SIMULIZI FUPI YA MAISHA: LIWALO NA LIWE
KITANDA cha kamba nilichokuwa nimelalia kilinifanya niyapate vyema maumivu makali mgongoni na upande ya shingoni.
Ni siku kadhaa tu nyuma nilikuwa nimetoka katika kulalia magodoro ya kunesa na vitanda vya kifahari.
Lakini sasa nilikuwa katika kitanda cha kamba!!
Naam! Kitanda kile kikanifanya nikumbuke kuwa sasa sikuwa shuleni tenma bali nilikuwa nimerejea nyumbani kwetu.
Kijiji cha Jang’ombe!! Nyumbani ni nyumbani!
Kila kitu kilikuwa hakijabadilika tofauti na watu wa kijiji changu kubadilika umri, urefu, unene na wembamba. Hakuna kingine kilichokuwa kimebadilika.
Akili na uwezo wa kufikiria ulikuwa uleule!!
Nilitamani kubadilisha kila kitu kwa muda mfupi sana lakini sikuona kama inaweza kuwa rahisi kiasi kile.
Yakawa mawio kisha machweo, siku zikaendelea kuhesabika hadi ile siku ambayo niliamua kuuvunja ukimya!!
Niliamua kuanza na mama yangu mzazi maana huyu ndiye angeweza kunielewa kisha na yeye amueleweshe baba yangu!!
Nafsi yangu ilikuwa haina amani tangu nilipozungumza na dada yangu Elizabeth. Kuna jambo zito sana ambalo alinieleza nikiwa kama kaka yake ambaye walau nimefanikiwa kupata elimu ya darasani.
Yeye alikuwa hajaenda shule kabisa kwa sababu tu kuna dada yangu mkubwa alikuwa amezaa na hivyo alitakiwa kumsaidia kulea.
Sasa Eliza alikuwa na miaka kumi na saba hakuwa akijua kusoma wala kuandika!!
Lakini mdogo wangu yule alikuwa na akili ya kuzaliwa na nilizidi kuamini hilo kutokana na maneno aliyozungumza nami.
“Alex kaka yangu pekee unayeweza kunielewa, naombna unisaidie bado mwezi mmoja tu lile zoezi la ukeketaji lifike tena, nimejaribu kukwepa kwa miaka yote hiyo lakini safari hii sina namna naona naenda kukeketwa.. sina elimu kaka yangu lakini najua ukeketaji si jambo jema hata kidogo. Wewe ni msomi kaka nisaidie…”
Maneno ya mdogo wangu akiwa katika huzuni kuu yalizunguka katika kichwa changu na kuitesa nafsi sana hasahasa pale nilipokuwa nakutana naye kila asubuhi na kuniuliza nimefikia wapi.
Naam! Sasa nikaamua kukivunja kile kimya!!
Nikaketi na mama yangu mzazi na kuanza kumuelezea juu ya madhara ya kukeketa watoto wa kike, nilijaribu niwezavyo kumfafanulia. Lakini baada ya maongezi marefu sana akanipa jibu moja kisha akatoweka.
“Nilikeketwa kabla sijakuzaa wewe, nikabeba mimba hatimaye nikakuzaa… huko shuleni kwenu wamewadanganya kuwa ukeketaji unamfanya mwanamke asizae au? Wapuuzi waalimu na nyinyi wanafunzi…”
Ndugu msikilizaji nilibaki nimejiinamia, mama akatoweka huku akinitukana matusi kikabila. Nafsi yangu ilipondeka sana na kuamini kuwa halikuwa jambo jepesi hata kidogo kuwashawishi watu wale.
Nikiwa nimejiinamia palepale, mara nikaisikia sauti masikioni mwangu.
“Kaka Alex, sitaki kukeketwa na sipo tayari yaani nikikeketwa najiua!!” ilikuwa sauti ya dada Eliza.
Kisha akaondoka. Huyu alizidi kunichanganya.
Sikuwa tayari dada yangu ajiue kisa zile mila za kishenzi ambazo hazina maana tena.
“Hautakufa Eliza…” nilijikuta najibu hewa kwa sababu Eliza hakuwa mbele yangu tena.
Nikakumbuka kuwa zilikuwa zimesalia siku kumi na nne tu iweze kufika ile siku ya tukio lile waliloliita la heshima!!
Tukio la ukeketaji!
Ajabu sasa wasichana wengi walikuwa wakilisubilia kwa hamu kubwa.
Maskini!! Walitia huruma kwa sababu hawakujua kama hawajui!!
Mtu wa pili kumfuata alikuwa ni baba yangu mzazi. Nikajaribu kuunda sentensi tofauti lakini baba hakuonekana kuwa pamoja nami kabisa, na mara ghafla akanimwagia togwa ambayo ilikuwa katika kikombe kikubwa pembeni yake. Kisha akachukua mkongojo wake aweze kuniadhibu. Hapo nikaona isiwe tabu, nikakimbia kuepusha shari.
Dada Eliza aliona wakati namwagiwa togwa na kisha kukoswakoswa kipigo! Nilimuona akilia…
Akazidi kunitia simanzi…
Na ilikuwa vyema kuendelea kumuona hata kama anayo huzuni lakini si kuyaona maiti yake ati amejiua kisa amekeketwa!!
Ikiwa baba amenikatalia na kutaka kunipiga, mama yangu mzazi naye amenikatisha tamaa…
Je? Nikubali kumwona dada yangu akijiua kisa kukeketwa!!!
Nini mama ya elimu niliyoihangaikia miaka mingi kwa ajili ya ukombozi wa kijiji changu?
Nini maana ya kukesha kote na hatimaye kufanikiwa kuvaa joho nikiwa nashangilia shahada yangu ya kwanza.
Laiti kama Eliza angejiua basi ni sawasawa sikusoma kabisa na sisitahili kuitwa msomi!
Siku zikazidi kusonga huku Eliza akizidi kukonda, mama akasema kuwa mtoto wake hali akashiba. Baba akasema atakuwa amepata mwanaume hivyo anamuwaza kila muda… ni mimi tu nilijua Eliza alikuwa anakondeshwa na mawazo juu ya ukeketaji!!
Nilimtazama mdogo wangu yule machoni.. nikamuona msichana ambaye miaka kadhaa ijayo anaweza kusimama kiujasiri na kutetea wanawake na watoto ama jamii kwa ujumla.
Yaani yupo kijijini na bado amehisi kuwa ukeketaji si jambo jema…
Nikasema liwalo na liwe, siwezi kuiachja dhahabu ile ikapotelea mchangani kwa sababu za kizembe…….
Na hapo nikaamua kuingia rasmi vitani!!
Vita dhidi ya watu wanaonijua zaidi ya mimi ninavyojijua!!
Lakini ilibidi tu iwe vile!!
Sikujua kama ingekuwa ngumu ya kutoa machozi, jasho na damu!!
Lilikuwa juma moja lililosalia lakini zikaanza kuhesabika zikawa siku sita, tano, nne na hatimaye zikabaki siku tatu tu. Aidha Eliza akeketwe kisha ajiue ama nimsaidie asikeketwe na aendelee kuishi.
Wazo la kushauri lilikuwa limeshindikana, sasa nikafikiria wazo mbadala.
Kuwa liwalo na liwe!
Nikajiapiza kuwa japokuwa nd’o kwanza nimemaliza chuo na sijapata kazi lakini kwa pesa kidogo ya akiba niliyokuwanayo basi nitamtorosha Eliza na kukimbilia mkoa mwingine kabisa. Kisha nikiwa naye huko tutaanzisha kampeni maarufu ya kupinga ukeketaji wa watoto wa kike. Niliamini kila kitu kitawezekana tu maana asilimia kubwa ya waishio mjini walikuwa nauelewa juu ya jambo hili hivyo wangeweza kutusaidia.
Nikamshirikisha Eliza juu ya ule mpango wangu thabiti niliousuka juu ya kumtorosha kisha tutakuja kuomba msamaha baadaye kabisa baada ya kuweka kila jambo sawa na kubadili mila zilizopo.
Eliza alikuwa tayari kwa lolote na alinikubalia kwa moyo mmoja. Nikamwambia hana haja ya kufanya maandalizi, na kubwa zaidi asithubutu kumshirikisha mtu yeyote yule.
Nikamweleza kuwa siku inayofuata ndiyo siku ya tukio lenyewe. Tukio la kutoroka!!
Tukaafikiana kukutana majira ya saa kumi na moja kisha kukimbia kuanzia hapo hadi pale ambapo jua litachomozea. Kiapo chetu kikawa kimoja tu hakuna kurudi nyuma!!
****
alfajiri tulivyokutana mambo yalikuwa tofauti na yalivyotakiwa kuwa. Eliza alikuwa mnyonge sana. Na hakuonekana tena kama yupo tayari kuondoka.
“Nimesikia kuwa wasichana watakaokeketwa ni arobaini na nne, na mimi miongoni mwao. Kaka Alex hivi mimi ni asilimia ngapi kati ya hao wengi. Sawa mimi natoroka lakini vipi hao wanaobaki, si wote wanaofurahia jambo hili, na hata hao wanaofurahia ni kwa sababu hawajui madhara ya kukeketwa…. Kaka Alex sitaondoka na sitaki kukeketwa… nafanya nini sasa.” Alizungumza kwa hisia kali huku mwisho akinitupia swali lile gumu.
Na kufikia hapo yalikuwa yamebaki masaa arobaini na nane tu!!
Akili yangu ilitaka kupandwa na wazimu. Kila kitu kilikuwa kimevurugika, masaa yalikuwa yamebaki machache sana na sikuwa najua ni kipi nitafanya ili kumnusuru Eliza pamoja na wasichana wengine na pia kizazi kijacho.
“Nenda ndani niachie mimi hili, kila kitu kitaenda sawa!!”nilimtia moyo, akaondoka huku nyuma akiniachia tabasamu dhaifu la kulazimisha.
Kama kumuokoa Eliza imechukua mwezi mzima kuamua hadi kufikiria kutoroka. Vipi kuhusu wasichana arobaini na nne.
Ama kwa hakika ulikuwa mtihani mkubwa sana!!
Nikaukumbuka usemi wangu wa liwalo na liwe!
Lipi hilo liwalo na liwe? Nilijiuliza na hapo nikapatwa na akili ambayo sikuwahi kudhani inaweza kunipata katika wakati huo.
Nikamfikiria bibi Shuku!! Bibi mlevi wa pombe za kienyeji.
Kila muda alikuwa tayari kunywa pombe hata ukimshtua usingizini, kama ni kwa nia ya pombe wala hamtagombana!!!
Bibi Shuku alikuwa ndiye alikuwa NGARIBA wa kijiji chetu. Huyu ndiye alikuwa amepewa dhamana ya kuwakeketa wasichana.
Hakuwa mzee sana bali aliitwa bibi kwa sababu tu ya heshima na ukongwe wake katika shughuli hiyo.
Nikaondoka na giza lile lile hadi kwa mama niliyemfahamu kuwa anauza pombe za kienyeji na huwa anadamka alfajiri sana kuziandaa.
Nilipofika nikahitaji huduma ya pombe, akanipimia ya kutosha nikamlipa na kuondoka. Nikaelekea nyumbani kwa bibi Shuku.
Niliamini kuwa huyu ni mtu pekee anayeweza kusababisha ukombozi kwa watoto wale arobaini na nne na kisha kizazi hadi kizazi kikombolewe.
Uzuri alikuwa anaishi yeye na binti mmoja aliyezoea kumuita mjukuu japokuwa hakuwa mjukuu haswa!!
Nikafika na kugonga hodi kwa muda mrefu, hatimaye bibi Shuku akaamka na kuufungua mlango. Nikamsalimia kikabila kisha nikamweleza kuwa nilikuwa nina safari majira ya saa moja asubuhi hivyo nimempitishia ile pombe kama zawadi tu.
Uso wake ukachanua kwa tabasamu baada tu ya kupokea mzigo ule.
“Lakini licha ya hayo nina mazungumzo nawe kidogo kama hautajali bibi Shuku!”nikamuomba. kwa sababu tulikuwa marafiki tayari hakunipinga akakubali tukaketi ili tuzungumze.
Wakati huo mapigo yangu ya moyo yalikuwa juu sana, niliamini maongezi hayana nafasi ya kumbadili bibi yule kwa masaa machache yaliyobakia. Badala yake vilitakiwa vitendo dhidi ya maneno.
Wakati bibi Shuku anagida pombe ile nilimwambia kuwa licha ya kupita kumuaga bdo nilikuwa na mazungumzo naye kidogo. Alitikisa kichwa kukubali mazungumzo huku akiendelea kugida pombe yake kwa fujo. Amakweli bibi shuku alikuwa chapombe!
Kadiri alivyokuwa anakunywa nami nilizidi kumuhesabia mafunda aliyokuwaa anameza. Sikuwa na mazungumzo naye kama nilivyomuomba bali kuna kitu nilikuwa nangoja. Naam! Hatimaye bibi shuku akaanza kulegea huku akijaribu kukabiliana na hali ile kwa kila namna.
Haikuwezekana na kamwe isingewezekana kwa mwanadamu wa kawaida kukabiliana na madawa niliyokuwa nimemchanganyia bibi shuku katika pombe ile.
Elimu yangu ya utabibu ikaanza kuonekana kimatendo.
Sikutaka bibi shuku aendelee kuwa pale nje!
Nikamburuta mpaka sebuleni kwake na kisha kumuacha pale, sikuwa na muda wa kupoteza hata kidogo! Nilikuwa naogopa kwa kitu nilichopanga kukifanya hakika!
Lakini kwa sababu nilishajiapiza Kuwa liwalo na liwe basi nikapiga moyo konde na kuanza kupekua upesiupesi chumbani kwake! Ama! Amakweli alikuwa ngariba bibi yule, chumba chake kilifanana na machinjio, matone ya damu huku na kule, hayo hayakunitisha nilichokitaka hatimaye nikakiona.
Kisu! Kisu pekee ambacho hutumika kuwahukumu wasichana wasiokuwa na hatia! Kisu cha kukeketea!
Nikachukua kitambaa na kutumia kushika kile kisu!
Nikatia katika mfuko kisha nikatoka mbio!
Mbio hzo hazikukoma, nilikimbia sana lengo likiwa moja tu kuifikia barabara ya magari ya makubwa ambapo ningeliwahi basi la saa kumi na mbili ambalo lingenifikisha wilayani ambapo ningeeleza malalamiko yangu juu ya tatizo la ukeketaji. Na iwapo wasingenielewa ningeenda mbali zaidi hadi mahali watu wanaitambua haki.
Nilipoitazama saa yangu zilikuwa zimebakia takribani dakika ishirini tu gari liweze kupita. Na ilikuwa lazima niwahi vinginevyo nilitakiwa kungoja gari linalopita majira ya saa mbili asubuhi. Muda ambao sikutakiwa kuwa katka kijiji hcho kwa usalama wangu! Nilikimbia sana ndugu msikilizaji, nilikimbia sana nilipochoka nikalazimika kutembea upesiupesi, na hapo pia nikachoka nikabaki kutembea kawaida! Liliposhndkana na hlo nikalazimika kuketi kidogo nivute pumzi. Hakika barabara ilikuwa mbali sana!
Nilipoketi nikasikia kwa mbali mchakacho mithiri ya watu wanakimbia, nikatulia palepale ili nisikie kama ni kweli ama mashaka yangu!
Hayakuwa mashaka, kuna watu walikuwa wanakuja kwa nyuma!
Nikasimama upesi na kujificha katika kichaka ili iwe rahisi kutambua iwapo hlo lilikuwa kundi la watu wabaya ama la!
Kadri walivyozidi kusogea nikaanza kuisikia sauti ya kike!
Na hatimaye wakapita na nikamshuhudia dada yangu, Eliza. Na katika jopo lile japokuwa ilikuwa gizani nikaisikia sauti ya mwanaume ambaye nilimtambua haswaa japo haikuwa rasmi! Alikuwa mpenzi wa dada Eliza.
Maskini dada yangu angelienda shule kidogo angelisoma kitabu kiitwacho Ngoswe penzi kitovu cha uzembe. Niliamini dada Eliza aliendekeza mapenzi na hatimaye alimshirikisha yule bwana kuhusiana na mpango wetu wa kutoroka!!
Walipita, nikayaona mapanga mikononi mwao huku wakimkoromea dada Eliza juu ya niwapi nilipokuwa nimeenda. Dada Eliza hakujibu kitu badala yake nilimsikia akitokwa na kilio na alikuwa akitweta katika namna ya kuchoka sana.
Nilimuonea huruma sana dada yangu!!
Baada ya kuniacha maili kadhaa nilijitokeza kisha nikaitazama saa yangu, zilikuwa zimesalia dakika nane tu basi liweze kupita, na njia ile waliyoifuata akina Eliza na wale vijana wenye mapanga ndiyo njia ambayo nilitakiwa kuifuata pia ili nifike barabarani.
Nitaifuata vipi njia hiyo!! Kuifuata njia hiyo ilikuwa ni sawa na kuweka sahihi katika fomu yangu ya kifo, wasingeweza kuniacha hai watu wale na nikisema nirudi nyuma basi nilikuwa najirudisha katika kesi nzito ya kujibu
Kisu cha ngariba!! Nikakumbuka kuwa nilikuwa nimebeba kisu hicho, kisu wanachokiita kitukufu!! Utukufu? Utukufu gani, kisu cha kifo kile! Yaani kisu kimoja kinahusika katika wasichana arobaini! Ule si usambazaji wa magonjwa! Utukufu upi wanaosema?
Nikiwa nimezama katika dimbwi lile la mawazo ghafla nikasikia naguswa begani! Nilipogeuka nikakutana na jambo ambalo sikulitarajia!
La haula! Walikuwa ni sungusungu wa kijiji chetu, walikuwa wawili wakanihoji muda huo nilikuwa nafanya nini pale! Nikajisahau kuwa hiyo wiki ya ukeketaji wanayoiita tukufu huwa si ruhusa kwa mwanakijiji yeyote kusafiri kwenda popote pale.
Nikawajibu kuwa nilikuwa nawahi basi la saa kumi na mbili. Wakanitazama kimashaka na kisha kuniuliza jina la baba yangu! Nikataja, wakatoa kidaftari na kusoma kwa sekunde kadhaa.
"Yaani wewe dada yako anahusika katika wiki tukufu halafu wewe unatoroka, afande Changas hapa kuna kitu. Haya kaa chini upesi, kaa chini kijana' alinifokea yule sungusungu nilibabaika sana hakika, kwani niliona wazi mwisho wangu ulikuwa umefika.
“Kwenye huu mfuko kuna nini kijana, kabla hatujakagua wenyewe” aliniuliza mmoja wao
Nikajibu kuwa zilikuwa ni nguo zangu pekee katika ule mfuko, sungusungu mwingine hakutaka maelezo akauvuta ule mfuko ili auchukue, nikajaribu kuungángánia.
Ghafla akalishusha rungu lake zito katika bega langu!!
Nikauachia ule mfuko bila kupenda huku nikitokwa na kelele za uchungu!!
Maumivu yale ya bega yaliniacha nikiwa pale chini nisijue nini cha kufanya.
Wale sungusungu kwa tamaa za waziwazi walizokuwanazo waliungana kwa pamoja tena kwa makini sana kupekua ni kitu gani kilikuwa ndani ya ule mfuko.
Kisu cha ngariba!!!
Kisu cha bibi Shuku kilikuwa katika ule mfuko.
Kitendo cha kuwapa waukague maana yake watanifumania na kile kisu na hapo watanichukua na kunirudisha kijijini huku nikiwa nimefungwa kamba ngumu na kupigwa sana.
Moyo ulipiga kwa nguvu sana wakati yule aliyejiita afande chotara alipoanza kuingiza mkono wake katika ule mfuko kwa umakini huku akitazamana na yule mwenzake.
Kitendo cha kuwaachia ule mfuko kikamfanya mmojawao aliweke rungu lake chini ili aweze kutumia mikono yote kubnaini ni kiitu gani nilikuwa naking’ang;ania.
Hilo lilikuwa ni kosa kubwa walilofanya, hawakujua kuwa kitu ninachokiwaza ni LIWALO NA LIWE!!
Sikuhitaji ukeketaji wa wanawake katika kijiji changu uendelee, nikakifikiria kile kisu jinsi kinavyoweza kusababisha kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi!!
Moyo ukaniuma sana na kukiona kizazi changu kimepotoka haswa!!
Na hapo nikahesabu hatua kadhaa nilihitaji wakifikie kile kisu na hapo nitajua nini cha kufanya.
Kweli, kama nilivyodhani ikawa!!
Wakakumbwa na mshtuko na mimi palepale nikakwapua lile rungu pale chini na kufanya bala ambalo hawakudhani linaweza kutokea!
Nikamtandika sungusungu mmoja aliyekuwa amekamata kile kisu akikishangaa, rungu likatua barabara katika mbavu zake akatokwa nay owe na uchungu kisha akaanguka chini na kuanza kugalagala.
Yule mwenzake ambaye awali alikuwa amelitua rungu lake akafanya kosa la jinai, akainama kuokota rungu lake ili tukabiliane.
Ndugu msikilizaji sikuwa mtu wa matukio ya kupigana mara kwa mara lakini walau ninalo la kujisifia kutokana na maisha ya pale kijijini, nilikuzwa kiasili na nilipofikia umri wa kuitwa kijana nilienda jando. Huko tulifunzwa ujasiri!!
Naam! Nikaiona faida yake palepale, alipoinama tu kuokota rungu lake nikamchabanga teke kali usoni akaangukia mbali nikakiokota kile kisu na kuwaonya kuwa sitasita kunyofoa pua ya mtu iwapo watathubutu kunisogelea!
Ebwana ee!! Wale sungusungu waligwaya. Sikujua ni kitu gani walikuwa wanazungumza. Lakini walikuwa wakinisihi jambo.. na hapo nikawaamuru watimue mbio mara moja kuelekea popote wajuapo.
Ni ndani ya sekunde kadhaa sikuwaona tena karibu yangu!!
Na wakati huohuo nikiwa nimefiura na rungu na kisu cha ngariba mkononi, nikazisikia kelele za mwanamke tena.
Pasi na shaka alikuwa dada Eliza!!
Nikatulia tena nikawa kama kivuli!
Nikamshuhudia dada yangu akiwa anatimua mbio, alikuwa anakimbizwa na wale wanaume watatu.
Alikuwa anapiga kelele za kuomba msaada!! Alikuwa akilia sana na hapo nikamwona mwanaume wa kwanza anayemkaribia kwa mita kadhaa akiwa amelinyanyua panga lake juu juu.
Bila shaka hakuwa katika utani, iwapo dada Eliza angesimama basi angeuwawa kwa kukatwakatwa mapanga.
Sikuwa tayari kwa ushuhuda huo, yaani dada yangu afe halafu asishuhudie jinsi kaka yake ninavyopigania kile alichioniomba!!
Hapana!!
Kwa mara nyingine tena nikasema liwalo na liwe, ni heri nijeruhiwe ama kupoteza uhai kabisa nikiwa napambana na si kushuhudia mauaji yale kwa macho yangu.
Palepale nikatoka mafichoni, nikatimua mbio na kuwa nyuma ya yule mwanaume wa kwanza. Sikungoja sana nilipomkaribia nikainasa miguu yake kwa nyuma, akajikwaa na kupiga mweleka mkali sana huku panga likienda mbali naye.
Eliza ambaye alikuwa amesalimu amri akiamini kuwa anakufa alipogeuka na kukutana na mimi hakuamini macho yake.
Nikamsihi ajifiche mimi nitoweke kwa ajili ya ukombozi wa wanawake wote kizazi na kizazi.
Akanisihi twende wote, nikajaribu kupinga lakini alivyolazimisha nikaondoka naye huku akinipitisha njia tofauti.
Tulitimua mbio haswa hadi kuifikia barabara.
Wakati huo ilikuwa yapata saa kumi na mbili na dakika kumi na tano na hatukuliona gari wala hatukulisikia likipiga honi zake hapo kabla.
Kulikoni!!
Nilijiuliza huku kisu na rungu vyote vikiwa mkononi mwangu!!
Tuliendelea kungoja dakika kumi zaidi bado basi halikutokea.
Mwanga ukaanza kulifichua giza!
Bado basi halikujitokeza.
Kuendelea kubaki pale barabarani ilikuwa ni sawa na kukisubiri kifo chetu sisi wawili huku tunajiona, balaa nililokuwa nimelianziasha kijijini halikuwa la kawaida!!
Wakati tunafikiria kutafuta mahali pa kujificha, mara tukazisikia honi kali za basi zikipigwa.
Tukapata sababu ya mwisho ya kutabasamu!!!
Basi lilifika nasi tukapanda upesi, sasa nilikuwa nimekificha kisu huku nikiliacha rungu chini. Tatizo kuna mwanakijiji mmoja ambaye alikuwa anashusha mizigo huyu ndiye aliyeleta gundu jipya.
Baada ya dakika kumi akiwa anahangaika kushusha magunia yake ya mkaa na viazi. Mara lile basi lilizingirwa na watu wasiopungua hamsini, kila mmoja akiwa na silaha. Nilimuona na baba yangu, akiwa ameshika panga kali. Nikawaona wale sungusungu niliowaadabisha, nikamwona na yule mchumba wa dada Eliza. Tukiwa katika uoga kila mtu asijue nini kinaendelea. Mara msemaji wa msafara ule akapaza sauti.
“Kuna shetani amebebwa katika gari hii, ni ama mnamshusha wenyewe ama tunaingia sisi wenyewe kumshusha….” Sauti ile ilisikika vyema. Ikarudia mara ya pili. Watu wakaanza kuangaliana, nami nikamuangalia dada Eliza ambaye alionyesha hofu ya waziwazi usoni.
“Kaka Alex, tumekwisha!!!” aliniambia kwa sauti ya kunong’ona. Naam! Nami nikalisikia lile jasho jembamba la uoga likichuruzika katika mgongo wangu!! Dada Eliza alikuwa sawa kabisa!!! Nikakiona kifo na dalili zake zote….. Ule usemi wangu wa liwalo na liwe nikauona hauna maana katika hili!!
Wakati abiria wakiendelea kujiuliza huyo shetani anayezungumziwa ni nani yule mkuu wa msafara alitoa angalizo jingine, kuwa kama wanaendelea kumficha huyo shetani basi gari zima litaadhibiwa vikali.
Nikazitazama silaha walizokuwa wamebeba, nikawatazama abiria wasiokuwa na hatia pale ndani. Abiria wasiojua nini kinaendelea kabisa, haikuwa jambo la busara kuwaacha wateketee kwa kosa ambalo hawajalifanya.
Dada Eliza alikuwa anatetemeka huku akisisitiza kuwa hayupo tayari kufa na hayupo tayari kukeketwa. Aliyarudia haya maneno nami sikuwa na cha kumjibu!!
Wakati naendelea kujiuliza ni kipi nitafuata, yule kiongozi wa ule msafara akatoa onyo la mwisho na kisha akapiga mkwara kuwa kama huyo shetani hashushwi basi gari zima ni mashetani na watalia na kusaga meno kama huyo shetani mwenzao!!!
Huyo shetani waliyemzungumzia ni mimi!!
Shetani kwa sababu ya kuzipinga mila za kishenzi za kufanyia ukeketaji watoto wa kike.
Hasira ikanipanda nikainama na kusema na Mungu wangu!!
“Mungu wewe ndiye unayejua nani mwenye haki katika hili, baba sipo tayari kutazama mamia ya abiria wakiuwawa ama kuteseka kwqa jambo wasilolijua. Baba! Naamini upo eneo hili. Nasimama na kujikabidhi mbele yao, kama wameamua kuniua baba isiwe sasa hivi, isiwe kabla ya ukombozi. Na hata kama umeamua iwe sasa kuniita baba isiwe kwa kifo cha kukatwakatwa na mapanga katika kijiji changu, Mungu naamini unanisikia, nasimama sasa lakini sitaki kufa kifo cha namna hii!! Sitaki kufa nahitaji kuishi ili nifanye ukombozi!!!” nilizungumza kwa sauti ya chini na mara ghafla abiria wote wakiwa kimya nikasimama wima. Nikampita dada Eliza kisha nikasimama katika korido nikaipaza sauti na kusema na abiria wote, nilikuwa najiamini kupita maelezo.
Nani alisema kuwa Mungu huwa hajibu maombi? Amekulaghai huyo, usiache kumtegemea Mungu ndugu msikilizaji!!
Mungu anajibu!!
Nikajikoza kidogo kisha nikaanza kuzungumza bila kukoma.
“Ni mimi… ni mimi huyo shetani anayetafutwa, sikujificha hata muumie kwa jambo lisilowahusu. Lakini hata kama mtaishi kushuhudia maiti yangu leo, tambueni kuwa naenda kufa sasa kwa sababu ya kisu hiki, kisu kibaya kupita vyote ulimwenguni, heri yenu nyinyi wa mjini hampati majanga haya. Kisu hiki cha Ngariba wanakiita kisu tukufu, kisu kinachowakeketa dada zetu, kisu kinachokeketa wasichana wadogo, mamia kwa mamia wanakufa kwa kupoteza damu nyingi kwa sababu ya kukeketwa, maelefu ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi chanzo ni kukeketwa kwa kutumia kisu kimoja.
Akinamama katika gari hili eleweni kuwa ushetani wangu ni kwa sababu naipigania haki yenu, akina baba nanyi tambueni kuwa naitwa shetani kwa sababu napigania haki za wake na watoto wenu wa kike.
Na kama kweli mimi ni shetani na nitatoka nje kuuwawa maana yake nyinyi ni wetu wema na mmebariki mila hizi potofu. Mila gandamizi kabisa!!
Mila za kiuaji!!” nilimaliza kuzungumza huku nikijiuliza lundo lile la maneno makali kama yale nilikuwa nimelitoa wapi…
Kile kimya kikageuka minong’ono sasa, minong’ono ile ikazua umoja… mara mashetani tukawa wengi. Mashetani wanaopinga ukeketaji!!
Na kama ilipangwa itokee, wakati wale wanakijiji walipookota mawe na kuanza kulishambulia gali mara nikamsikia mwanaume mmoja akisema kwa sauti ya juu sana.
“LIWALO NA LIWE”
Na mara akajipekua katika kiuno chake, kilichofuata ulikuwa mtafutano wa hali ya juu.
Akafyatua risasi hewani kupitia dirishani.
Wale wanakijiji wakayaacha mapanga yao.
Haikuendelea safari bali kila mmoja alikuwa ameingiwa na pepo la kuleta mabadiliko.
Bahati nyingine nzuri pale ndani walikuwepo viongozi wa serikali, wakaingia kazini rasmi simu zikapigwa, na baada ya masaa mawili kijiji kilikuwa kimezingirwa na maaskari waliovalia sare. Msako mkali ukapitioshwa, mwenyekiti wa kijiji akakamatwa yeye na wafuasi wake.
Nilikuwa katrika tabasamu la uhakiika wakati wanakijiji walipokuwa wakitikisa vichwa wakati wanapewa juu ya elimu ya uzazi na masuala ya ukeketaji.
Walikuwa wanatikisa vichwa kuashiria kuwa wameridhika.
Na mwisho kabisa, kiongozi yule wa serikali na msafara wake wakanikabidhi kiti cha uongozi wa kijiji changu!!
Naam! Kijana wa kwanza kabisa kuongoza kijiji.
Awali walidhani sitaweza lakini ule ukawa ni ukombozi.
Ukeketaji ukasahaulika, unyanyasaji wa kijinsia ukatoweka.
Kijiji kikatawaliwa na amani na mshikamano.
**Jifunze!! Wewe ni chanzo cha mabadiliko, jaribu kubadilisha kile ambacho unaona kinawezekana kubadilishwa! Usisubiri ajitokeze mtu wa kubadilisha ambacho wewe unaweza kubadili..
TOA MAONI YAKO JUU YA SIMULIZI HII
ASANTE!!!
MWISHO
0 comments:
Post a Comment