Search This Blog

Sunday, January 1, 2023

MKOMBOZI

 






SIMULIZI FUPI : MKOMBOZI

MTUNZI : W. LYAMBA



Katika kijiji cha Matare wilaya ya Mugumu Serengeti, bwana Wambura alikamatwa kwa kesi ya kusingiziwa na kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu.

Huku nyuma akiacha mke na watoto wanne waliokuwa wanasoma. Hukumu hiyo ilimtesa sana kichwa chake, alitamani kila mtu anayemhisi kuwa ana makosa aingie katika moyo wake na kuupata ukweli.

Alilia na umaskini wake, lambda angepata wakili mzuri angeweza kumtetea, kumkosa wakili kukahalalisha kifungo hicho!!

Alikwenda gerezani huku akiumia sana rohoni. Aliyaanza maisha mapya kwa shida sana, akawa mnyonge kila mara na mwili ukapoteza afya kiujumla.

Huko gerezani alifanikiwa kupata rafiki aliyekuwa na cheo ama jukumu la uzikaji wa wafungwa hasahasa ambao hawakuwa na ndugu ama ambao ndugu zao huwa hawajitokezi pale gerezani.

Mzikaji alijaribu sana kumtia nguvu Wambura na kumwaminisha kuwa hiyo ilikuwa hatua tu ya maisha anapaswa kuizoea na siku moja ukweli utajulikana tu! Bwana Wambura maneno ya mzikaji hayakumuingia kabisa.. alizidi kunyong’onyea.

“Siwezi kuvumilia kukaa gerezani miaka mitatu…..kama unajali kilio changu nisaidie nitoroke kwa namna yoyote ile ndugu yangu!!” Wambura alimsihi mzikaji.



SIKU MOJA mzikaji akamwambia Wambura kuwa msaada umepatikana. Lakini yataka moyo!!

“Nipo tayari kwa lolote ilimradi tu nitoke humu!!” alijibu kwa msisitizo huku akimtegea sikio mzikaji.

“Msaada pekee wa kukutorosha humu ndani ni kwa njia ya jeneza… yaani mfungwa akifa mimi nakuunganisha naye kwenye jenerza…..” akashusha pumzi kisha akaendelea “Wewe ukisikia kengere ya msiba, njoo mara moja kwenye chumba cha maiti, utakuta tayari sanduku liko katikati ya chumba linakuwa halijafungwa, funua kifunioko ingia ndani yake ulale pembeni ya maiti kwani sanduku huwa kubwa la kutosha kila aina ya maiti na hata miili miwili inaingia. Kisha nitakuja na kulipigilia misumari. Baada ya muda tutalipakia kwenye gari na kutoka kwenda nje ya gereza makaburini nikiongozana na baadhi ya wafungwa na maaskari magereza.

Tutakuzika huko lakini baada ya dakika 20 hadi 30 nitarudi kukufukua. Hautaweza kushindwa kupumua kwa dakika hizo, utatoka ukiwa huru.”



JAPOKUWA wazo lilikuwa zuri lakini lilimtisha sana Wambura. Hata hivyo akaona afadhali afanye hivyo kuliko kukaa gerezani miaka mitatu bila kosa.



Siku moja akasikia kengere ya msiba. Akafanya kama alivyoelekezwa na mzikaji. Akaenda na kuingia chumba cha maiti. Kweli akalikuta sanduku, akiwa na hofu kuu akaingia na kulala pembeni ya maiti iliyokuwepo. Mara akasikia mtu ameingia na kulipigilia msumari sanduku. Muda mfupi baadaye sanduku likainuliwa na kuwekwa kwenye gari.

Gari ikatoka nje ya gereza hadi makaburini. Sanduku likashushwa na kuwekwa kaburini na kuanza kufukiwa.

Wambura alijitahidi sana kuvumilia japo hofu ilizidi kutanda. Alimtegemea sana mzikaji na alianza kumuona mkombozi wa maisha yake.

Kama alivyoambiwa, akasubiri dakika kumi, ishirini.. zikapita kimya!!

Dakika thelathini kimya. Joto nalo likazidi kuongezeka.

“Nitavumilia hadi afike…” alijisemea kisha akajiongezea kauli ya ujasiri.

“Kama nilitakiwa kuishi gerezani miaka mitatu kivipi dakika kadhaa za hapa kaburini”



KWA kuwa alishakaa gerezani kwa muda kiasi akatamani kujua aliyekufa ni nani… ni kwewli aliogopa kuitazama maiti lakini aliona kama inatisha zaidi ikiwa imefunikwa vile kuliko ikiwa wazi.

Akaifunua upande wa usoni… Kwa kuwa kulikuwa na giza nene alikodoa sana macho kuitazama.

LAHAULA!!! MACHO YAKAKUTANA NA SURA YA MZIKAJI!!!

MZIKAJI ALIKUWA AMEKUFA NA AMEZIKWA NA AHADI ZAKE ZA UKOMBOZI!!



________________

FUNZO::

Usimtegemee sana mwanadamu katika maisha yako, kwanza ni dhambi!!

Pili mwanadamu anakumbana na vikwazo kama unavyokumbana navyo wewe hadi kumwendea yeye. Hivyo kumpatia maisha yako ni kuzidi kuyaweka hatarini zaidi!!

Umeonewa umesingiziwa unanyanyaswa….. mwachie Mungu afanye maamuzi…

_______________

Haya mzikaji aliyetegemea atamfukua naye ni maiti…… tazama mateso atakayoyapata hadi kufa kwake…..

Bila shaka atatamani kurudi gerezani kwa miaka mingine kumi lakini haitawezekana tena!!!

0 comments:

Post a Comment

BLOG