idadi kubwa ya magari kuingia kijijini hapo kwa mpigo.
Watu wote hamsini wakateremka kutoka garini na kuanza kuelekea kule walipoelekezwa kwamba ndipo alipokuwa akiishi mtoto aliyekuwa na sura mbaya, Issa. Walipofika, kitu cha kwanza wote kwa pamoja wakapiga magoti chini, wakaongea maneno kadhaa na kisha kuomba kuingia ndani.
Kwa msaada wa waandishi wa habari kutoka katika magazeti hayo ya burudani na habari za uhakika, walikuwa wakitafsiri kila neno lililokuwa likizungumzwa na watu hapo mbele ya wanakijiji.
Zubeda alipotoka na kuambiwa kwamba watu hao walikuwa wametoka nchini Botswana na walikuwa wamefika kijijini hapo kwa ajili ya kumuona mtoto, wala hakuwa na pingamizi kwani kila siku watu walikuwa wakifika mahali hapo kwa ajili hiyohiyo ya kumuona mtoto.
Mzee mmoja mwenye ndevu nyingi akaingia ndani, alipomuona mtoto Issa kitandani, akapiga magoti na kuanza kumsogelea mtoto Issa, alipomfikia, akamshika na kumbeba huku machozi yakianza kumtoka.
“This is our God (Huyu ni mungu wetu)” alisema mzee yule, waandishi wa habari wakapigwa na mshangao
Kila siku Pau alikuwa mtu wa kulia tu, kitendo cha kupewa mimba na Robbin kilimpa majonzi moyoni mwake. Moyoni mwake alijuta, kitendo cha kuwa na mahusiano na Robbin kilianza kumletea matatizo maishani mwake.
Kichwa chake kilimfikiria Chifu Khama III ambaye alijitahidi kila siku kumpa wosia kuhusu wanaume. Pamoja na kuambiwa mambo mengi kuhusu wanaume, kupigwa mikwara ya kila namna lakini leo hii alikuwa amepata mimba, tena mimba ya Mzungu, mmoja wa watu wasipendwa ndani ya kijiji hicho kutokana na kuileta dini ya Kikristo.
Hakukuwa na mtu aliyejua kile kilichoendelea zaidi ya Pau na Robbin. Siku zilikatika, mimba hiyo haikujificha tena kwani mara baada ya kufikia miezi kadhaa, tumbo lake likaanza kuonekana, kila mmoja akagundua kwamba Pau alikuwa mjauzito.
Mimba yake ikazua gumzo kijijini hapo, Chifu Khama III akakasirika na kujiona mpumbavu kwa kujitahidi kumzuia msichana huyo lakini mwisho wa siku kulikuwa alipata mimba.
Kutokana na hofu aliyokuwa nayo, Pau hakuendelea kuishi ndani ya kijiji hicho, alichokifanya siku moja usiku ni kukimbia na kuelekea kusipojulikana huku nyuma akiwa ameacha gumzo kubwa juu ya mvulana ambaye alimpa ujauzito ule.
***
Chifu Khama III alikuwa na hasira, hakuamini kama kweli juhudi zake za kumchunga na kumpiga mikwara msichana Pau hazikufanikiwa na mwisho wa siku kupewa mimba na mwanaume ambaye mpaka kufikia kipindi hicho hakujulikana.
Hilo, kwake likaonekana kuwa dharau kubwa, kila wakati alipokuwa akikaa, alikuwa mwingi wa hasira, kitendo alichokifanya Pau kilimkasirisha mno.
Chifu Khama III akawa kama mbogo aliyejeruhiwa, hata alipokaa na wake zake saba aliowaoa bado chifu huyo alionekana dhahiri kuwa na hasira. Kuna kipindi chifu huyo hakutaka kufanya kitu chochote kile, alikuwa akimfikiria msichana Pau na ujinga wake alioufanya.
Alichokifanya Chifu Khama III ni kuwaweka wapelelezi wake kwa ajili ya kuchunguza mwanaume aliyehusika kumpa mimba Pau. Hiyo haikutosha, kila siku chifu aliondoka na kuelekea msituni na kuanza kumuomba mungu mti ili afanikishe kumtajia mtu aliyehusika na mimba ile.
Kila alichokifanya kiligonga mwamba, japokuwa alitumia siku kumi na nne lakini bado haikuwezekana kabisa kumfahamu mtu aliyehusika na mimba ile kitu kilichomchanganya chifu.
“Umutitou nhuluo? (Mmmefikia wapi?)” aliuliza chifu huku akionekana kuwa na hasira.
“Umukhama Ubhibhito (Hatukufanikiwa mkuu)” alijibu mmoja wa wapelelezi aliokuwa amewatuma kumtafuta mwanaume aliyehusika na ujauzito ule.
Chifu Khama III akashusha pumzi ndefu, jibu alilopewa lilimchanganya kichwa chake, akasimama na kuanza kutembea huku na kule. Fimbo yake haikutoka mkononi mwake japokuwa mara kwa mara alikuwa akiipigapiga chini.
Alichokifanya ni kutoka ndani ya chumba kile huku akiwaacha wapelelezi wake wakiwa wametulia tu. Kwa muonekano wake tu, Chifu Khama III alikuwa radhi kufanya kitu chochote kile ili mradi kumpata mwanaume aliyesababisha hayo yote.
Ndani ya dakika tano, chifu akarudi chumbani humo na kuwataka wapelelezi wake waondoke huku yeye akibaki chumbani humo akijifikiria ni kitu gani alitakiwa kukifanya ili kumpata mhusika huyo.
****
Mawingu mazito yalitanda angani hali iliyoonyesha kwamba muda wowote ule mvua kubwa ingenyesha. Wanakijiji waliokuwa wameanika mazao yao kama karanga na mihogo, wakaanza kuyaanua na kuyaingiza ndani.
Hazikupita dakika nyingi, upepo mkali ukaanza kuvuma. Kila mwanakijiji alionekana kuwa na wasiwasi kwani upepo uliokuwa ukivuma kwa wakati huo haukuonekana kuwa wa kawaida hata kidogo.
Nyumba zilizokuwa na nyasi zikaanza kuachwa wazi huku nyumba nyingine zikiangushwa na upepo huo. Kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo upepo ule ulivyozidi kuvuma zaidi hali iliyowatia hofu wanakijiji wengi.
Mvua kubwa ikaanza kunyesha huku ikiambatana na upepo mkali. Kila mtu akaanza kuogopa kwani kwa jinsi hali ilivyoonekana na ukubwa wa mvua ile, hakukuwa na dalili za kuzuia mafuriko kukikumba kijiji kile.
Nyumba ya Chifu Khama III ambayo ilikuwa na paa kubwa alilopewa kama zawadi na Wazungu kutoka Uingereza baada ya kuwapa kilo zaidi ya mia mbili za dhahabu likaondolewa na upepo mkali ambao uliambatana na mvua hiyo kubwa.
Miti ikaanza kung’oka msituni na kuingia ndani ya kijiji hicho, hali hiyo ya hatari ilionyesha dhahiri kwamba kungekuwa na maafa makubwa zaidi ambayo yangeendelea kutokea ndani ya kijiji hicho.
Si upepo mkali wala mvua kubwa ambayo iliacha, vyote kwa pamoja viliendelea kuja kwa pamoja kitu kilichoendelea kuwatia hofu watu wa kijiji hicho.
Mvua hiyo na upepo viliendelea kwa takribani masaa mawili, vikaacha huku kukiwa na maafa makubwa yaliyokiacha kijiji hicho kwenye hali mbaya.
Wanakijiji wakaanza kutoka kwenye nyumba zao, matawi ya miti ilikuwa imejikusanya katika kila eneo la kijiji hicho, nyumba nyingi za nyasi hazikuwa katika hali ya usalama, nyingi ziliezuliwa na upepo mkubwa uliokuwa ukivuma.
Hiyo ndiyo hali iliyotokea katika kijiji hicho, kila kitu kilichokuwa kimetokea kilikuwa historia kubwa ambayo ingeweza kusimuliwa vizazi mpaka vizazi.
“Mkuu,” alisikika kijana mmoja, alimuita Chifu Khama III ambaye alikuwa katika hali ya sintofahamu huku pembeni akiwa na wazee wa kijiji hicho wakiizungumzia hali hiyo.
“Kuna nini?”
“Mungu wetu,”
“Amefanya nini?” Chifu aliuliza huku akisimama, alionekana kuwa na wasiwasi.
“Ameng’olewa,” alisema kijana huyo.
Kila mmoja akashtuka, maneno aliyosema kijana yule kwamba mungu wao mti alikuwa ameng’olewa ziliwachanganya, kwa haraka bila kupoteza muda wakasimama kwa pamoja na kuanza kuelekea msituni.
Kila mmoja alikuwa na maswali kuhusiana na maafa yaliyokuwa yametokea katika kijiji hicho mpaka kupelekea mungu waliyekuwa wakimtegemea katika kujibu sala zao kung’olewa.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika sehemu kulipokuwa na mungu wao, mti huo ulikuwa chini hali iliyomchanganya kila mtu.
Kwa miaka zaidi ya mia tano, leo hii mungu wao alikuwa ameng’olewa na upepo mkali uliokuwa umevuma huku ukiambatana na mvua kubwa.
Hicho kilikuwa kilio kikubwa, bila kutegemea, Chifu Khama III akajikuta akianza kutokwa na machozi, hilo lilikuwa pigo kubwa, tegemezi la kijiji hicho alikuwa ameng’olewa na hivyo kijiji hicho kubaki katika hali ya upweke.
Taarifa zikapelekwa katika kijiji hicho, kila aliyezikisia alilia, kijiji kizima kikawa katika hali ya majonzi.
“Mzungu,” alisema Chifu Khama III.
Mchungaji Mzungu, Antony akaonekana ndiye alikuwa tatizo kubwa kijijini hapo. Chifu Khama III hakutaka kuendelea kujifikiria kwamba nani alikuwa chanzo cha tatizo hilo kubwa, huku akionekana kuchanganyikiwa, yeye na wazee wa kijiji kile wakaanza safari ya kumfuata mchungaji huyo.
Nyusoni walionekana kuwa na hasira, macho yao yalikuwa mekundu huku meno yao yakiwa yanagongana kutokana na hasira kali walizokuwa nazo.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika katika sehemu iliyotengwa kwa ajili ya mchungaji huyo, wakaifuata nyumba yake na bila kupiga hodi wakaingia ndani ambapo wakamkuta Mchungaji Antony akiwa na familia yake wakisali.
Hawakutaka kuuliza kitu chochote kile, wakaanza kumtoa mchungaji huyo ndani ya nyumba ile. Wote kwa pamoja walionekana kuwa na hasira naye kwa kuamini kwamba huyo ndiye alikuwa chanzo cha mungu wao kung’olewa na upepo mkali ulivuma huku ukiwa umeambatana na mvua ile kubwa.
Walichokiamua wao kama wakuu wa kijiji kile ni kumfukuza Mchungaji Antony na familia yake ndani ya kijiji hicho kwani uwepo wao mahali hapo ulionekana kama laana, hawakutakiwa kuwepo.
Wanakiji walichanganyikiwa, mungu wao aliyeng’olewa akawa amekufa na hivyo watu hao kubaki bila mungu. Hayo yalikuwa ni majonzi makubwa, hawakuamini kile kilichotokea.
Baada ya miaka mingi huku kizazi mpaka kizazi kikiwa kinamuabudu mungu huyo, leo hii waliachwa ukiwa, tegemeo lao kubwa likawa limepotea na hivyo kijiji kubaki bila mungu.
Hali hiyo iliendelea kwa takribani miezi kadhaa, hapo ndipo walipoanza kusikia taarifa kwamba kulikuwa na mtoto aliyezaliwa ambaye kichwa chake hakikuwa na nywele kabisa. Mbali na hivyo, taarifa hizo zilisema kwamba mtoto huyo pia alikuwa na vidole sita katika kila mkono wake huku akiwa mweupe mno.
Hizo zilikuwa taarifa zilizowachanganya wanakijiji hao, hawakuamini kama kungekuwa na mtoto ambaye angezaliwa huku akiwa hana hata nywele kichwani na pia kuwa na vidole sita katika kila mkono, imani yao ikawatuma kwamba huyo alikuwa mungu.
Mleta taarifa akaambiwa aeleze zaidi juu ya taarifa hiyo na yeye bila kuficha akawaambia wazi kwamba mtoto huyo alizaliwa msituni na mwanamke mmoja ambaye hakuwa amemuona, mwanamke huyo alikuwa akiishi na bibi mmoja msituni.
Hakukuwa na cha kusubiri, walichokifanya ni kuanza kuelekea katika msitu huo kwa ajili ya kujihakikishia wao wenyewe. Chifu Khama III ndiye alikuwa kiongozi, alitaka kuhakikisha kwa macho yake kile kilichokuwa kimezungumzwa.
Walichukua saa tano, ndipo wakafika katika sehemu moja ndani ya msitu huo iliyozungukwa na miti mikubwa, katikati ya miti hiyo kulikuwa na nyumba moja ya nyasi, wakaanza kuisogelea na kuanza kupiga hodi, mwanamke mmoja mzee akatokea na kuufungua mlango, yeye mwenyewe alipigwa na mshangao, mbele yake alikuwa amesimama Chifu Khama III na wazee wengine wanne.
“Tumekuja kumuona mungu mwenye nguvu,” alisema Chifu Khama III.
“Mungu mwenye nguvu?”
“Ndiyo. Mungu aliyemuua mungu wetu, huyu ndiye mungu mwenye nguvu,” alisema Chifu Khama III.
Bibi yule hakutaka kubisha, alichokifanya ni kuwakaribisha watu hao ambao wakaingia ndani na kuanza kupiga hatua kitandani alipolala mtoto yule na mama yake aliyegeukia ukutani.
Walipokifikia kitanda kile, bibi yule akamchukua mtoto yule na kumkabidhi Chifu Khama III, akamchukua na kuanza kumwangalia. Mtoto alikuwa na kipara huku kwenye kila mkono akiwa na vidole sita. Wote kwa pamoja wakapiga magoti kama ishara ya kumuabudu kwa kuona kwamba mtoto huyo alikuwa mungu mpya mwenye nguvu ambaye alifanikiwa kumuua mungu wao, mti kwa ajili ya kuanzisha utawala wake mpya.
“Mungu wetu mkuu,” alisema Chifu Khama III huku naye akiwa amepiga magoti na mikononi akiwa na mtoto yule.
Huku wote wakiwa wameendelea kupiga magoti, mara mama wa mtoto yule akaamka kutoka usingizini, kitu cha kwanza kukifanya, alianza kupapasa pale alipomlaza mtoto wake, hakuwepo, alipogeuka nyuma, akapigwa na mshtuko, mtu ambaye alikuwa akimfahamu vilivyo, Chifu Khama III alikuwa amembeba mtoto wake.
Chifu Khama III alipoyainua macho yake na kumwangalia mwanamke yule, alikuwa msichana ambaye alimfahamu vilivyo, msichana aliyeikaidi amri yake ya kujitunza na hatimaye kupata mimba na kutoroka kijijini kwake, japokuwa alijitahidi kumtafuta, alimkosa.
Leo hii msichana huyo alikuwa mbele ya macho yake. Hakuwa Pau kama alivyomjua, kwa wakati huo msichana huyo alikuwa na cheo kikubwa, alikuwa ni mama mungu na hivyo alitakiwa kupewa heshima.
Watu wote waliokusanyika mahali hapo hawakujua kwamba kwa kila Mzungu aliyekuwa akizaa duniani, ilikuwa ni lazima mtoto azaliwe akiwa na upara. Kwa mtoto wa Pau, mtoto huyo alichukua vitu vingi kutoka kwa baba kwa sababu mbegu zake zilikuwa na nguvu zaidi na ndiyo maana hata kichwa cha mtoto huyo hakikuwa na nywele.
Kwa sababu waliishi katika kipindi ambacho mambo mengi hawakuwa wakiyafahamu, kila kitu cha tofauti, hasa kwa binadamu, kwao kilionekana kama uungu fulani hivyo mtu alitakiwa kuheshimiwa.
“Umututule khuilize uyukhilu (Umetuletea mungu mwenye nguvu)” alisema Chifu Khama III mbele ya Pau aliyekuwa akitetemeka kwa hofu.
****
Kitendo cha kuzaliwa binadamu ambaye walimchukulia kuwa kama mungu wao kiliwapa furaha mno, kila wakati Chifu Khama III alionekana kuwa na furaha kwani tayari waliona kwamba mwisho wa matatizo yao kijijini ulikuwa umefika.
Hakukuwa na aliyekumbuka kwamba Pau alikuwa akitafutwa baada ya kutoroka kijijini kwa sababu tu alikuwa mjauzito, hata Chifu mwenyewe hakutaka kukumbuka hilo kwani mtu huyo alikuwa amemzaa mungu, hivyo aliitwa mama mungu.
Kwanza wakamtoa hofu Pau na kumtaka ajiandae kwa ajili ya kurudi kijijini. Ndani ya dakika ishirini, Pau alikuwa amekwishajiandaa na hivyo kuanza kurudi kijijini pamoja na Chifu Khama III akiwa na wazee wale.
Kupatikana kwa mungu huyo kukawa faraja katika kijiji hicho, katika kipindi ambacho watu hao walikuwa wakiingia kijijini hapo, wanakijiji wote wakapiga magoti kama heshima kwa mungu wao.
Pau akawa amebadilika, hakuwa mchungaji tena, alikuwa ni mwanamke mwenye heshima ambaye alipewa nyumba nzuri na kutakiwa kumtunza mungu huyo ili aendelee kuwa bora na kufanya miujiza katika kijiji chao.
Kwa sababu mungu huyu alikuwa mpya, siku ya ibada haikuwa Alhamisi kama ilivyokuwa bali ilibadilishwa na kuwa Jumatano. Kila siku ya Jumatano wanakijiji walikuwa wakijikusanya nje ya nyumba hiyo na kisha kuanza kumuabudu mtoto huyo aliyepewa jina la Kitite.
Uwepo wa mungu huyo, wanakijiji kutoka vijiji vingine wakaanza kumiminika katika kijiji hicho. Ni kweli, kwa kumwangalia tu Kitite alionekana kuwa binadamu asiyekuwa wa kawaida, weupe wake, vidole vyake na upara wake uliwafanya watu kuamini kwamba alikuwa mungu.
Kwa sababu kila walichokifanya walikifanya kwa imani kubwa, mambo yao mengi yakaanza kufanikiwa. Katika kipindi ambacho hakukuwa na mvua kijijini hapo, walipoamua kumuomba mungu wao, mvua kubwa ikanyesha.
Wazungu waliendelea kumiminika kijijini kwa sababu waliambiwa na Wazungu wenzao kwamba Chifu Khama III alikuwa akitoa dhahabu nyingi endapo tu ungebadilishana naye na kitu chochote cha kijinga.
Hicho ndicho kilichowafanya Wazungu wengine kumletea vioo na vitu vingine vikiwepo bunduki ambazo kwao waliziita kuwa ni uchawi, yaani hata mtu akikaa umbali gani, ukifyatua tu mtu yule alikuwa akianguka na kufa.
Huo, kwao ukaonekana kuwa muujiza mkubwa, hawakuijua bunduki, silaha hiyo ikaonekana kuwa na thamani kubwa na hivyo Chifu Khama III kutoa kiasi kikubwa cha dhahabu kwa ajili ya kubadilishana na kupewa bunduki kadhaa.
Ilipofika mwaka 1904 wakati mungu wao, Kitite alipokuwa na umri wa miaka kumi, Chifu Khama III akafariki dunia kutokana na umri mkubwa aliokuwa nao na hivyo mtoto wake aliyezaa na mke wake wa kwanza kuwa Chifu wa kijiji hicho na kupewa jina la Chifu Khama IV.
Bado wanakijiji waliendelea kumuabudu Kitite kama ilivyokuwa kawaida yao. Kitite alikuwa Mzungu kabisa japokuwa vidole vyake sita kwenye kila mkono uliwafanya watu kuona kwamba mtu huyo alikuwa mungu wao wa kweli.
Maisha yaliendelea kama kawaida, kila siku ya Jumatano wanakijiji wa kijiji hicho na baadhi ya vijiji vya jirani walikuwa wakikusanyika mahali hapo na kumuabudu Kitite.
Wazungu walishangazwa na jambo hilo, kitu walichokuwa wakikifahamu ni kwamba Kitite alikuwa binadamu kama walivyokuwa binadamu wengine na wala hakuwa mungu kama alivyokuwa akijulikana.
Wazungu hao walijitahidi kuwaambia wanakijiji kwamba Kitite alikuwa binadamu lakini hakukuwa na mtu aliyeamini hilo, bado kwao Kitite aliendelea kuabudiwa kama kawaida.
Miaka iliendelea kusonga mbele kama kawaida. Wazungu walifika kijijini hapo na kujichukulia mali kadiri walivyotaka na hakukuwa na mtu aliyewazuia kufanya hivyo. Ilipofika mwaka 1915, mama mungu, Pau akafariki dunia huku akiendelea kuwa na siri kubwa moyoni mwake juu ya baba wa mtoto wake.
Hiyo ilionekana kuwa huzuni kwa Kitite, tukio la mama yake kufariki lilimuumiza mno. Mara kwa mara alikuwa akijifungia chumbani kwake na kulia kitu kilichoanza kuzua hofu kwamba mungu alikuwa kwenye majonzi na hivyo jambo lolote baya linaweza kutokea kijijini hapo na kwenye vijiji vya jirani.
Hapo ndipo wanavijiji walipoanza kuleta zawadi mbalimbali kwa mungu wao, hakukuwa na mtu aliyeamini kama Kitite alikuwa binadamu wa kawaida kama walivyokuwa binadamu wengine, wao walimchukulia kama mungu wao, hakuwa binadamu hata kidogo.
Siku zikaendelea kukatika, ilipofika mwaka 1930, mungu aliyekuwa akitegemewa, Kitite akafariki dunia huku akiwa na umri wa miaka thelathini na tano.
Hilo ndio likaonekana kuwa pigo kubwa kuliko mapigo yote waliyowahi kuyapata katika vijiji hivyo. Vilio vilitawala katika kila kona ya vijiji hivyo, hawakuamini kama kweli wasingeweza kumuona tena mungu huyo.
Kuanzia siku hiyo, hawakubahatika tena kupata mungu wa kumuabudu. Kila mtu aliyekuwa akizaa mtoto, alikuwa akikamilika kitu kilichomaanisha kwamba hakukuwa na uwezekano wa mungu kupatikana.
Siku zikaendelea kwenda mbele huku miaka nayo ikisonga mbele. Vizazi vilikuja na kupotea huku wakiambiwa kwamba ilikuwa ni lazima mungu apatikane kwa ajili ya kuabudiwa kijijini hapo.
Mwaka 1966, Botswana ikapata uhuru wake na kujitegemea lakini kijiji hicho hakikutaka kubadilika, kiliendelea kuwa vilevile huku kila siku wakiendelea kutega masikio yao kuona kama mungu alikuwa amezaliwa katika kijiji hicho au hata vijiji vya jirani.
Japokuwa maendeleo yalikuwa yakizidi kuongezeka lakini wanakijiji wa kijiji hicho cha Bechuana hawakuyakubali maendeleo hayo, waliendelea kuwa kama walivyokuwa kipindi cha nyuma, hawakumjua rais, mtu waliokuwa wakimfahamu alikuwa ni chifu wao tu.
Mwaka 1990, hapo ndipo walipopata taarifa kwamba kulikuwa na mtoto alizaliwa katika moja ya nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki, hawakujua ni nchi gani hivyo wakawaagiza wapelelezi wao kufanya uchunguzi wa kimyakimya.
Sifa ya mtoto huyo ilijitosheleza kabisa kuona kwamba alikuwa mungu wao waliyemsubiri kwa kipindi kirefu sana. Upelelezi uliendele huku wanakijiji wakipewa taarifa kwamba mungu wao waliokuwa wakimsubiri alikuwa amezaliwa katika nchi ya mbali na hapo hivyo ilikuwa ni lazima mungu huyo aletwe kijijini hapo.
Upelelezi ulipokamilika, taarifa rasmi zikaletwa kwamba mtoto huyo mwenye sura mbaya hata zaidi ya nyani alikuwa amezaliwa katika nchi ya Tanzania ndani ya mkoa wa Lindi. Hawakutaka kusubiri, kwa sababu kijiji kilikuwa na fedha nyingi kutokana na uuzaji wa dhahabu waliokuwa wakiufanya, wakatumwa watu wakuu wa nyumba yao ya ibada, watu zaidi ya hamsini kwa ajili ya kwenda nchini Tanzania.
Ndani ya siku mbili walikuwa wamekwishaingia ndani ya jiji la Dar es Salaam. Waandishi wa habari wakapewa taarifa juu ya ujio huo na hivyo kuanza kuelekea mkoani Lindi tayari kwa kumuona mungu wao.
Njiani walikuwa wakiimba nyimbo nyingi za kumsifu mungu wao huku wakishukuru kwamba mwisho wa matatizo ulikuwa umefika. Walichukua saa kadhaa, wakaingia mkoani Lindi katika Wilaya ya Kilwa ambapo wakaanza kuelekea katika kijiji cha Nanguruwe kwa ajili ya kumuona mungu wao.
Walisafiri kwa muda mrefu sana na hatimaye mwisho wa siku walilifika katika kijiji hicho ambapo mara baada ya kufika mbele ya nyumba aliyokuwa akiishi Zubeda na mtoto wake, Issa, wakapiga magoti na kiongozi wao kuingia ndani.
Kitendo cha kumuona mtoto Issa, mzee yule akapiga magoti na kuanza kumsogelea Issa kitandani pale, akamchukua na kisha kumbeba huku waandishi wa habari wakibaki na mshangao, hali aliyoionyesha mzee yule haikuwa ya kawaida.
“This is our god (Huyu ni mungu wetu)” alisema mzee yule maneno yaliyowafanya waandishi wa habari kushtuka, hawakuamini kama mtoto yule tayari alifanywa kuwa mungu na watu wale waliotoka nchini Botswana katika kijiji cha Bechuana.
Katika kipindi chote hicho, mzee yule alikuwa akibubujikwa na machozi kutokana na furaha kubwa aliyokuwa nayo kipindi hicho.
***
Mungu mtu alikuwa amezaliwa na katika kipindi hicho alikuwa mkononi mwake. Mzee yule mwenye ndevu nyingi alikuwa akimwangalia mtoto Issa huku machozi yakiendelea kumbubujika. Hakuamini kwamba siku hiyo alikuwa amefanikiwa kumuona mtoto ambaye bila shaka aliamini kwamba alikuwa mungu wao.
Ubaya wa sura ya Issa ukampa uhakika mzee yule kwamba mtoto huyo alikuwa mungu wao na kwa kipindi kirefu sana alikuwa akisubiriwa kwa ajili ya kuja na kuwapa tumaini kama walivyofanya miungu iliyopita.
Waandishi wa habari bado walipigwa na butwaa, hawakuamini kama duniani kulikuwa na watu wajinga kama alivyokuwa yule mzee. Walizoea kusikia kwenye televisheni na kusoma kwenye magazeti mengine kwamba kulikuwa na watu walioabudu miungu mingine ikiwepo Buddha, mungu wa Waindi wengi na Wachina.
Leo hii, kwa macho yao walikuwa wakimuona mzee huyo ambaye alimshika mtoto Issa na kwa masikio yao walimsikia akisema kwamba mtoto huyo alikuwa mungu. Nguvu za kupiga picha zikawaisha, kitendo cha mzee yule kusema kwamba mtoto Issa alikuwa mungu, mioyo yao ilikufa ganzi kwani kitu cha ajabu kilichotokea, miili yao ilisisimka mno.
Mzee yule, huku akionekana kuwa mwenye furaha kubwa, akasimama na kuanza kutoka nje huku mtoto Issa akiwepo mikononi mwake. Wale watu wengine waliokuwa nje walipomuona mzee yule akitoka ndani huku mtoto akiwa mikononi mwake, wakasujudu, wakakaa hivyo kwa dakika kadhaa na kisha kuviinua vichwa vyao.
Hapo ndipo waandishi wa habari walipopata nguvu ya kupiga picha kila kilichoendelea. Tayari wanakijiji walikusanyika mahali hapo na walifuatilia kila kitu kilichoendelea mahali hapo.
Zubeda alibaki na mshangao, kitendo cha watu wale kumsujudia mtoto wake kilimshangaza, maswali mengi yakawa kichwani mwake lakini alikuwa akisubiria kuona nini kingeendelea ili aweze kuuliza swali moja baada ya jingine.
“We have to go back home with him (Inatupasa turudi nyumbani pamoja naye)” mzee yule aliwaambia waandishi wa habari, alikuwa akihitaji msaada wa kuyatafsiri maneno yale kwa Zubeda ambaye hakuwahi kusoma hata darasa moja.
Mwandishi mmoja wa habari, Deogratius Mongela akamgeukia Zubeda na kumwambia kile mzee yule alichokisema. Zubeda alishtuka lakini hakutaka kuwaruhusu watu hao waondoke na mtoto wake.
“Haiwezekani, mtoto wangu haendi popote,” alisema Zubeda huku akianza kumchukua mtoto wake kutoka mikononi mwa mzee yule.
“This is our god, we have to take him home. Please... tell her that we need him (Huyu ni mungu wetu, tunapaswa kumpeleka nyumbani. Tafadhali...mwambie tunamhitaji)” alisema mzee yule na mwandishi kumtafsiria Zubeda.
“Nimesema sitakiiiii,” alisema Zubeda kwa sauti kubwa.
Mapenzi aliyokuwa nayo kwa mtoto wake yalikuwa makubwa, hakutaka kumwacha mtoto wake, hakutaka kusikia mtu yeyote akitaka kuondoka na mtoto wake aliyempenda. Ni kweli alikuwa na sura mbaya hata zaidi ya nyani lakini kwake mtoto huyo alionekana kuwa mzuri na alikuwa na thamani kubwa maishani mwake kuliko mtu yeyote yule.
Watu wale hawakuridhika, walikuwa wamesafiri umbali mrefu mpaka nchini Tanzania kwa ajili ya kuja kumchukua mungu wao, mtoto Issa, kitendo cha kuwaambia kwamba warudi nyumbani bila mungu wao kilikuwa ni kitu kisichowezekana hata kidogo.
“Ubumile hutujitwe bomoli uyukhilu,” (Hatuwezi kuondoka bila mungu wetu) alisema mzee yule kwa lugha ya Kisetswana.
“Utwelileti,” (Tumteke) alisema mzee mwingine.
Hicho ndicho walichokitaka, halikuwa jambo jepesi kumwachia mtoto huyo aendelee kuishi nchini Tanzania na wakati walimhitaji kijijini kwao na kumfanya kuwa mungu wao.
Kijiji kiliharibika, kwa kipindi kirefu sana kulikuwa na mambo mengi yaliyotokea, kwao, mambo hayo yote yalionekana kuwa kama laana, kitendo cha kutokuwa na mungu wa kumuabudu ndicho kilichoonekana kuleta mambo hayo yote.
Leo walikuwa wamefika katika kijiji hicho na hatimaye kumkuta mtoto waliyeamini kwamba ndiye alikuwa mungu wao pekee ambaye kwa kipindi kirefu walimsubiri.
Uamuzi wa kumteka mtoto huyo ukapitishwa kwani hawakutaka kurudi Botswana bila mungu wao. Walichokifanya, wakajifanya kuaga huku wakikubaliana na matokeo kwamba walikuwa wameshindwa kumchukua mungu wao.
Muda wa kuondoka kurudi Dar es Salaam, watu arobaini na nane walikwenda lakini wazee wawili walibaki kwa ajili ya kukamilisha mchakato mzima wa kumteka Issa.
Huo ndiyo mpango walioupanga na kitu kilichokuwa kimebaki ni utekelezaji wa jambo hilo tu. Zubeda hakujua kilichokuwa kikiendelea, muda wote alikuwa amemkumbatia mtoto wake hali iliyoonyesha kwamba hakutaka mtu yeyote amchukue kutoka mikononi mwake.
“Mbona unamwangalia mtoto kwa hasira hivyo?” aliuliza Zubeda mara baada ya kumuona mume wake akimwangalia mtoto Issa kwa macho yaliyojawa na hasira.
“Simpendi sana,” alijibu Mtungulu.
“Humpendi mtoto wako?”
“Ndiyo. Yaani anatisha sana. Huyu si mtoto wangu,” alisema Mtungulu.
Maneno hayo yalimuumiza Zubeda, hakuamini kama kweli mume wake huyo angeendelea kumchukia mtoto aliyezaa naye. Zubeda hakuongea kitu, japokuwa maneno yale yalimuumiza mno lakini akaamua kuyapuuzia na kubaki na maumivu yake moyoni mwake.
Usiku huo, Zubeda alikuwa amelala huku akiwa amemkumbatia mtoto wake. Matungulu hakuwepo ndani ya chumba hicho, kila alipomwangalia mtoto wake, Isaa, moyo wake ulijawa na hasira kali.
Kila wakati alitamani kumuua mtoto huyo, hakumpenda hata mara moja na alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile kwa ajili ya kumtoa mtoto mbele ya uwepo wake. Huku akiwa na mawazo tele, akakumbuka kitu, alichokifanya, tena kwa haraka sana, akaondoka kwenda sehemu fulani huku tabasamu pana likiwa usoni mwake.
“Afadhali...ni lazima nifanye hivi, hakika nitafanikiwa na atatoka mbele ya uso wangu milele,” alisema Matungulu huku akipiga hatua za harakaharaka kwenda sehemu, alijiona akichelewa, kuna kipindi alitamani kupaa ili afike haraka.
****
Mtu aliyehitajika kwa wakati huo alikuwa ni mtoto Issa pekee. Watu kutoka Botswana waliobaki ndani ya Kijiji cha Nanguruwe walitakiwa kuhakikisha wanafanya kila liwezekanalo mpaka mtoto huyo mwenye miezi sita, Issa anatekwa na hivyo kurudi naye Nchini Botswana.
Kazi haikuwa nyepesi, kila wakati watu hao walijifikiria juu ya kile walichotakiwa kukifanya kwani kwa kila hatua waliyotakiwa kuichukua, hawakutakiwa kugundulika.
Ujio wa watu wale ndani ya kijiji hicho zilisambazwa kwa kasi mpaka katika vijiji vingine na kufika Mtwara Mjini, wengi waliosikia kwamba watu hao walikuwa wamekuja kwa ajili ya kumchukua mtoto Issa na kuondoka naye kwa kuwa alikuwa mungu wao kiliwashangaza.
Kwa kila mtu aliyesikia kuhusu suala hilo, alibaki na mshangao, hakukuwa na aliyeamini kwamba mbali na China, India na nchi nyingine za barani Asia, pia kulikuwa na watu barani Afrika walioabudu binadamu kwa kumfanya kuwa mungu wao.
Walipoona kwamba kila kitu walichokuwa wamekipanga kisingeweza kufanikiwa, hapo ndipo walipoamua kutafuta msaada tena kutoka kwa wanakijiji wengine kwa malipo makubwa ya fedha.
Wakatafuta vijana wawili ambao walisaidiwa na kijana mwingine wa tatu katika kutafsiri Lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili. Mpango walioupanga ulikuwa ni kuhakikisha kwamba kila kitu kinafanikiwa ili waweze kurudi na mtoto Issa mpaka nchini Botswana.
Siku hiyohiyo usiku, vijana wale wakaamua kumwendea Matungulu na kumwambia mpango waliokuwa nao na kiasi cha fedha walichoahidiwa, zaidi ya shilingi laki saba.
Matungulu hakukubali, japokuwa alikuwa hampendi mtoto wake lakini suala la kumuuza kilikuwa ni kitu kingine kisichowezekana kabisa. Hapo ndipo alipokumbuka kwamba Issa alikuwa mtoto wake, hata kama alikuwa mbaya kama nyani, baso aliitwa Issa Matungulu.
“Kwa hiyo hautaki mahela yote hayo?” aliuliza kijana mmoja aliyeitwa Msuva.
“Haiwezekani kabisa. Yaani nimuuze mtoto wangu! Haiwezekani,” alisema Mtungulu huku akionekana kumaanisha kile alichokisema.
“Aisee Mtungulu. Unakataa laki saba! Duuh! Sasa wewe unataka Mungu akupe bahati gani tena?” jamaa mwingine alimuuliza swali.
“Siwezi kumuuza mtoto wangu.”
“Una uhakika gani kama yule ni mtoto wako? Wewe uso wako ni kijana handsome sana, yaani hata Mzungu anaweza kuwa na wewe, sasa mtoto ana sura ya nyani, hivi kweli ni mtoto wako yule?” aliuliza jamaa huyo.
Maneno hayo yakamfanya Mtungulu kutulia kwa muda, akaanza kujifikiria kama ingewezekana kumuuza mtoto wake au la. Alibaki katika hali hiyo kwa dakika kadhaa, aliposhtuliwa, alitoa uamuzi wake wa mwisho kwamba lisingekuwa jambo jepesi kumuuza mtoto wake.
Mtungulu hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, tayari alikwishaweka uamuzi wake kwamba kamwe hawezi kumuuza mtoto wake hata kama hakuwa akimpenda.
Siku hiyo hakutaka kwenda klabuni, maneno aliyoambiwa na vijana wale yalimpa mawazo mengi, akaondoka na kuelekea nyumbani huku kwa mtazamo tu akionekana kuwa mwingi wa mawazo.
“Kuna nini?” alimuuliza Zubeda mara baada ya kumuona mume wake akiwa mwenye mawazo mengi.
“Hakuna kitu mke wangu,” alijibu Mtungulu.
“Hapana. Niambie nini kinaendelea mpenzi, huwa haupo hivyo,” alisema Zubeda.
“Kichwa kinauma tu,” alijibu Mtungulu.
Usiku huo hakujisikia vizuri, bado kichwa chake kilifikiria mengi kuhusu ahadi ya fedha alizopewa kama angefanikisha kutekwa kwa mtoto wake.
Mtungulu aliendelea kukaa nyumbani, ilipofika saa tatu usiku, kiu kubwa ya pombe ikaanza kumkamata. Hakutaka kwenda klabu siku hiyo lakini kiu ile ikamfanya kuanza kuuona umuhimu wa yeye kuelekea katika klabu ya pombe.
Mfukoni hakuwa na fedha, alipozifikiria fedha alizoahidiwa kupewa endapo angefanikisha kutekwa kwa mtoto wake, alikiona ni kiasi kikubwa mno.
Kama kila siku alitumia shilingi mia tatu kwa kila kikombe kunywa pombe haramu ya gongo, akafikiria huku akijiuliza kwenye laki saba alizoahidiwa kupewa ilikuwa imebeba shilingi mia tatu ngapi.
Mpaka kujiuliza swali hilo, tayari aliona kulikuwa na umuhimu wa kumteka mtoto wake ili maisha yake yabadilike na kunywa pombe kadiri alivyoweza.
Mapenzi juu ya mtoto wake yakamtoka tena, kila alipomwangalia chuki iliyokuwa imeondoka ikaanza kurudi tena. Sura ya nyani ikaanza kuonekana. Kiu pamoja na ubaya wa mtoto wake, akaona lingekuwa jambo lisilowezekana kuendelea kubaki nyumbani na wakati kulikuwa na fedha za bure
Hapo ndipo alipoinuka na kuwafuata vijana wale, Msuva na wenzake. Njiani, Mtungulu alikuwa na presha kubwa, mawazo yake yalibadilika kwa asilimia mia moja, katika kipindi hicho alizitaka zile fedha ambazo angekabidhiwa endapo angefanikisha zoezi zima.
“Kwanza yule siyo mtoto wangu, mimi sijafanana na nyani hata mara moja, hata ukimwangalia mama yake na ndugu wengine, hakuna aliyefanana na nyani. Sasa atakuwaje mtoto wangu na wakati sisi wote hatujafanana na nyani?” alijiuliza Mtungulu.
Katika kila swali alilojiuliza, alijiwekea wepesi wa kujibu na kuyasapoti mawazo yake aliyokuwa amejiwekea kwamba ilikuwa ni lazima amuuze mtoto wake.
“Vipi tena?” aliuliza Msuva.
“Mzigo upo?”
“Mzigo upo. Ila mtoto atapatikana?”
“Hilo siyo tatizo. Mimi si ndiye niliyesingiziwa kuwa ni mtoto wangu, atapatikana tu,” alijibu Mtungulu.
“Poa. Twende tukamchukue.”
“Malipo kwanza,” alisema Mtungulu.
“Malipo kabla ya kazi?”
“Kazi kabla ya malipo? Acheni hizo,” alisema Mtungulu.
“Sawa. Tutakupa nusu ya malipo, ukifanikisha tunakumalizia,” alisema Msuva.
“Hakuna noma,” alisema Mtungulu.
Kilichofanyika ni kuletewa fedha hizo na kukabidhiwa mkononi. Mtungulu hakuamini kama kweli naye alikuwa ameshika shilingi laki saba. Kila alipozingalia, mawazo yake yalimkumbuka mama muuza gongo.
Kichwa chake kikajawa na taswira. Alijiona amekaa klabuni huku akiwa amezungukwa na marafiki zake ‘wakipiga maji’ huku msichana mwenye kifua cha saa sita akiwa mapajani mwake.
Kwa kiasi hicho cha fedha, Mtungulu akajiona kuwa tajiri mkubwa. Hapo ndipo wakaanza safari ya kuelekea nyumbani huku ikiwa imetimia saa tano usiku. Katika kipindi chote hicho, wote walikuwa na furaha.
Msuva na wenzake walifurahi kwani waliona wamefanikiwa kutumia fedha kumpa mtoto huyo huku Mtungulu akifurahi kwa kujiona kwamba amekuwa tajiri ghafla. Fedha kwake zilionekana kuwa na maana kuliko mtoto.
Walipofika nyumbani, Mtungulu akaanza kuufungua mlango na kuingia ndani. Vijana wale wengine wakabaki nje kwani kile kilichopangwa, tukio lilitakiwa kufanyika kwa Matungulu kuingia ndani, kumchukua mtoto na kisha kuwakabidhi watu hao.
Hilo wala halikuwa tatizo kwa Matungulu, akaingia kimyakimya na kuelekea chumbani. Katika kipindi chote alichokuwa amepanga kufanya hayo yote, moyoni hakujisikia hukumu, alijiona kuwa kawaida kabisa.
Hakumpenda mtoto wake, hakutaka kumuona tena na ndiyo maana wakati huo alitaka kumuiba na kuwagawia watu hao waliokuwa wakimtaka. Alipofika chumbani, macho yake akayapeleka kitandani, mkewe, Zubeda alikuwa amelala na mtoto Issa.
Matungulu akaanza kunyata, hakutaka kusikika kwa kuhofia kumuasha mke wake aliyeonekana kuwa kwenye usingizi mzito.
Akamshika mtoto Issa, ili kuepuka mtoto huyo kupiga kelele, akamziba mdomo na kuanza kutoka nje kwa mwendo uleule wa kunyata.
“Vipi?”
“Mzigo wenu huu hapa,” alisema Matungulu huku akiwakabidhi vijana wale mtoto wake.
Hakukuwa na muda wa kupoteza mahali hapo, kwa sababu kile walichokitaka walikwishakipata, vijana wale wakaondoka huku wakimuacha Matungulu akiondoka kivyake.
Kituo cha kwanza kilikuwa ni kwa wale watu kutoka Botswana, walipowaona vijana wale wanakuja na mtoto Issa, wakaanza kuwafuata na kuwapokea. Ilikuwa furaha kubwa kwao, hawakuamini kama kweli muda huo walikuwa wakijiandaa kurudi nchini kwao huku wakiwa na mtoto huyo ambaye kwao walimuona kuwa mungu wao.
“Tuondoke lini?” aliuliza mtu mmoja, miongoni mwa wale watu kutoka Botswana.
“Leo hiihii, ishu inavyoonekana, tukibaki mpaka asubuhi, itajulikana,” alisema mwanaume mwingine.
“Kuna usafiri usiku huu kweli?” aliuliza mwanaume mwingine.
“Sijui. Twende tu, tutajua mbele ya safari,” alisema mwanaume mwingine.
Kila kitu kilikuwa tayari, umbali kutoka hapo kijijini Nanguruwe mpaka Mtwara Mjini kulikuwa na kilometa zaidi ya thelathini, kwa maana hiyo ikaonekana kwamba wasingeweza kusafiri kwa miguu, walitakiwa kupanda gari.
“Tutaweza kupata gari kweli?”
“Hapana. Cha msingi tutembee tu.”
“Mmh! Hauoni kama ni mbali?”
“Haina jinsi, kwa leo hii, hatutakiwi kubaki hapa kijijini.”
Hicho ndicho walichokubaliana. Walijua fika kwamba wangeweza kupata tatizo endapo wangeamua kubaki kijijini hapo mpaka asubuhi. Usiku huohuo, wakaamua kuanza safari yao kuelekea Mtwara Mjini.
Kitu walichokifanya ni kuelekea mpaka katika kituo cha daladala kijijini hapo ili waweze kupata usafi wa kuelekea Mtwara Mjini ambapo huko wangepanda basi kuelekea Dar es Salaam.
Muda ulikuwa ni saa 5:15 usiku, wakaondoka kijijini hapo huku wakiwa na mtoto Issa. Ukimya ulikuwa umetawala, walipita katika njia ndogo zilizokuwa wazi huku sehemu kubwa kukiwa na giza kutokana na kukosekana kwa mwezi angani.
Njia nzima, walikuwa wakipongezekana kwa jinsi mchezo ulivyokuwa umechezwa kwani walijiona kufanikiwa kwa kila mpango waliokuwa wameupanga.
Kutoka hapo kijijini mpaka kituoni, wala hakukuwa mbali, wakafika, hakukuwa na mtu yeyote zaidi ya mlinzi aliyekuwa akilinda vibanda kadhaa vilivyokuwa hapo.
Hawakutaka kumfuata na kumuuliza, kwa sababu walikuwa wakiujua upande wa kuelekea mjini, wakaanza kuelekea huko. Haikuwa safari ndogo, kila wakati waliangalia nyuma kuona kama kulikuwa na gari linakuja ili waweze kupata lifti, lakini hakukuwa na gari lolote lile.
Walitembea na kutembea, ndani ya masaa mawili, kutokana na umri wao, walikuwa wametembea kwa zaidi ya kilometa tano, kila mmoja alikuwa hoi. Walitamani kupumzika lakini hakukuwa hawakutaka kufanya hivyo kwani kitu walichokuwa wakikitaka ni kufika mjini ambapo huko wangechukua gari na kuelekea Dar es Salaam.
Mwendo uliendelea zaidi, walipobakiza kilometa ishirini kabla ya kuingia mjini, mwanga wa gari ukawamulika kutoka nyuma, kwa harakaharaka wakageuka na kuanza kulisimamisha gari hilo ili wapate lifti na ikiwezekana wamlipe dereva huyo.
Gari lile lilizidi kusogea, lilipofika karibu yao, likasimama na mlango kufunguliwa, ilikuwa gari ndogo ya abiria, hiace. Wakaingia ndani, hakukuwa na abiria yeyote zaidi yao.
Safari ya kueleke mjini ikaendelea, kila mmoja akafurahi kwani walikuwa na uhakika wa kuingia mjini muda wowote kuanzia wakati huo. Safari iliendelea zaidi huku kila mtu akiwa kimya ndani ya gari, mtoto Issa alikuwa kwenye usingizi mzito, hakuamka wala kupiga kelele, bado aliendelea kulala kitu kilichowapa nafuu watu wale.
****
Zubeda alishtuka kutoka usingizini, akapigwa na mshangao mara baada ya kuona kwamba mtoto wake, Issa hakuwa pamoja naye. Kama mtu aliyechanganyikiwa, Zubeda akashuka kitandani, kitu cha kwanza alichokifanya ni kuyafunua mashuka yaliyokuwepo kitandani, akili yake ilimwambia kwamba inawezekana mtoto alifunikwa na mashuka hayo.
Mtoto hakuwepo, hakuridhika, akainama chini na kuanza kuangalia uvunguni mwa kitanda. Alijua fika kwamba Issa hakuwa akitambaa lakini katika kipindi hicho, kwa jinsi alivyochanganyikiwa, aliamini kwamba mtoto huyo alikwenda chini ya kitanda, huko napo hakuwepo.
Japokuwa alikuwa na usingizi, wote ukamtoka. Hakuishi hapo, alichokifanya ni kuangalia katika kila kona ndani ya nyumba hiyo, hali ilikuwa ileile, Issa hakuonekana.
Mpaka kufikia hatua hiyo, Zubeda akashindwa kuvumilia, akaanza kulia kama mtoto huku akilitaja jina Issa. Majirani waliokuwa wakimuona toka alipoanza kutafuta mtoto nje ya nyumba hiyo, wakamsogelea na kuanza kumuuliza ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.
Zubeda hakuwaficha, akawaambia ukweli kwamba alikuwa akimtafuta mtoto wake, alikuwa amelala naye lakini alipotea katika mazingira ya kutatanisha.
“Kwa hiyo ulipoamka asubuhi mtoto hakuwepo?” aliuliza jirani mmoja.
“Hakuwepo...mtoto wangu hakuwepo...uwiiiiiiii,” alisema Zubeda na kuanza kulia tena.
“Au alipotea kichawi, si wale watu walisema ni mungu wao,” alisema jirani mwingine.
Taarifa hizo zikasambazwa kama upepo, habari zilizosambazwa hazikusema kwamba Issa alikuwa amepotea tu bali ziliongezwa chumvi na kusema kwamba mtoto Issa alikuwa amepotea kimazingara.
Taarifa zikatolewa kwa mwenyekiti wa kijiji ambaye moja kwa moja akazifikisha katika kituo cha polisi waliofika mahali hapo, mtu wa kwanza kuhojiwa alikuwa Zubeda, baada ya kumaliza mahojiano, akaanza kutafutwa mume wake, Matungulu.
“Mumeo yupo wapi?” aliuliza polisi.
“Sijui....wakati mwingine huwa harudi nyumbani,” alijibu Zubeda.
“Kwa hiyo hujui mume wako yupo wapi?” aliuliza polisi.
“Labda kilabuni,” alijibu Zubeda.
Hapohapo polisi wakamtuma mtu aende katika kilabu cha pombe kwa ajili ya kumuita Matungulu. Ndani ya dakika tano, mtu huyo alirudi mahali hapo akiwa na Matungulu.
“Mtoto yupo wapi?” Lilikuwa swali la kwanza alilouliza polisi.
“Mtoto yupi?” aliuliza Matungulu huku akijifanya kushangaa, muda wote huo Zubeda alikuwa akilia kama mtoto, watu waliendelea kujazana.
****
Kila mmoja alichanganyikiwa, Matungulu waliyekuwa wakimuuliza maswali kuhusu mtoto alijifanya kutokuelewa kile kilichoulizwa mahali hapo japokuwa alifahamu kila kilichoendelea.
Hakukuwa na mtu aliyemtilia mashaka kwa sababu wote walifahamu kwamba huyo alikuwa mzazi hivyo asingeweza kufanya jambo lolote baya kwa mtoto wake pekee aliyekuwa naye.
Zubeda hakunyamaza, kila wakati alikuwa mtu wa kulia tu, uchungu mkubwa juu ya mwanae ulikuwa umemkamata, japokuwa alijua fika kwamba watu walimcheka mtoto huyo mwenye sura mbaya lakini hilo halikumfanya kumchukia mtoto wake, bado alimpenda mno.
Hakukuwa na muda wa kuchelewa, kwa sababu kila mmoja aliamini kwamba mtoto huyo bado alikuwa kijijini hapo, msako ukaanza mara moja.
Polisi huku wakisaidiana na wanakijiji wakaanza kumtafuta mtoto Issa. Katika kila nyumba, upekuzi ulifanyika kwani katika kipindi hicho hakukuwa na haja ya kumuamini mtu yeyote yule.
Taarifa za kupotea kwa Issa zikaanza kusambazwa, kila mtu aliyepata taarifa hiyo alipigwa na mshangao, lilikuwa jambo lisilowezekana kwa mtoto mdogo kama Issa kupotea katika mazingira ya kutatanisha namna ile.
“Atakuwa wapi?” jamaa mmoja aliuliza.
“Au ameibwa?”
“Haiwezekani. Nakumbuka kuna wale watu waliofika hapa na kusema kwamba alikuwa mungu, inawezekana wakawa wamemchukua,” alisema jamaa aliwaambia wenzake.
“Mmmh! Inawezekana kweli?” aliuliza jamaa mwingine.
“Kwa nini isiwezekane? Unajua kwamba kuna wengine walibaki hapa?” aliuliza jamaa huyo.
“Kuna wengine walibaki?”
“Ndiyo. Nafikiri nao wanatakiwa kutafutwa,” alisema jamaa huyo.
Tayari wasiwasi ukaanza kuwashika juu ya watu hao waliokuwa wamebaki. Walichokifanya wakawafuata polisi na kuwaambia kuhusu watu hao, kilichofanyika ni kuanza kuwatafuta kijijini hapo. Kila mtu alisema kwamba siku iliyopita waliwaona watu hao lakini siku hiyo waliwatafuta, hawakuwaona.
Hakukuwa na maswali tena, kila mmoja akaona kwamba inawezekana watu hao ndiyo waliomchukua mtoto huyo.
“Ila walimchukua vipi? Waliingiaje ndani?” aliuliza polisi maswali yaliyokosa majibu.
“Au walivunja mlango?”
“Hakuna, mlango haukuvunjwa, na kama ungevunjwa, mama yake angesikia,” alisema polisi mwingine.
“Sidhani. Nafikiri kuna kitu. Mlipomhoji mama yake alisemaje?”
“Hajui chochote kile.”
“Na baba yake?”
“Hakuwepo siku ya tukio.”
“Mmmh!”
“Nini tena?”
“Alikuwa wapi?”
“Katika kilabu cha pombe.”
Maswali waliyoulizana yalikuwa ni ya msingi mno. Ni kweli lilikuwa jambo lisilowezekana kwa mlango kufunguliwa na mtoto kuchukuliwa kirahisi, kwa namna moja au nyingine ilikuwa ni lazima mtu aliyeingia ndani alikuwa akifahamu kila kitu, mpaka chumba alichokuwa akilala mtoto.
Hapo ndipo polisi hao walipopata wazo la kumuita Matungulu kwa mara nyingine tena, wakaanza kupata wasiwasi juu yake kwa kuona kwamba inawezekana mtu huyo akawa anafahamu kitu fulani walichotaka kuambiwa.
“Unafahamu nini juu ya upotevu wa mtoto wako?” aliuliza polisi mmoja.
“Sifahamu chochote kile,” alijibu Matungulu.
“Usiku ambao mtoto wako aliibwa, ulikuwa wapi?”
“Nilikuwa kwenye kilabu.”
“Unawafahamu waliohusika na kumuiba mtoto wako?”
“Hapana. Mimi mwenyewe nimeshtuka,” alijibu Matungulu.
“Mbona macho yako yapo tofauti na hicho ukisemacho?”
“Yapo kawaida afande,” alijibu Matungulu huku kwa mbali akionekana kuwa na wasiwasi.
“Kuna kitu unakifahamu. Tunataka utuambie,” alisema polisi huyo.
Macho ya Matungulu yalionesha kila kitu kwamba kulikuwa na kitu alichokuwa akikifahamu juu ya upotevu wa mtoto wake. Polisi yule hakutaka kumuacha, aliendelea kumbana maswali mfululizo ili aeleze ni kitu gani alichokifahamu zaidi.
Kwa sababu tayari Matungulu alionekana kufahamu kitu japokuwa kukisema hakutaka kukiweka wazi, hapo ndipo walipoanza kumpa mikwara kwamba endapo asingesema ukweli aliokuwa akiufahamu basi angeanza kupewa mateso makali kituoni hapo mpaka atakapozungumza ukweli.
“Sijui chochote kile,” alisema Matungulu huku uso wake ukianza kubadilika.
“Utatuambia tu. Muingizeni show room,” alisema polisi yule na Matungulu kuingizwa.
Chumba kilikuwa na vitu vingi vya kuwapa watu mateso. Kulikuwa na rungu moja kubwa ambalo kazi yake kubwa lilikuwa ni kupiga ugoko wa watu waliokuwa wakikataa kusema ukweli, kulikuwa na ndoo ya maji huku pembeni kukiwa na taulo zito, hayo yote yalikuwa yakitumika katika kutoa mateso makali.
Mbali na vitu hivyo, pia kulikuwa na waya wa umeme ambao kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwachapa watu waliokuwa wakificha ukweli. Mbali na hayo, pia kulikuwa na kiti kilichokuwa wazi sehemu ya kukalia, hapo, mtu alikuwa akikarishwa mtupu huku korodani zikining’inia, na hizo ndizo zilizokuwa zikichapwa.
“Utasema tu. Wamesema majangili wakubwa waliokuwa maarufu kwa kuua tembo, sembuse wewe mlevi. Utasema tu,” alisema polisi mmoja ambaye kwa kumtazama tu, alionekana kumaanisha alichokisema.
Matungulu akaanza kufungwa kamba, tayari kijasho chembamba kikaanza kumtoka. Kwa kuwatazama tu watu hao waliokuwa ndani ya chumba kile, hawakuonekana kuwa na masihara hata mara moja, walikuwa mahali hapo kwa ajili ya kufanya kazi tu.
Saa kumi alfajiri, watu hao wawili walimnunua mtoto Issa wakaanza kuingia Mtwara Mjini ambapo moja kwa moja wakaelekea katika kibanda kilichokuwa na watu waliokuwa wakisubiri usafiri na kutulia.
Bado mtoto Issa alikuwa mikononi mwao, hakuwa ameamka, bado aliendelea kulala jambo lililoendelea kuwapa nafuu kwa kuona kwamba wangeweza kufika Dar es Salaam pasipo usumbufu wowote ule.
Waliendelea kusubiri huku kila mmoja akionekana kuchoka, hawakutaka kubaki mahali hapo, walichokihitaji ni kufika Dar es Salaam ambapo huko safari ya kuelekea Botswana ingeanza.
Ilipofika saa kumi na mbili asubuhi, basi la kwanza kabisa likafika mahali hapo, baadhi ya abiria waliotaka kwenda Dar es Salaam, wakasimama, wakachukua mizigo na kuanza kulisogelea basi lile na kuingia ndani.
Watu wale hawakutaka kubaki, kwa sababu walikwishasikia kwamba basi lile lilikuwa likielekea Dar es Salaam, nao wakasimama, wakalifuata, wakakata tiketi na kuingia ndani, safari ya kuelekea Dar es Salaam ikaanza huku tayari mioyo yao ikianza kuwa na amani.
Safari iliendelea kama kawaida, ndani ya saa kadhaa, wakafika Mikindani ambapo kulikuwa na foleni kubwa iliyokuwa imesababishwa na polisi walioshika mbwa ambao walionekana kufanya msako fulani.
Hali hiyo ikawashtua watu wale, wakatoa vichwa vyao dirishani kuchungulia, magari ya polisi yalikuwepo katika eneo hilo, mbwa walikuwa wakibweka, kwa jinsi hali ilivyoonekana, ilionyesha kabisa kwamba polisi hao walikuwa wakimtafuta mtoto Issa.
“Tufanye nini?” aliuliza jamaa mmoja.
“Sijajua,” alijibu mwingine huku akishusha pumzi nzito huku magari yakizidi kusogea.
****
“Subirini kwanza,” alisema Matungulu, alionekana kutetemeka japokuwa hakukuwa na baridi, kwa jinsi watu wale walivyoonekana, hakukuwa na aliyekuwa na masihara.
“Kuna kitu unataka kutueleza?” aliuliza polisi mmoja, alikuwa akikunja mikono mirefu ya shati lake.
“Mimi mtanionea bure, sifahamu chochote kile,” alisema Matungulu.
Polisi wale wakakasirika zaidi, maneno aliyoongea Matungulu yaliwakera mno. Kutokana na maelezo waliyopewa na majirani kutokana na upendo finyu alioonyesha Matungulu kwa mtoto wake, walijua kwamba mtu huyo alikuwa amehusika kwa asilimia mia moja.
Hakukuwa na mtu aliyeleta masihara, kila mmoja alionekana kuwa ‘serious’ na kile walichotaka kukifanya mahali pale. Matungulu alijua kilichoendelea, hivyo hawakutaka kumuacha.
Hapo ndipo mateso yalipoanza rasmi, Matungulu akashindwa kuvumilia, mwili wake dhoofu ulioharibiwa na pombe ukashindwa kuvumilia kabisa, akaanza kupiga keleke na kusema kwamba angesema ni nani aliyekuwa akihusika.
“Umetuchelewesha sana. Aya, tuambie,” alisema polisi mmoja.
Matungulu alikuwa akihema kwa nguvu kama mtu aliyekimbia umbali mrefu kwenye mbio ndefu. Mateso madogo aliyoyapa yalimfanya kuchoka mwili, alijiona ni bora kuzungumza ukweli kuliko kuendelea kupokea mateso makali namna ile.
“Nimemuuza mtoto,” alisema Matungulu, polisi wale wakavuta viti na kutulia.
“Umemuuza kwa nani?”
“Nimemuuzia Msuva na marafiki zake,”alisema Matungulu huku akilia kama mtoto.
“Sawa.Wapo wapi?”
“Wapo hapahapa kijijini,” alijibu Matungulu.
Hawakutaka kupoteza muda, walichokifanya polisi wale ni kutoka ofisini kwao. Safari yao iliishia hapohapo kijijini, kwa sababu walikuwa wakipafahamu alipokuwa akiishi Msuva, wakaelekea huko.
Hawakupata tabu sana, kwa sababu walikuwa wamevalia nguo za kiraia, wakamkamata Msuva na kuelekea naye kituoni. Tayari Msuva alikwishajua kile kilichoendelea, alichokiangalia ni njia za panya za kuweza kuwatoroka polisi hao.
Katika kila alilofikiria, hakupata jibu, akajikuta akifikishwa kituoni bila kuwatoroka polisi hao. Akaingizwa ndani, kitendo cha kumuona Matungulu akiwa hoi, tayari kichwa chake kilikwishamwambia ni kitu gani kilichoendelea, Matungulu aliunguza picha.
“Hatutaki maswali, tuambie mtoto yupo wapi,” alisema polisi mmoja, kwa muonekano wake tu, alionekana dhahiri kutokuhitaji maswali.
“Mtoto yupi?” aliuliza Msuva.
Kwa kitendo cha haraka na cha kushtukiza, akajikuta akipigwa kofi moja lililomyumbisha na kuanguka chini. Polisi hao hawakuwa na mchezo, walijua kile kilichowafanya kuwa ndani ya chumba kile.
“Tumekwishasema hatutaki maswali,” alisema polisi aliyemzaba kofi.
Msuva akawekwa kitini, tayari aliona kilikwishanuka ndani ya chumba hicho huku polisi wale wakitaka kufahamu ukweli juu ya kile walichokuwa wamekiuliza kuhusu mtoto.
Msuva akabaki kimya kwa muda, kichwa chake kilianza kufikiria mambo mengi. Jambo la kwanza alijiuliza ni kama ilikuwa sahihi kuwaambia kwamba alikuwa amewauzia Wabotswana wale mtoto au la.
Endapo angewaambia kwamba amewauzia basi ilikuwa ni lazima wamwambie mahali walipokuwa na kama angesema kwamba hajamuona mtoto huyo basi adhabu ingeongezeka kwa sababu kwa muonekano alionyesha Matungulu, alimtaja kwamba naye alihusika.
“Mtoto yupo wapi?” aliuliza polisi yule.
“Sijui unamzungumzia mtoto yupi,” alijibu Msuva.
“Unajifanya mbishi siyo?”
“Kivipi kaka? Nimekuja hapa mnaniuliza kitu nisichokijua, mnategemea niwajibu nini?” aliuliza Msuva.
“Unamjua huyu?” aliuliza polisi yule huku akimnyooshea kidole Matungulu.
“Najua, ni jirani yangu, mnywa gongo,” alijibu Msuva.
“Unamfahamu mtoto wake?”
“Nafikiri hakuna mtu asinyemfahamu mtoto wake,” alijibu Msuva.
“Unatujibu jeuri?”
“Hapana, nimewajibu kawaida, tena kwa nidhamu kubwa afande,” alisema Msuva.
Japokuwa alikuwa akiongea kwa kujiamini lakini kwa mbali alionekana kutetemeka kwani kwa muonekano wa kawaida tu, chumba kile hakikuonekana kuwa na amani.
Kila alipomwangalia Matungulu, alihisi kwamba endapo angediriki kudanganya, angepewa mateso makubwa lakini pia hata kama angesema ukweli, bado mateso makali yangemhusu sana.
“Ok! Tuanze kazi,” alisema polisi mmoja.
Pamoja ya kwamba ndani ya chumba kile kulikuwa na vitu kadhaa vya kuwapa mateso lakini bado kulikuwa na vitu vingine ambavyo vingetumika kama mateso ikiwa pamoja na pasi ya umeme iliyokuwa ikiwapa wakati mzito watu wasiotaka kuonyesha ushirikiano.
“Tunaanza na pasi,” alisema polisi yule huku akiichomeka pasi katika soketi ya umeme.
Japokuwa hakuwahi kupewa adhabu ya kuunguzwa na pasi lakini Msuva aliyafahamu vilivyo maumivu hayo, aliogopa kwa sababu hayakuwa maumivu ya kuja na kuisha mara moja, ilikuwa ni lazima aungue sana na mpaka ngozi kutoka.
Kwanza akaanza kumwangalia Matungulu, uso wake bado ulionesha woga kwani watu wote wa mateso walioletwa ndani ya chumba kile hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa na huruma.
“Kaka, naomba niseme ukweli,” alisema Msuva huku pasi ikiendelea kupata moto.
“Ukweli gani?”
“Juu ya mtoto.”
“Mtoto gani? Wewe si umesema hujui chochote!”
“Naomba niwaambieni ukweli.”
“Acha masihara...wewe hujui chochote kile, au hukumbuki?”
“Nilikuwa nawadanganya, najua afande, haki ya Mungu najua,” alisema Msuva.
“Aya tuambie mtoto yupo wapi?”
“Tulimuuza,” alijibu Msuva.
“Mlimuuza kwa nani?”
“Kwa Wabotswana.”
“Wapo wapi?”
“Sijui, ila walikuwa wakitaka kuelekea Dar kisha warudi kwao,” alisema Msuva.
Mpaka kufikia hapo hakukuwa na kitu kingine walichotaka kukisikia kwani walichokihitaji ni kujua ukweli juu ya mtoto huyo tu. Kwa sababu watu wenyewe walikuwa wakielekea Dar es Salaam, wakaanza kuwasiliana na polisi wote wa njiani kwa ajili ya kuhakikisha kwamba msako unafanyika katika kila gari mpaka wahakikishe kwamba mtoto huyo anapatikana.
****
Polisi wa Mikindani walipewa taarifa iliyohusu kuibwa kwa mtoto aliyejulikana kwa sura mbaya. Kwanza kila mtu aliyesikia alishangaa, hawakujua sababu zilizowapelekea hao wezi kumuiba mtoto kwani hakukuwa na mtu aliyekuwa tayari kuwa na mtoto huyo.
Walichokifanya ni kutoka katika kituo chao na kuelekea barabarani, walichokifahamu ni kwamba inawezekana wezi hao walikuwa katika safari kuelekea jijini Dar hivyo ilikuwa ni lazima wahakikishe kwamba wanakamatwa na mtoto kurudishwa kwa mama yake.
Bunduki zilikuwa mikononi mwao, walipofika barabarani, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuyasimamisha magari kisha kuanza kufanya msako wa gari mpaka gari.
Kusimamishwa kwa magari hayo kukasababisha foleni kubwa, msongamano wa magari ukawa mkubwa huku kila mtu akijiuliza sababu ya polisi hao kufanya msako huo lakini hakukuwa na mtu aliyepata jibu kwamba watu hao walihitaji nini.
“Kuna nini afande?” aliuliza dereva mmoja huku uo wake ukiwa kwenye tabasamu pana.
“Hakuna kitu.”
“Hakuna kitu?”
“Wewe subiri.”
Hakutakiwa kuambiwa mtu yeyote juu ya kile kilichokuwa kikiendelea kwa kuhisi kwamba inawezekana hao watu waliomuiba mtoto huyo kupigiwa simu na hivyo kubadilisha njia. Kila gari lililopekuliwa, liliruhusiwa na hivyo kufuata gari jingine.
“What should we do?”(Tufanye nini?) aliuliza mmoja wa wezi wale.
“We have to leave.” (Inabidi tuondoke.)
“You mean escaping?” (Unamaanisha kutoroka?)
“Yes! We must escape.” (Ndiyo! Ni lazima tutoroke)
Walichokuwa wakikifikiria ni kuondoka mahali hapo, hawakujua ni kwa namna gani wangeweza kuondoka lakini ilikuwa ni lazima kuwakimbia polisi hao ambao walizidi kusogea kule walipokuwa.
Hawakujua Lugha ya Kishwahili hivyo hawakudhani kama dereva alu utingo angeweza kuwaelewa kwani muda mwingi waliokuwa ndani ya gari hilo ni lugha ya Kiswahili ndiyo iliyokuwa ikisikika mara kwa mara.
“Where are you heading?” (Mnaelekea wapi?) aliuliza mmoja wao, kila mtu ndani ya gari lile akabaki akiwaangalia.
“Zungumza Kiswahili kaka,” alisema utingo wa gari hilo.
“Wanauliza basi linaelekea wapi,” alisema jamaa mmoja.
“Si tunakwenda Dar, kwani kuna sehemu nyingine zaidi?” alijibu utingo huku mmoja wa wale wezi akiwa ameshika simu na kufungua sehemu iliyoandikwa ‘map’ na kuanza kuiangalia Mtwara.
“Hey! Are we not heading to Mbawala?” (Hey! Hatuelekei Mbawala?)
“Mbawala! You have to go back my friends,” (Mbawala! Mnatakiwa mrudi rafiki zangu) alisema jamaa aliyeifahamu lugha hiyo.
Hawakuwa na jinsi, walichokifanya watu hao ni kuteremka na kuanza kuelekea katika upande mwingine wa magari yanayokwenda Mtwara Mjini ili kuona ni kitu gani wangetakiwa kufanya zaidi.
Kila mtu ndani ya daladala aliwaonea huruma, kila mmoja aliwasikitikia kwani walikuwa na mtoto na pia walionekana kuhangaika sana, yaani walikwishafika Mikindani, walitakiwa kurudi tena mpaka Mtwara Mjini kitu kilichoonekana kuwapotezea muda.
Kwa kuwaangalia kwa nje, haikuwa rahisi kuhisi kwamba watu hao walikuwa wezi na hata mtoto waliyekuwa wamembeba hakuwa wao bali walimuiba. Walipofika upande wa pili, wakatembea kurudi nyuma, tena kwa mwendo wa kasi, walipofika mbele, wakaona gari likija nyuma yao, wakalisimamisha.
“Please help us,” (Tafadhali tunaomba utusaidie) alisema jamaa mmoja, gari walilosimamisha lilikuwa ni la Wizara ya Misitu na Maliasili.
“What can I help you?” (Niwasaidie nini?)
“We are heading to Mbawala!” (Tunaelekea Mbawala!)
“Mbawala?”
“Yes! Can you give us a ride?” (Ndiyo! Unaweza kutusaidia usafiri?)
“No problem...lets roll,” (Hakuna tatizo...twendeni) alisema mwanaume huyo kwa Kingereza cha uswahilini.
Wanaume wale wawili wakaingia ndani ya gari lile na safari ya kurudi Mtwara kuanza mara moja. Kidogo wakashusha pumzi ndefu kwa kuona kwamba afadhali walifanikiwa kurudi mkoani Mtwara kwani vingenevyo wangeweza kukamatwa na kushitakiwa kwa kosa la kumuiba mtoto yule.
Safari iliendelea, kila mmoja alikuwa mchangamfu garini, hakukuwa na aliyekuwa kimya, walichukua saa moja na nusu na ndipo walipfika Mtwara ambapo hapo wakateremka na kuelekea katika gesti moja huku wakiwa na mtoto Issa.
Tetesi zikaanza kusikika Mtwara kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wamemuiba mtoto Issa, yule mto aliyekuwa akisifika kwa ubaya hapo Mtwara. Watu hawakuacha kushangaa, hawakujua malengo ya wezi hao kumuiba mtoto yule.
“Kuna watu kama vichaa....”
“Hahah! Hata mimi nashangaa! Au wanataka utajiri?”
Kila mtu alijiuliza maswali yasiyokuwa na majibu yoyote yale. Kilichokuwa kikiendelea, walishindwa kukielewa, wakawa wanajiuliza kama kweli watu hao waliomuiba mtoto Issa walikuwa na uhitaji naye au kulikuwa na kitu kingine.
Katika hospitali nyingi hapo Mtwara, wakinamama waliokuwa huko hawakutakiwa kuwaficha watoto wao, walitakiwa kuwaacha wazi ili watu wawaone.
Walichokifanya polisi wale mara baada ya kusikiliza maelezo ya mwanamke yule ni kurudi ndani. Wakawa na uhakika kwamba inawezekana watu hao walikuwa ndani ya hiyo gesti, hivyo wakarudi tena.
Walijitahidi kuangalia huku na kule chumbani mule lakini hawakufanikiwa kumuona mtu yeyote yule. Kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba watu hao walikuwa chumbani mule ila kitu kilichowashangaza ni kwamba hakukuwa na mtu yeyote yule.
“Hebu tutoeni vitu,” alisema polisi mmoja.
Wakaanza kufanya kazi hiyo mpaka chumba kikawa cheupe lakini hawakuona kitu chochote kile, hivyo wakavirudisha vitu vile. Hawakutaka kubaki humo ndani, walichokifanya ni kutoka na kuondoka huku wakiwa na dada yule wa mapokezi.
Walipofika kituoni, wakamuweka msichana yule sero kwani kulikuwa na mengi waliyotakiwa kujulikana siku hiyo. Muda ulizidi kwenda mbele, msichana yule aliendelea kusisitiza kwamba hakuwa akiwafahamu watu wale, walikwenda pale gesti hausi kama wateja wengine hivyo hakuwa na hofu ya chochote kile.
“Hivi hapo gesti kuna watu wanakujaga na watoto?”
“Hapana!”
“Sasa hukushangaa kuona watu wamekuja na watoto?”
“Nilishangaa ila sikuwauliza sana kwani hata Kiswahili hawajui.”
“Hawajui Kiswahili? Sasa wao wanajua lugha gani?”
“Kingereza.”
“Kwa hiyo ni Wazungu?”
“Hapana! Ni Waafrika, ila Kiswahili hawajui.”
“Sawa. Ngoja tuendelee kufuatilia.”
Wakati wapo hapo wakiendelea na mazungumzo, wakapigiwa simu na kuambiwa taarifa ambazo zilionekana kuwashangaza sana kwamba wanaume wawili waliokuwa na mtoto walitoka ndani ya gesti ile na walikuwa wakielekea kituoni.
Taarifa zile zikawashangaza kwani kama kupekua ndani ya chumba kile, walifanya hivyo tena mpaka kutoa vitu lakini hawakubahatika kuona kitu chochote kile. Hawakutaka kuzipuuzia taarifa zile, walichokifanya ni kuanza kurudi kule gesti tena kwa mwendo wa kasi kana kwamba walikuwa wakienda mkoani.
“Ni lazima tuwawahi hata kabla hawajaondoka, nasikia wanaelekea kituoni,” alisema polisi yule aliyepokea simu.
“Basi tuwahini. Ila kwa nini wananchi hawakuwaweka chini ya ulinzi?”
“Hatuwezi jua wana nini! Cha msingi twendeni...”
*****
Kelele za mtoto ziliwakasirisha, hawakutaka kujulikana kama walikuwa na mtoto, kitendo cha Issa kulia sana kiliwafanya kuweweseka kwa kuona kwamba wangeweza kukamatwa kwani tetesi za mtoto mwenye sura mbaya kuibwa ziliendelea kutapakaa kadiri muda ulivyozidi kwenda mbele.
Hawakukaa sana, mlango wa chumbani kwao ukaanza kugongwa na sauti ya msichana wa mapokezi kusikika. Hawakujua aliongea nini kwani hawakuwa wakikifahamu Kiswahili ila kwa jinsi mtoto yule alivyokuwa akilia, walikuwa na uhakika kwamba msichana huyo alitaka wamnyamazishe mtoto huyo.
Si sauti ya msichana huyo tu ilisikika bali baada ya sekunde kadhaa, kulikuwa na sauti za watu wengine zilizosikika ambazo zilionyesha ni kwa jinsi gani walikuwa wakilalamika, hivyo walichokifanya ni kumfumba mdomo mtoto Issa.
Haikusikika sauti yake tena, hata alipokuwa akilia, sauti yake ilitoka kama mguno. Hilo ndilo walilolifanya. Siku hiyo walihisi kwamba ni lazima wangekamatwa hivyo waliona kulikuwa na kitu walitakiwa kufanya hili kuwaepuka polisi.
“Tufanye nini?”
“Tusikilizie upepo kwanza, kama kuna tatizo, tutaingia kwenye dari,” alisema mmojawao.
Ndani ya chumba kile, kulikuwa na mlango wa kuingia katika dari, hawakuwa na sehemu nyingine ambayo waliifikiria zaidi ya hiyo. Baada ya dakika kadhaa mbele, wakasikia muungurumo wa gari kutoka nje, hawakutaka kujiuliza ulikuwa mlio wa gari la watu gani, hisia zao zikawaambia kwamba walikuwa polisi.
Hawakutaka kuchelewa, kwa haraka sana wakaanza kupanda katika dari kwa kubebana kisha kuufunika mfuniko wa dari lile.
Haikuchukua muda mrefu, polisi wakaingia ndani ya chumba kile, waliwasikia kule juu, hawakupiga kelele, tena katika kipindi hicho waliuziba mdomo wa Issa vilivyo kwa kuogopa kulia na hatimaye kufumwa mule darini.
Polisi wale wakaanza kupekua mpaka kutoa vitu vilivyokuwa mule ndani, kila hatua waliyokuwa wakiendelea nayo, watu wale walikuwa wakifuatilia kwa kutumia masikio yao mule darini. Polisi walipoona hawajafanikiwa, wakaondoka.
Hawakuteremka mpaka nusu saa baadaye ndipo wakashuka, wakamshika Issa vilivyo, hawakutaka kubaki mahali hapo, walichokifanya ni kuondoka ambapo huko nje, baadhi ya watu walikuwa wakiwaangalia, hawakutaka kujali, walichokifanya ni kusonga mbele. Lengo kubwa kwao kwa kipindi hicho ni kufika Msumbiji tu.
****
Barabara haikuwa nzuri, haikuwa na lami, ilikuwa na mashimoshimo, vumbi jingi lakini dereva hakutaka kuendesha kwa mwendo wa taratibu, aliendesha kwa mwendo wa kasi huku lengo lake likiwa ni kuwawahi watekaji hata kabla hawajaanza safari ya kuelekea walipokuwa wakielekea.
Japokuwa gari liliendeshwa kwa mwendo wa kasi lakini polisi wote waliokuwa mule ndani waliona gari hilo likiendeshwa kwa mwendo wa taratibu hivyo kumtaka dereva kuendesha gari lile kwa mwendo wa kasi vinginevyo wasingeweza kuwakamata watu hao.
“Kaka unazingua...”
“Kwa nini mkuu?”
“Tunasindikiza harusi au?”
“Mkuu! Mbona naendesha kwa mwendo wa kasi!”
“Spidi mita mwisho ngapi?”
“160.”
“Na wewe upo ya ngapi?”
“120.”
“Si unaona! Ndiyo maana nakwambia unazingua! Kanyaga moto bwana...” alisema kamanda wa msafara huo na kumtaka dereva yule kuongeza mwendo zaidi.
Hilo halikuwa tatizo, kilichofanyika ni kukanyaga moto hasa, baada ya dakika chache wakafika katika kituo hicho cha mabasi ambapo wakateremka na kuanza kuelekea ndani ya kituo hicho na kuwafanya watu wote kushtuka kwani hakikuwa kitu cha kawaida kwa kituo hicho kuvamiwa.
“Vipi tena?” aliuliza jamaa mmoja.
“Hata mimi sijui bro, nawaoba mwela wameshuka na kuvamia kituo, sijui wamekuja kukamata watumiaji poda!”
Polisi hawakutaka kuzungumza na mtu yeyote yule, walichokuwa wamekifuata hapo ni kuwakamata watu waliokuwa wameteka mtoto na kurudi nao kijijini kule.
“Kuna watu waliingia na mtoto humu?” polisi mmoja alimuuliza utingo wa basi moja aliyekuwa akiitia abiria.
“Wakina nani?”
“Wanaume wawili wakiwa na mtoto...”
“Mmmh! Kwa kweli sijawaona.”
“Una uhakika?”
“Ndiyo!”
Hawakutaka kuondoka, walichokifanya ni kuingia ndani ya mabasi yaliyokuwemo kituoni hapo na kuanza kuwatafuta watu hao. Kwa kila basi waliloingia na kuwatafuta mpaka uvunguni mwa viti, hawakufanikiwa kuwapata.
Watu hao walionekana kama wachawi, mara ya kwanza waliambiwa kwamba walikuwa bdabi ya gesti moja katika Mtaa wa Bandari, walipofika huko, wakaambiwa chumba walichokuwemo, wakawafuata ila cha kushangaza, hawakukuta mtu.
Hiyo ilikuwa mara ya pili, waliambiwa kwamba watu hao walikwenda kituoni hapo, bila shaka walitaka usafiri lakini kitu kilichowashangaza, walijitahidi kuwatafuta kila kona lakini hawakuwapata, kwa matukio hayo mawili, wakahisi kwamba watu hao walikuwa wachawi tu.
“Hii ni mara ya pili tunawakosa! Hawa watu wachawi!” alisema polisi mmoja.
“Hata mimi nimeanza kuhisi hivyohivyo! Hawa watakuwa wachawi tu,” alisema polisi mwingine.
Hawakuwa na jinsi, walichokifanya ni kuanza kuwauliza watu mbalimbali waliokuwa hapo kituoni, kwa kila mtu aliyeulizwa aliwaambia kwamba hawakuwaona watu hao, majibu hayo yaliwashangaza mno.
“Mimi niliwaona,” alisema mzee mmoja, polisi wote wakamsogelea.
“Wapo wapi?”
“Waliingia hapa kituoni wakiwa wamembeba mtoto!”
“Wakaelekea wapi?”
“Wakaingia kwenye basi.”
“Lipi?”
“Bijampopapompa!”
“Lipo wapi?”
“Lishasepa dakika ishirini zilizopita kuelekea Msumbiji!”
Polisi wale hawakutaka kuendelea kukaa mahali hapo, walikwishaambiwa juu ya mahali kulipokuwa na uwezekano mkubwa wa watu wao kuwepo hivyo walichokifanya ni kuingia ndani ya gari lao na kuanza safari ya kulifuata basi hilo lililokuwa likielekea Msumbiji.
“Kumbuka hatusindikizi harusi!” kamanda alimwambia dereva.
“Sawa mkuu!”
Kilichofuata ni kuanza kuliendesha gari kwa mwendo wa kasi. Polisi wote waliokuwa ndani ya gari walikuwa kwenye presha kubwa, jinsi gari lilivyokuwa likiendeshwa kwa kasi kipindi hicho kila mmoja akaona kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa maisha yao.
“Alisema basi gani vile?”
“Bijampopapompa!”
“Nahisi ndiyo lile pale mbele, lina picha ya simba nyuma.”
“Yeah!”
“Basi ongeza kasi kidogo tulifikie,” alisema kamanda na dereva kukanyaga mpaka mwisho kabisa, ikawa ni sauti ya upepo tu ndiyo inayosikika...vuuuuu...vuuuuu.
****
Kama kulia, Zubeda alilia sana lakini ukweli haukuweza kubadilika, ulibakia uleule kwamba mtoto wake hakupatikana. Hakukuwa na mtu ambaye alitokea kumchukia kama mume wake ambaye alishiriki kuibwa kwa mtoto wake, Issa aliyekuwa akimpenda sana.
Siku hizo zilikuwa ni za kulia tu, hakuwahi kuona unafuu wowote ule kwake, usingizi haukuja na sehemu kubwa ambayo alikuwa akiitembelea ni kwenye kituo cha polisi ambapo huko alikuwa akishinda kusikiliza ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea.
Polisi walimtia moyo kwamba kila kitu kingekwenda vizuri na mtoto wake angepatikana, alifarijika lakini wakati mwingine alikata tamaa baada ya kuhisi kwamba hayo yalikuwa maneno ya polisi tu ambao hawakutaka kumuona akiwa kwenye mawazo juu ya mwanaye.
“Atapatikana tu!”
“Kweli?”
“Kweli! Huwa jeshi la polisi halishindwi kitu, vumilia, atapatikana tu,” alisema polisi aliyekuwa akituoni.
Hali ilikuwa mbaya ndani ya basi lile waliloingia, kila mtu alibaki akiwaangalia, wakawa na wasiwasi kwamba kungekuwa na jambo baya ambalo lingetokea ndani ya basi hilo.
Wakajifanya kutokujali kitu chochote kile, hivyo walichokifanya ni kuendelea kukaa na yule mtoto ambaye hakunyamaza kwani alisikia njaa na tabgu jana hakuwa amekula.
Kelele zile ziliwaudhi abiria na hivyo kumwambia dereva awashushe watu hao lakini wao wenyewe hawakuwa radhi kushuka, walitaka kufika nchini Msumbiji haraka iwezekanavyo.
Basi likaondoka hapo kituoni na kuanza safari ndefu ya kuelekea nchini Msumbiji. Mtoto Issa hakunyamaza, bado aliendelea kupiga kelele tu kiasi kwamba ile kero ikaongezeka ndani ya basi lile.
Dereva hakutaka kusimama kwani tayari walikuwa wamekwishauacha mji na hivyo walikuwa wameingia porini. Safari iliendelea zaidi mpaka walipofika umbali wa kama kilometa hamsini kutoka mjini, dereva akapigiwa simu na kuambiwa kwamba kulikuwa na gari la polisi lililokuwa likija kule walipokuwa wakielekea.
Dereva hakujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea, alichokifanya ni kumwambia utingo wake kwa sauti ya juu kwamba walikuwa wakifuatiliwa na polisi.
“Unasemaje?” aliuliza utingo.
“Nasikia kuna polisi wanatufuatilia,” alijibu dereva.
“Kisa?”
“Hatujui! Ngoja nipunguze mwendo ili hao polisi wakija basi wafanye wanachokitaka,” alisema dereva yule.
“Hakuna tatizo. Ila leseni si unayo?”
“Ndiyo!”
“Passipoti?”
“Ninayo.”
“Basi hakuna noma.”
Japokuwa hawakuelewa kile kilichokuwa kikizungumzwa lakini waliposikia neno polisi, wakaanza kuwa na hofu, wakajua kwamba kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea.
Wakaanza kuwa na wasiwasi mwingi, hawakuwa tayari kuona wakikamatwa na kupelekwa jela, hivyo walichokifanya ni kuwaambia abiria wawasaidie kumwambia dereva kwamba walitaka kujisaidia haja ndogo.
“Kuna nini jamani?”
“Hawa abiria wanataka kujisaidia haja ndogo.”
“Abiria gani?”
“Nahisi ni watu wa Msumbiji, hawajui Kizungu.”
Dereva alivyosikia hilo, hakutaka kubisha sana kwani mambo ya kujisaidia njiani yalikuwa ya kawaida sana, akalipeleka basi pembeni kisha kulipaki na kuwataka watu hao wateremke kwa ajili ya kujisaidia.
Wabotswana wale walipoteremka, hawakutaka kuteremka na mtoto, walimpa mwanamke mmoja awashikie kisha wao kushuka na kwenda kwenye kichaka. Hakukuwa na abiria yeyote aliyeonekana kuwa na hofu, wote wakakuwasubiri wamalize ili warudi na kuendelea na safari yao, cha kushangaza, mpaka dakika tano zinakwisha, watu hao hawakurudi.
“Vipi tena? Wameliwa na simba au? Mbona hawarudi?” aliuliza dereva.
“Hata sisi hatujui. Hebu tukawatafute jamani, inawezekana wamepatwa na matatizo,” alisema abiria mmoja.
Wanaume wanne wakateremka na kuanza kuelekea kule porini huku lengo lao likiwa ni kuwatafuta wanaume hao. Walipofika huko, walijaribu kuangalia kila kona lakini hawakuonekana.
Kila mtu akaogopa, kitu walichojua ni kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba watu hao watakuwa wameliwa na wanyama wakali, hakukuwa na mtu aliyefikiria kwamba watu hao waliamua kuondoka na kumtelekeza mtoto Issa kwa abiria waliyemwambia awashikie.
“Hawapo bwana.”
“Hawapo?”
“Ndiyo! Hakuna mtu.”
“Sasa wamekwenda wapi?”
“Hata sisi hatujui. Hivi wale si ndiyo waliongia na mtoto?”
“Ndiyo! Na mtoto wamemuacha kwenye basi.”
Kila mmoja alionekana kushangaa, hawakuamini kile kilichokuwa kimetokea, ilionekana kuwa ngumu sana kwa mtu kusafiri na kwenda sehemu fulani, akaishia njiani na ghafla kukimbia.
Hawakujua chochote kilichokuwa kikiendelea, walichokifanya ni kulisubiri lile gari la polisi ambalo lilifika mpaka hapo, polisi waliokuwa na bunduki wakateremka na kuwafuata abiria hao walioonekana kuwa na wasiwasi.
“Kuna nini wakuu?” aliuliza utingo.
“Kuna watu tunawatafuta,” alisema kamanda wa polisi hao na baadhi ya polisi kuingia ndani ya gari.
Mule, wakaanza kuwatafuta watu waliokuwa wakiwataka, waliwatafuta kila kona lakini hawakuweza kuwapata kitu kilichowafanya kumwambia dereva juu ya watu hao.
“Kumbe ndiyo mnaowatafuta, waliondoka,” alijibu dereva.”Waliondoka? Kwenda wapi?”
Dereva akaanza kusimulia kilichotokea, polisi walikuwa kimya wakisikiliza, maelezo ya polisi yale yalionyesha kwamba walikimbiwa, hawakutaka kujali sana, walichokuwa wakikihitaji zaidi kilikuwa ni mtoto mtu, hivyo wakapewa. Walipomwangalia, alikuwa mtoto Issa, alikuwa mbaya wa sura hivyo wakamchukua na kuondoka naye.
Walipofika kituoni, wakawasiliana na polisi wa kijijini ambao ndani ya saa sita, wakafika katika Kituo cha Polisi cha Mtwara na kumchukua Issa na kurudi naye kijijini.
“Kumbe walimchukua mtoto kwa ajili ya kwenda kumwabudu!” alisema polisi mmoja.
“Unasemaje?”
“Ndiyo hivyo! Eti Mungu wao! Hii dunia hovyo kabisa.”
“Kwa hiyo walitaka kwenda kumwabudu?”
“Ndiyo! Walimhitaji kwa nguvu zote.”
“Mmh! Kweli hilo ni hitaji lenye uovu! Haiwezekani umuhitaji sana binadamu mwenzako kwa lengo la kwenda kumwabudu. Huo ni uovu kabisa, Mungu hapendi,” alisema polisi mmoja huku gari likiendelea na safari ya kuelekea kule kijijini.
*****
“Nyie ni lazima tuwapeleke mahakamani mkahukumiwe,” alisikika polisi mmoja akiwaambia Matungulu na Msuva.
“Tusamehe polisi.”
“Hakuna msamaha, hapa ni lazima aisee! Tena sanasana wewe unayemuuza mtoto wako, lazima upelekwe ukahukumiwe,” alisema polisi huyo maneno ambayo yaliwatia wasiwasi mno.
Matungulu na Msuva bado walishikiliwa na polisi kwa kosa la kumchukua mtoto Issa na kumuuza kwa Wabotswana waliofika kijijini hapo kisha kuondoka naye. Hilo lilikuwa kosa kubwa ambalo waliambiwa wazi kwamba ilikuwa ni lazima washitakiwe.
Walijaribu kuomba msamaha lakini hakukuwa na mtu aliyewasamehe, bado msisitizo wa polisi ulikuwa uleule kwamba ni lazima wafikishwe mbele ya sheria kisha kuhukumiwa kwa kosa walilolifanya.
Zubeda hakuacha kwenda kituo cha polisi, ilikuwa ni lazima kwenda mara kwa mara kwani alitaka kuona ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea. Hakutaka kuonana mume wake, alimchukia, kwa kitendo alichofanya, aliuwa radhi kuwaambia polisi kwamba alikuwa radhi mumewe kufungwa jela.
“Unasema?”
“Nipo radhi kumuona akifungwa jela.”
“Kweli?”
“Ndiyo! Sipendi kumuona tena,” alisema Zubeda huku akibubujikwa kwa machozi.
Saa sita alasiri, gari la polisi likaanza kuingia katika kituo hicho, Zubeda hakuwepo, alikishaondoka kitambo kurudi nyumbani kwake, polisi hao waliofika kituoni hapo, walikuwa na mtoto Isaa.
Wakateremka na kuelekea ndani ya gari, polisi waliokuwa kituoni hapo hawakuamini kama kweli mtoto alipatikana. Walichokifanya ni polisi kutumwa kwenda kumuita Zubeda aje kumuona mtoto wake aliyeletwa kutoka mjini.
Ndani ya dakika ishirini, Zubeda alikuwa kituoni hapo, alikuwa akihema kama mbwa kwa jinsi alivyochoka. Akachukuliwa na kuingizwa ndani ya chumba maalumu ambapo huko akakabidhiwa mtoto wake.
Alishindwa kuamini kama kweli hatimaye alimshika mtoto wake mikononi mwake, machozi yakaanza kumbubujika, alimpenda mno, alikuwa tayari kupoteza kila kitu katika maisha yake lakini si kuona mtoto wake akitoka mikononi mwake.
“Asante sana...asanteni sana,” alisema Zubeda huku akibubujikwa kwa machozi ya furaha.
Kesi ikafunguliwa kwa jalada lililoandikwa Wizi wa Mtoto ambapo baada ya siku chache wakachukuliwa na kupelekwa mahakamani. Huko, kesi ikaanza kwa kusikilizwa na baada ya miezi miwili hukumu ikatolewa kwa wote wawili kutumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani.
Ilikuwa ni kilio kikubwa kwa Mtungulu lakini hakuweza kubadilisha ukweli, uliendelea kubaki vilevile kwamba walitakiwa kutumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani.
Kwa upande wa Zubeda, aliendelea kumlea mtoto wake, hakutaka tena kuishi kwa mume wake, alichokifanya ni kujenga nyumba yake kupitia fedha ambazo alichangiwa na watu mbalimbali kwa ajili ya mtoto wake.
Maisha yake yakawa na unafuu, hakukuwa na shida kama kipindi cha nyuma. Maisha yake yakawa na furaha, yalibadilika kwani hakupata masimango kutoka kwa mume wake kama iilivyokuwa kipindi cha nyuma.
Kila kitu kilichoendelea baada ya hapo, kilikuwa ni historia ya kipekee katika maisha yake, hakukumbuka kile kilichopita, akajijenga kwa ajili ya maisha yake ya baadaye.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment