Search This Blog

Wednesday, December 21, 2022

MKONO WA FARAJA

 





    Katika maisha yangu sikuwahi kufikiri kuwa ipo siku nitapata chochote cha kunigusa moyo wangu hasa katika matembezi tofauti na ajali,kuibiwa,kuumia mwili au kukutana na marafiki wa zamani ambao wangenipa habari za kusikitisha. Hayo ndio niliyaona yanaweza kunitokea na kuniumiza sana moyo.



    Lakini kumbe kunamengi yamejificha katikati ya jiji na maisha ya binadamu. Sikujua kuwa kuna watu tena watoto, wanahangaika kutafuta tonge ambalo sisi tunalifagia kwa kuliona kama kipolo. Sikujua kama kuna watu wanalia kila kukicha kuhusu njaa ilihali familia zao zina-uwezo wa kuwalisha milo zaidi ya mitatu kwa siku,lakini kwa sababu ya hila za watu na ndugu wenye tamaa,wanalia njaa watu hao.

    Ni vipi tunasaidia vilio hivi ambavyo kila kukicha vinatupiwa serikali? Tunawasaidia hawa watu kwa kuwapa MIKONO YETU YA FARAJA. Kama una chochote unachoona kitafaa,wape watoto na watu hawa wa mitaani. Nasema haya kwa sababu katika tembea yangu nimekutana na mtoto ambaye anahitaji mkono huo ambao wewe ba mimi tuna uwezo wa kumpa.

    Namleta mtoto huyo kwenu kwa mwakilishi wa watoto wengine. Wewe utakayesoma mkasa huu,fanya kama wale watoto wote ndio umewatokea. Wanahitaji MKONO WAKO.

    *************

    Nakumbuka ilikuwa ni siku ya Chrismas ya mwaka 2013. Siku hiyo rafiki yangu mmoja aliniomba tukutane maeneo ya Ufukwe wa Coco au Coco Beach iliyopo jijini Dar es Salaam. Na mimi bila kinyongo nilimkubalia kwa sababu ni mtu wangu wa karibu.

    Yeye akitokea Kijitonyama na mimi nikitokea zangu Buza Temeke,wote kwa pamoja tulitakiwa kukutana Posta na safari yetu ya kwenda huko Coco ianze.



    Kwa sababu sikuwa mwenyeji sana wa maeneo yale,niliamua kuwahi saa moja kabla ya ile tuliyopanga na mwenzangu.

    Nilifika kituoni na kukaa nikimsubiri rafiki yangu yule ambaye wala sikuhangaika kumpigia simu na kumuuliza kama kisha ondoka kwa sababu nilijiwahisha mwenyewe.



    Kama wengi wenu mnavyojua eneo lile lilinavyojaa watu,sasa ilikuwa sikukuu,vuta picha mwenyewe.

    Picha ulioiona ndiyo hasa mimi nilikuwa napambana nayo maeneo yale.Watu walikuwa wengi na wengi wao walikuwa wanaelekea ufukweni.Nlifurahi mjumuiko wa watu ule kutokana na wengine kuwa wanavutia jinsi walivyokuwa wamependeza.



    Wakati nipo katika pepesa yangu ya macho huko na huko,ndipo nilishikwa mkono wangu na kwa kuwa eneo lile lilikuwa na watu wengi,nilishikwa na woga kidogo na kuhisi labda nimeshatekwa,si wajua ugenini bwana na jinsi maeneo yale yanavyosifika kwa vibaka,mawazo yakaenda huko.Ila pia nilihisi labda ni rafiki yangu kishafika ila kwa kitendo cha kunishika mkono na kuung’ang’ania kilinipa mashaka kidogo na kunifanya nigeuke kuangalia ni nani afanyaye hivyo.

    Alikuwa ni binti asiyezidi miaka kumi na mitano.Nguo na muonekano wake,alionekana ni mtoto wa mitaani.

    Nilimwangalia tena kwa macho ya swali na nadhani alitambua hilo.Alichofanya ni kusema shida yake ambayo alisema anaomba hela.Nilijisachi na kumpa mia tano na alinishukuru kwa kile.

    Upande wangu mwingine wa moyo,uliona naweza kufanya kitu ambacho wananchi wenzangu wanaweza kukufanyia kazi zaidi kuliko mimi.Hapo ndipo wazo la kutaka kujua kwa nini yupo pale,lilikuja. Na nikamwita ili nipate chochote hasa historia yake.



    Si wote wana historia zinazofanana,na ukipata atakayekupa historia yake na ukamwelewa,nadhani utakuwa umefanikiwa sana.

    Nilimchukua dada binti yule japo nilikuwa sina fedha za kutosha,ila nilijitolea kumpa chochote kama kumvuta ili anipe historia yake.



    Tulienda kwenye mgahawa mmoja na nilimpa uhuru wa kuagiza chochote atakacho wakati huo rafiki yangu alikuwa ananitaarifu kuwa anapanda usafiri wa kuja Posta.



    Binti aliagiza chakula chake na kuanza kula taratibu huku mimi nikiagiza kinyaji changu laini na kuburudika nacho taratibu huku nikichati kwa meseji na rafiki yangu yule tunayetaraji kukutana.

    Dakika kumi baadaye,alikuwa tayari kishamaliza chakula chake na hapo ndipo nilianza kumuuingia ili anipe hadithi ya maisha yake.Japo aliongea kwa haraka,ila nilipata japo taswira aliyowahi kukutana nayo mtoto yule. Aliongea mengi sana kwa haraka,ila yaliyonigusa,ndio yamefanya niandike hii kitu na kuongezea na bashasha zangu za uandishi. Si yote ambayo binti yule aliniambia na wala majina ya humu hayahusiki na binti yule. Simjui na wala sijakutana naye tena tangu siku ile.



    WANAHITAJI MKONO WA FARAJA. WAPE MKONO HUO.

    ***************

    Hakuna ajuaye raha ya wazazi kama mtoto mwenye wazazi,na hakuna ajuaye uchungu wa watoto kama wazazi. Yakupasa kuwa na furaha na tabasamu kama umepata malezi ya wazazi wako kwa ujumla,na pole sana kama hukuyapata malezi hayo kwani ni sehemu moja ya mapito kwa mwanadamu.



    Kama umepata malezi hayo ya wazazi wako na sasa umefanikiwa na wewe kuwa na familia yako,fanya kama wazazi wako walivyokufanyia. Na kama hukupata malezi hayo ya wazazi lakini sasa umefanikiwa kuwa na uwezo wa kupata familia,basi ipe familia hiyo malezi ambayo wewe ulipenda kuyapata kwa wazazi wako.

    Hapa na maana kwamba, usiwe mchoyo wa fadhila na mwenye moyo wa kisasi kwa watoto wengine kwa sababu wewe ulikosa malezi hayo ya wazazi wako. Kama uliyakosa malezi hayo kutoka kwa wazazi wako,basi usilipe kisasi kwa kuwafanyia wana wengine vivyo hivyo.



    Ongezeko la watoto wa mtaani ambao ni yatima,linazidi kuchukua nafasi kubwa sana katika dunia ya leo kuliko upungufu wa watoto hao. Sababu kubwa ya ongezeko la watoto hawa ni mimba zisizotarajiwa,dhuruma kutoka kwa ndugu,vifo vya wazazi,mimba kukataliwa,umasikini kutoka kwa wazazi,na visasi kutoka kwa baadhi ya ndugu waliopewa majukumu ya kuwalinda watoto hawa.

    ************

    HII NI HISTORIA FUPI YA MTOTO HUYO AMBAYE MIMI NIMEMUITA COLETHA.



    Anasema, katika maisha yake hakuwahi kujua maana ya shida wala karaha za maisha.

    Wazazi wake walimpenda na kumlea katika misingi iliyobora kabisa. Elimu aliyokuwa ameianza ilimfanya awe mtoto wa kipekee kabisa kuonekana katika familia ya Mzee Tunda. Kila muda aliweka mkazo kwenye masomo yake kuliko watoto wengine waliyokuwa wanaishi pale.

    Kila mara alionekana mwenye kujali zaidi shule kuliko mambo mengine ya watoto,kama kucheza magemu na michezo mingine ya watoto. Sababu hiyo ilimfanya wazazi wake wampende sana na kuzidi kumfanya malkia,kwa sababu alikuwa ni mtoto wao wa pekee.



    Anasema kuwa,baba yake alikuwa ana uwezo sana kuliko kaka yake,yaani kaka wa baba wa Coletha ambaye Coletha anamuita baba mkubwa.

    Uwezo huo ulimfanya baba Coletha kuwachukua wana wa kaka yake na kuanza kuishi nao pale nyumbani,wakati huo Coletha alikuwa ana umri wa miaka kumi tu!. Baba Coletha aliishi na wale watoto ambao wote walikuwa wa kiume kwa upendo mkubwa na amani tele hadi baadhi ya wageni au wasiyoijua ile familia wakahisi labda wale ni watoto wa Mzee Tunda,baba yake Coletha.



    Wivu wa siku nyingi uliyokuwa umemtawala kaka wa baba Coletha,ndiyo uliomtoa duniani mzee yule pamoja na mke wake. Dukuduku lililokuwa limemkaba kooni baba mkubwa wa Coletha,la kwa nini mdogo wangu ananizidi mali hadi ananilelea watoto,ndilo hilo ambalo hatimaye likatolewa kwa kumtumia majambazi na kuzidondosha zile nguzo muhimu za binti mdogo Coletha.



    Coletha aliniambia kuwa siku hiyo wakiwa ndani wamelala,mara walisikia vishindo vya watu kwenye mlango wao ambao Coletha yeye alikuwa analala na wale watoto wa baba yake mkubwa.

    Baada ya kusikiliza vizuri vile vishindo,waligundua kuwa wale ni wazazi wao wanaowalea, wanaburuzwa na majambazi yale kupelekwa sebuleni. Ni Coletha pekee ndiye alikuwa anaweza kuelewa ni nini kinachozungumziwa kwa sababu alikuwa ana umri mkubwa kiasi kuliko wale watoto wengine.

    Aliniambia kuwa wazazi wake waliomba sana msamaha,lakini wale majambazi walimwambia majigambo yake kwa kaka yake ndiyo yanampeleka kaburini.Hawakuwa na msamaha wala muda wa kusikiliza kelele za wazazi wa Coletha. Walichofanya ni kutoa bastola iliyozuiliwa sauti na kuwaondoa duniani wazazi wa Coletha kwa kuwapiga risasi za kichwani.

    Baada ya kazi hiyo kutimia,waliondoka pale nyumbani bila kuchukua kitu chochote zaidi ya roho za wazazi wale muhimu wa Coletha.

    Akiwa na shahuku ya kujua nini kimetokea kwa wazazi wake.Coletha ndiye wa kwanza kutoka na kuwaangalia ni nini kimewapata watu wale muhimu kwake.





    Ujasiri uliyomjaa moyoni hadi hivi sasa,ndiyo ujasiri uliomfanya mtoto yule kwenda hadi kwenye miili ya wazazi wake na kuanza kulia kwa uchungu huku akilazimisha kufuta damu zilizokuwa zimefunika nyuso za wazazi wake,nyuso ambazo zilikuwa na tundu moja dogo kwa mbele na moja kubwa kwa nyuma. Walikuwa wanaogopesha kuwaangalia,lakini binti yule mwenye miaka kumi,alikuwa kakaa nao bila wasiwasi.



    Kelele zile za kilio,ndizo zilizowaamsha watoto wengine na kuja kuangalia ni nini kimetokea.

    Baada ya kuona damu imetapakaa pale chini,watoto wale waliogopa sana na kurudi nyuma huku wakipiga mayowe yaliyofanya majirani kutoka na kuja kuangalia ni nini kimewakuta wana wale wadogo.



    Wengi walihamaki kukuta mtoto mdogo kama Coletha akiwa kapakata maiti zile bila uoga,lakini ni MUNGU pekee ajuaye kumpa ujasiri mwanadamu kwa namna ile. Hakuna kiumbe ambacho MUNGU kakiumba na kikakosa kukipa ujasiri wa jambo lolote. Coletha MUNGU alimuumba vile,na alithibitisha hilo baada ya hali aliyoikuta kwa wazazi wake.



    Majirani walijaribu kumtoa mtoto yule kutoka kwenye miili ya wazazi wake,lakini hawakuweza kwani mwana yule alionekana mwenye uchungu juu ya vifo vya wazazi wake,na alionekana mwenye kujali wazazi wake kuliko kitu chochote,na hiyo ni kwa sababu wazazi wake walimjali.



    Baada ya muda sana,ndipo majirani walipofanikiwa kumtoa mtoto yule kwenye miili ya wazazi wake wapendwa na wakati huo askari polisi walishapewa taarifa juu ya uvamizi huo wa majambazi kwa Mzee Tunda,baba mzazi wa Coletha.

    Baada ya Askari kufika,walifanya yanayokusudiwa kufanywa na askari yeyote duniani,na kisha wakaondoka na miili ile kwa ajili ya uchunguzi zaidi.



    Ilibainika ni majambazi ndio walifanya vile lakini haikufahamika walitumwa na nani na kwa nini. Suala hilo likawa siri ya Coletha ambaye aliogopa naye kuuawa kama wazazi wake endapo angesema alichokisikia. Nao utoto ndio hasa ulimsababisha awe kimya namna ile.



    Anasema,kaka wa baba yake au baba yake mkubwa alipopata taarifa kuwa mdogo wake kauawa ,alijifanya kama kapagawa na machozi kedekede yalitawala katika macho hadi mashavuni mwake. Kilio alichoangua baba mkubwa wake,usingedhani kama yeye ndiye muhusika wa matendo yale.

    Alilia huku akigalagala kwenye simenti iliyokauka na kutengeneza kibaraza. Lakini hayo yote Coletha aliyaona maigizo japo kuna moyo mwingine alihisi labda wale majambazi walitaja jina la kaka yake ili iwe kisingizio kwa atakayesikia.

    Labda walihisi atakayesikia yale maneno,atasema yote ili kaka yake Mzee Tunda,baba mkubwa wa Coletha achukuliwe hatua na kumfanya Coletha akose msaada kabisa,na muhisika wa kweli aje achukue mali zile na kuhamishia katika imaya yake.

    Coletha alikuta moyo wake unaenda kuamini fikra za kuwa baba yake mkubwa,alitaka kufanyiwa chezo na fitna. Zile hisia za kuona yale afanyayo baba yake mkubwa ni maigizo,zilifutika kwa muda ila zilikuja kuibuka tena mbeleni.



    “Hii ni dunia kaka yangu. Usione watu wanatembea wameweka vitambi mbele ndani ya magari mazuri,ukadhani kila kitu ni chao. Wamejaa wivu,chuki na roho ya mbaya hata wakifa hawapokelewi na yeyote huko waendapo,hata Shetani atawakataa”.Nakumbuka aliongea maneno haya yule binti mdogo. Japo alikuwa anaongea lakini hakuonekana kama kujali sana yaliyopita,cha msingi nadhani alishukuru kuwa anaishi na kuna watu wanajali uwepo wao hapa duniani.



    Anasema moyo wa mtu umefichwa na uzio wa ukuta ambao huwezi kuona ndani yake kuna nini.

    Baada ya maziko ya waazi wake,yule baba yake mkubwa alikuwa karibu sana na yeye Coletha. Kila mara alikuwa alikuwa kama faraja na kila kitu kwake. Alimpenda vya kutosha ndani ya wiki ile ya kwanza baada ya maziko.

    Alimpenda kwa sababu familia nzima ilikuwa pale nyumbani,hivyo ili kujipepea upepo wa mali zile ili ziende kwake,aliona ni kuwa karibu na Coletha huku kila mara akijidai analia sana amuonapo Coletha.

    Hisia na mambo ya mzee yule,iliufanya upepo ule wa mali kweli uende kwake. Akapewa jukumu la kuilea familia aliyoiacha Mzee Tunda,baba mzazi wa Coletha.



    Ndani ya mwezi mmoja kulikuwa kuna hali ya amani sana pale nyumbani,ila baada ya miezi mitatu ya kila kitu kukamilika. Yaani mali zile kupewa jina la Mzee yule,kaka wa Mzee Tunda na Baba Mkubwa wa Coletha,hapo ndipo mambo yalipoanza kubadilika.

    Ilikuwa kama utani pale mama yake mkubwa alipoanza kumkataza asiende shule bali abaki pale nyumbani akifanya kazi ndogo ndogo.

    “Ndiyo kaka.Ilikuwa kama utani huwezi amini. Mama akaanza kunikataza kwenda shule hadi nimalize kazi za pale nyumbani. Sikuwahi kufanya kazi hizo alizotaka na ndio maana niliona kama utani. Aliponiambia nisiende shule,mimi nilivaa sare zangu za shule na kumuomba dereva wetu anipeleke shule. Dereva alinipeleka kama nilivyotaka,lakini kimbembe nilikiona baada ya kutoka shule.

    Sijui ni nini kilichokuwa ndani ya mioyo ya watu wale,lakini nilichofanywa siku ya kwanza baada ya kujidai nunda na kwenda shule,sidhani kama kuna binadamu anaweza kufanya vile.

    Mimi nilipigwa kama mtu mzima,kumbe na miaka kumi. Nilibanwa kwenye ukuta na kukandamizwa hapo kwa dakika kama mbili.Alipotoka hapo, akaninyanyua juu kwa mikono yake yule mama kwa kunikaba shingoni. Alikuwa kama ananinyonga vile.

    Baada ya kumaliza mateso yake ambayo yalinilegeza mwili mzima,aliniachia onyo la kutofanya vile tena kwani ningefanya,angenipa adhabu zaidi ya ile”.Aliongea maneno hayo mtoto yule huku macho yake yakiwa makavu kabisa. Labda alishalia sana hivyo machozi yalikuwa hamna,siwezi jua,ila kwa upande wangu,niliumia.



    Anasema ilibidi afanye kama sheria mpya zilivyokwenda. Akaanza kudamka saa kumi na moja za asubuhi na kufanya kazi alizoambiwa azifanye wakati huo yule mfanyakazi wao wa mwanzo,alishaachishwa kazi kwa sababu ambazo hazikuwa sababu za kumfanya aachishwe kazi.



    “Kaka nilikuwa naamka saa kumi na moja,hadi saa mbili nilikuwa nimeshamaliza kazi zote na kujiandaa kwenda shule.

    Mara ya kwanza waliniacha niwe naenda na gari pamoja na watoto wao,lakini ikafika kipindi wakawa wananipa kazi za ziada,mfano tukimaliza kunywa chai,wananiambia nioshe kwanza vyombo ndio niende shule. Wakati naosha vyombo,wao wanaondoka na gari na kuniacha. Na gari likirudi,nafasi ya kupelekwa shule peke yangu inakuwa haipo.

    Nikachukua jukumu la kuanza kutembea kwa miguu kila nilipoachwa na gari. Niliimudu ile hali kwa kuwa nilikuwa napenda shule.

    Licha ya kuimudu,lakini nilikuwa nikichelewa darasani. Nilionywa sana juu ya tabia ile ya kuchelewa,lakini kamwe sikuthubutu kusema yanayonisibu kwa kuwa nilijua ipo siku yataisha.Nilijifariji kwa namna hiyo.

    Wale watoto wa baba mkubwa,nao wakajazwa maneno na wazazi wao ili wanichongee kitanzi pale shuleni. Wakawaambia walimu mimi nachelewa shule kwa kuwa silali nyumbani na nina majivuno kwa kuwa baba yangu kaniachia mali nyingi,hivyo pale shule hata nikifukuzwa,sitajali.

    Maneno hayo yakajenga chuki baina yangu na walimu. Wale wanaonifahamu waliniita na kuniuliza juu ya hilo,nilijitetea huku nikificha maovu nayofanyiwa,lakini nilibanwa sana nikaamua kusema ukweli wote wa mambo nayofanyiwa pale nyumbani.

    Ikawa kosa kubwa kuliko makosa yote niliyowahi kuyafanya katika maisha yangu”.Mtoto yule aliendelea kunielezea maneno hayo na wakati huo rafiki yangu niliyetaraji niwe naye siku ile,alikuwa karibu kufika.



    Coletha anasema baada ya kufichua ukweli wa afanyiwacho,habari hizo wakapelekewa viongozi wa shule na viongozi kwa kujidai wao ndio wao,wakapanga siku ya kwenda nyumbani kwa akina Coletha na kuongea na walezi wale wa Coletha

    “Siku hiyo mimi sina hili wala lile,mara ikagongwa hodi nyumbani.Wakafunguliwa viongozi wawili wa shule. Wakakaribishwa ndani na baba mkubwa. Ila baada ya dakika kumi na tano,zikasikika kelele za baba mkubwa zikiwafokea wale viongozi na baadaye kufukuzwa pale nyumbani. Hapo ndipo niliiona joto ya jiwe kaka yangu”.Coletha aliongea kama utani au hadithi tu!Kwani alikuwa anaongea huku anapiga makofi kama wafanyavyo wanawake wakiwa wanahadithiana mipasho ya mtaani.

    “Nakwambia kaka hee hee. Si umeona hii mikono(Huku ananionesha viganja vyake vya mikono). Si umeona kama vimeungua vile,basi mwenzako niliwekwa mikono yangu kwenye jiko la oveni,halafu baba akaikandamiza hapo kwa kutumia mwiko. Wee usiombe nakwambia. Niliumia lakini hakuona hilo. Akaanza kunichalaza kwa mwiko,hadi wale watoto wake wakaanza nao kulia.

    Nilipigwa na kumwagiwa maji ya moto huku miguuni na baadaye baba alitaka kuniunguza mdomo ili nisiseme tena,wale watoto wake ndio walikuja kumshika miguuni ili aache kufanya hivyo”.Coletha alikuwa anaongea kwa ujasiri ambao nadhani akikua kwa njia ile,watapata shida sana hawa wanaotenda haya.

    Kwa umri wake niliona kama hajitambui kuwa yale aliyofanyiwa ni mabaya mno.Ila akishajitambua kuwa yale yalikuwa ni maovu,basi Coletha anaweza kuwa mtu wa ajabu sana huko mbele.

    Nilichojaribu ni kumuhasa asije kufikiria kufanya kisasi au kuwafanyia wengine kama alivyofanyiwa yeye.

    Haina ubishi ya kuwa watoto wengi wa mtaani wamepitia makubwa.Na pale wanapojitambua kuwa walikuwa wanaonewa,ndipo nao huanza kutafuta njia za kulipa kisasi. Hapo ndipo ujikuta wanajiingiza katika makundi mabaya kama ya ujambazi,ukahaba na dhuruma kwa wanyonge wao. Na mwisho wa haya,huwa ni ongezeko la uharifu nchini.

    Tuwape mkono wa faraja watoto hawa,ushauri wako pia waweza kuwa chachu ya kuwatoa vifungoni mwa fikra chafu ambazo wanataraji kuzifanya.



    Hadi rafiki yangu anakuja pale nilipo,tayari Coletha alikuwa anasimulia jinsi alivyotoroka pale nyumbani kwao. Na rafiki yangu aliponikuta pale naongea na yule binti,alivutiwa sana hasa stori yenyewe ilivyokuwa inatolewa kiujasiri na katika hali ya kupuuzia wakati mimi msikilizaji nikiwa katika hisia za kutaka kutoka machozi



    Anasema vile vidonda vya maji na moto,wao wenyewe walivitibu kwa kumpeleka hospitali,na wakati vinaelekea kupona na yeye alikuwa anapanga kutoroka. Hadi vidonda vile vinapona,tayari alishajua wapi pa kukimbilia.

    Vilipopona ndipo alienda nyumba ya mwalimu mmoja anayemfundisha na kumweleza kila kitu juu ya maisha yake.

    Mwalimu yule aliona cha maana ni kumtoa pale Arusha na kumkimbizia Dar es Salaam kwa mdogo wake aliyekuwa anasoma chuo.

    Anasema huku Dar es Salaam,mambo yalienda vizuri kwa mwaka mmoja kwani mwalimu yule alikuwa anatuma hela za matumizi. Lakini mambo yalibadilika baada ya mwalimu yule kufukuzwa kazi.

    Msaada ukakosekana na mambo yakawa magumu. Yule dada aliyekutana naye Dar,alikuwa hana uwezo wa kulea familia kwa sababu naye alikuwa analelewa na wazazi wake.

    Ikabidi Coletha aingie mtaani rasmi. Na maisha yakaanza bila msaada huku mtaani. Na mambo ya mtaani ni mengi sana hasa inapofika usiku,lakini kishazoea.

    Hadi anamaliza hadithi yake,tayari nilishapata cha kumshauri na kwa kuwa rafiki yangu naye alikuwepo,nilimpa hadithi kwa juu juu tu! Alijiunga nami katika kuwapa watoto wale faraja.



    Tulimtuma Coletha aende kuchukua rafiki zake naye akafanya hivyo. Ndani ya dakika kumi,alikuwa kaja na watoto wenzake wa kutosha tu!.

    Namshukuru sana rafiki yangu Tinner,si kwa kuwa tu!Alikuwa anauwezo,lakini pia alikuwa anamoyo wa kutoa. Tuliwachukua watoto wale na kwenda nao hadi kwenye maduka ya mle Coco na kuwanunulia japo Ice Cleam. Walikuwa wengi na waliongezeka kadiri ya wawezavyo.

    Na kuna baadhi ya wananchi,walikuja kujumuika nasi. Huo ndio ulikuwa MKONO WETU WA FARAJA. Tuliwapa ushauri,na tuliwahasa japo sidhani kama walielewa kwa muda ule kwa sababu walikuwa katika furaha na akili ya utoto nayo naweza kusema hawakutilia maanani ushauri ule.Ila wakikua na kama wanakumbukumbu,nadhani wataufanyia kazi ushauri ule.



    TUWAPE MKONO WA FARAJA WATOTO HAWA. SI SERIKALI WALA VIONGOZI WA DINI WALA WALIMU.NI JUKUMU LETU SOTE WANANCHI.TUWAANGALIE PIA.



    Ni tungo yenye ukweli kiasi chake. Si vyote vyenye ukweli.

    Asante kwa Tinner,nitakukumbuka.

    MWISHO.



0 comments:

Post a Comment

BLOG