Search This Blog

Wednesday, December 21, 2022

SIKU MBAYA KAMA HII

 





    SIMULIZI YA KWELI: SIKU MBAYA KAMA HII:



    NA: George Iron Mosenya

    Kwa: Hilal Maximillian Magege



    Jua lilikuwa linazama katika namna yake ya kawaida likiuacha ule mwanga mwekundu wa mwisho ukiiaga dunia.

    Niliutazama mwanga ule na kujiuliza una maana gani kwani?

    Nilijiuliza swali lile ilimradi tu nijisahaulishe kabisa kuwa katika mizunguko yangu siku nzima nilikuwa nimefanikiwa kuingiza shilingi elfu nane. Elfu nane tu!!

    Waweza kujiuliza kuwa huenda sikuwa mtu wa kuridhika ama nina tamaa ya kupata pesa nyingi sana kwa siku.

    Lakini hapo nyumbani mdogo wangu wa kike alikuwa alikuwa akihitaji ada, mama alikuwa ni mgonjwa, ugonjwa wa mama ulikuwa umeongeza tatizo jingine. Mwenye nyumba alihitaji tuhame katika nyumba yake!!

    Alidai kuwa mama yangu anawakera wapangaji wengine!!

    Ulikuwa umebakia mwezi mmoja tu wa notisi hiyo.

    Niliendelea kuutazama ule mwanga mwekundu huku nikikumbuka kuwa ni mimi pekee nilikuwa mtoto wa kiume katika familia ile ya watoto sita akiwemo kaka yangu ambaye siwezi kumtaja kama mtoto wa kiume katika familia maana yeye kama ilivyokuwa kwa baba yangu mzazi wote walijitenga na familia katika namna nisizoweza kuzielezea. Nawe ukanielewa!!

    Naam! Nikabakia kuwa baba na mama pia kwa sababu yule mama halisi alikuwa wa kulala kitandani tu!!

    Hatimaye ule mwanga ukaondoka na kuliachia giza nafasi yake ya kila siku.

    Lile giza likaambatana na kelele nyingi sana katika hizo kelele nilisikia jina Nashon likitajwa mara kwa mara.

    Nashon gani mwingine zaidi yangu mtaani pale.

    Nikatoka mbio kukimbilia pahali kelele zilisikika.

    Naam! Kabla hata sijafika nikakutana na shuhuda mmoja, akanieleza kuwa mama yangu alikuwa ameanguka barabarani na kuvunjika mguu.

    Nilikimbia mara moja huku nikiita mama! Mama!....

    Nikafika pale barabarani, mama alikuwa kimya!!

    Kimya kabisa!!

    Nilipofika wakanipisha njia kana kwamba kuja kwangu mimi ndiyo pona pona ya mama yangu.

    Hawakujua kuwa ninayo shilingi elfu nane tu mfukoni.

    Nikajiuliza mama alikuwa ameenda wapi ilhali alijua wazi kuwa anaumwa na hatakiwi kabisa kutembea hovyo mpaka atakapopata nguvu mwilini.

    Baada ya watu kumaliza kushangaa, walianza kupungua hatimaye tukabaki watu watano tu! Majirani na rafiki mmoja.

    “Hapa itabidi ichukuliwe taksi!” alitoa wazo lile huku akionekana wazi kunirushia mimi mpira ule wa kuwajibika.

    Nikatikisa kichwa kuonyesha kukubali.

    Baada ya muda kidogo ikapita taksi, nikamuita dereva na kuzungumza naye nikamuuliza gharama ya kwenda hospitali. Akanitajia pesa mara nne zaidi ya ile niliyokuwanayo mfukoni.

    Akanitajia shilingi elfu thelathini!!

    Nitamshusha vipi hadi afikie kwenye kiasi nilichonacho.

    Nikaona nimsihi huenda atanielewa tu!!

    “Ndugu yangu na kaka yangu… najua yawezekana umeajiriwa na watakiwa kukabidhi hesabu kwa mkuu wako wa kazi lakini hapa nilipo ninazo shilingi elfu nane tu za kumfikisha mama yangu hospitali na kuhudumiwa. Yule pale chini ndiye mama yangu, ni yule ndiye kila kitu katika maisha yangu,…” kabla sijamaliza kuzungumza yule dereva alikuwa ndani ya teksi yake akaitia moto na kutoweka akiniacha mdomo wazi.

    Nilipogeukia lile giza alipokuwa mama yangu ambaye amevunjika mguu sikukuta mtu yeyote. Nikakumbuka kuwa pale mtaani baba yangu mzazi wakati anaikimbia familia alimzushia mama yangu kuwa ni mchawi. Na anamroga. Akadai kuwa hata tatizo lake la kunywa pombe ni mama alimroga ili asipate mafanikio pesa zote awe anazimalizia katika pombe!!!

    Maneno ya baba yangu yule mlevi yakawakaa watu wapuuzi, wakawa wanajiweka mbali na familia yetu.

    Nikatikisa kichwa na kufanya tabasamu hafifu, nikazipekua pesa nilizokuwanazo mfukoni.

    Bado zilikuwa ni elfu nane!!

    Nilipomfikia mama safari hii alikuwa anaweza kuzungumza japo kwa shida.

    Nikamuuliza ni kipi kilimtoa ndani, nilimuuliza kwa ukali.

    Akaniambia niiname aseme nami.

    “Nashon, mdogo wako Grace ametoa mimba… na imetoka vibaya anavuja damu huko ndani. Niache hapa wewe nenda ukampiganie mdogo wako.. hakikisha anakuwa salama Nashon!! mimi nitasaidiwa tu na Mungu wangu!!!” alimaliza kuzungumza.

    Nikajikuta nalichomoa shati ambalo awali nilikuwa nimelichomekea katika suruali yangu.

    Yaani Grace naye na shida zote zile zilizokuwa pale nyumbani akaenda kubeba mimba, halafu ametoa na sasa anavuja damu.

    Ni mjinga kiasi gani dada yangu!!!

    Ama nisimlaumu yeye, wana roho mbaya kiasi gani hawa wanaume. Mbona mimi sipo hivyo eeh!!

    Nikakimbia kuelekea nyumbani lakini ghafla nikarudi tena nikaona si sahihi kumwacha mama yangu mzazi pale japokuwa alinisihi.

    Laiti kama ningekuwa na gari langu ningewabeba wote na kuwapeleka hospitali!! Nilijisemea.

    Lakini sikuwa na gari ndugu msikilizaji, nikazitoa shilingi elfu nane zangu na kuzitazama jinsi zilivyokuwa zikinidhihaki dhidi ya matatizo yaliyokuwa mbele yangu.

    “Nashon nenda kwa mdogo wako!!” sauti ya mama ilinisihi.

    Ghafla nikaamua kufuata alichokuwa akinisihi… nikatimua mbio kuelekea nyumbani.

    Ama!! Yalikuwa makubwa kuliko kawaida.

    Nilipokelewa na kilio cha mtoto mdogo, alikuwa akilia sana. Nilipoingia nikakutana na sauti ya mama yake.

    “Ehee afadhali umekuja Nashon!! Naomba umpeleke mtoto wangu hospitali, dada yako ameenda kumlisha madamu yake huko mwanangu anaumwa tumbo… nasema ole wenu mwanangu akikutwa na mambo mabaya…” alizungumza huku akiwa amenishikia kiuno.

    Hapo hata hali ya dada sijaijua!! Nimekutana na jambo jipya.

    Nikajipekua mfukoni, yule mama akatumbua macho akitarajia kuona pesa nyingi labda.

    Nikazitoa zile shilingi elfu nane ambazo zilionyesha pia kuchoshwa na ile hali ya kuzitoa na kuzirudisha.

    Sasa elfu nane ingemfikisha wapi yule mtoto mdogo aliyekuwa analia kana kwamba amaeunguzwa na kaa la moto.

    Nikaukunja uso wangu kwa hasira na kuingia ndani. Sasa kichwa kilikuwa kinaniuma.

    Ile naondoka yule mama akanidaka shati langu.

    Asalaale! Likapasuka katikati.

    Nikalitazama kwa huzuni sana!!

    Kisha nikaingia ndani na kumkuta dada yangu akiwa hoi lakini sasa damu zilikuwa zimeacha kutoka.

    Nikawaza tena juu ya kuwa na gari!!

    Lakini sikuwa na gari nilikuwa nazo shilingi elfu nane tu!!

    Nilichoamua kufanya ni kitu kimoja tu! Kuliko kufa nikiwa nimesimama ni heri nife nikiwa nimelala.

    Nilikuwa nimezidiwa mpenzi msikilizaji. Kichwa kilikuwa kinaelekea kupasuka kwa mawazo mazito.

    Nikaingia chumbani kwangu, nikapiga goti na kuinyanyua mikono yangu juu.

    “Ewe Mungu uliye hai. Ikiwa vyema yafanye mambo haya yote yawe ndoto tu baba. Sina moyo wa kupokea hiki ninachokiona kikienda kutokea.”

    Baada ya hapo nikakifunga chumba changu!!

    Nikalala kitandani, na hapo nikapitiwa na usingizi.

    Sikujua nini kilichoendelea nyuma yangu.

    Na hatimaye lile jua lililoniaga likachomoza tena…..

    Nami nikaamkia katika SIKU MBAYA KAMA HII!!



    Nikajipekua mfukoni nikajikuta na ile shilingi elfu nane.

    Elfu nane ile haikuhitajika ili kumzika mama yangu aliyekufa akiwa palepale chini, haikuhitaji kumzika dada yangu aliyevuja damu hadi kufa wala haikuhitajika kumzika yule mtoto mdogo aliyekula damu iliyokuwa ikimtoka dada aliyekuwa ametoa mimba.

    Ajabu! Walijitokeza watu na magari yao, wakasimamia shughuli yote ile. Nayakumbuka maneno yao, walisema mama yangu alikuwa mpole mcheshi na mkarimu!!

    Nikayakariri “Mcheshi, mpole na mkarimu” .. mbona sasa hawakujitokeza ili kumsaidia!!

    Niliwatazama huku nikijiuliza walikuwa wapi wakati natapatapa na shilingi elfu nane yangu ili kuokoa uhai wa watu watatu kwa pamoja!!

    Ama hakika niliumia sana na sijawahi kuwa na siku mbaya kama hii!!!

    MWISHO

0 comments:

Post a Comment

BLOG