SIMULIZI FUPI: KUKUPENDA KOTE KULE
Taarifa aliyokuwa akiipuuzia kila siku kutoka kwa marafiki zake ikaanza kumpanda kichwani. Akaanza kujihisi kuwa anajiongezea mzigo wa madeni kichwani mwake.
Litakalokuwa na liwe!! Alijisemea huku akiipanga siku ile kuwa maalumu kwa ajili ya tukio hilo ambalo hakulipa asilimia kubwa sana za ukweli kwani alikuwa akimuamini
Majira ya saa kumi za jioni alipokea ujumbe kutoka kwa rafiki yake ambaye aliitwa Maria.
“Wapo Lamadi Lodge chumba namba 18”
Ujumbe ule ulimuumiza sana Mage. Alijiuliza itakuwaje kama kweli ni Roman alikuwa akifanya kile ambacho alikuwa akikifanya.
“Roman…hapana Roman hawezi kunifanyia unyama kama ule…” alijikosoa fikra zake hukun akikumbuka ni mangapi makubwa alikuwa amefanya akiwa katika mahusiano na Roman.
Akajitazama kwenye kioo, akajaribu kutabasamu midomo ikagoma. Akaugusa moyo wake na kugundua kuwa ulikuwa unaenda kasi sana….
Mage akatambua kuwa alikuwa katika hofu kubwa sana ya kukabiliana na ukweli.
Akachukua vipodozi kadhaa akajipodoa lakini uso haukupata nuru. Kwa tukio lolote la dharula akachukua na ‘pedi’ za ziada alitambua wazi kuwa iwapo atashtuka ni lazima tu atavuja damu.
“Ewe mwenyezi Mungu nipe nguvu mpya…isiwe kama nidhaniavyo.” Akafanya ombi fupi kisha akatoka cvhumbani kwake.
Akaitazama saa yake ilikuwa yapata saa kumi na dakika kadhaa!!
Akampigia simu dereva wa Bajaji. Wakati akizungumza akatambua kuwa hata sauti yake ilikuwa inakwama.
Mage alikuwa anaogopairia kuwa ni uongo halafu aende na kukuta ni ukweli.
Bajaji ikafika na kumchukua.
“Nipeleke Igoma…”
“Elfu tano….”
“Twende…”
Bajaji ikaanza kuondoka kuitafuta Igoma. Nje kidogo ya jiji la Mwanza.
Baada ya dakika zipatazo thelathini, Mage alishuka na kulipa kilichohitajika.
Akasahau chenchi yake, yule mwenye Bajaji akamkumbusha.
Mage alikuwa amevurugwa!!
Kilichobaki kilikuwa kidogo tu kuifikia ile nyumba ya kulala wageni ambayo alielezwa kuwa chumba namba kumi na nane alikuwemo Roman ambaye ni mpenzi wake na mchumba kabisa.
Hatua moja baada ya nyingine hadi akaifikia ile nyumba, akazungumza na mtu wa mapokezi…..alikuwa ni mwanamke akamweleza kuwa ana mwenyeji wake katika chumba kile na wamepigiana simu tayari hivyo anaenda kuonana naye.
Mtu wa mapokezi hakumpinga….kwanza nyumba ile haikuwa ya kisasa sana, hapakuwa hata na simu ya kufanya uhakikisho huo.
CHUMBA 18.
Hatimaye alikuwa amesimama mbele ya kile.
Vipi kama sio kweli niwakute watu wasionihusu? Alijiuliza kisha akajipa jibu, “Nitajifanya nimekosea chumba….”
Akapiga moyo konde na kisha akagonga ule mlango….lakini hakupata majibu, akajisogeza karibu na kutega sikio akasikia sauti ya mwanamke akilalamika kimahaba.
“Mungu epusha asijekuwa Roman.” Alijisemea kimoyomoyo.
Baada ya dakika tano za kusimama bila kufunguliwa mlango, aligonga tena. Safari hii hakusimama sana mlango ukafunguliwa.
“Waambie jikoni walete Kuku mzima….chipsi mbili…aaah hebu” akasita kuzungumza yule binti aliyekuwa amevaa taulo peke yake. Kisha akachungulia ndani, “Husband aweke mbili chipsi ama moja itatutosha maana mi sijisikii kula” akauliza.
Mage akayalazimisha masikio yake yasisikie sauti inayofanana na ya mchumba wake ambaye wamepitia mengi lakini haikuwa hivyo. Sauti ikajibu.
“Mamii we nawe, aweke mbili tu!! Mi njaa…” alijibu kwa kulalamika.
Kama ambavyo huwa anamdekea Mage.
Yule binti alivyorudi kutaka kumwelekeza Mage akiamini kuwa ni muhudumu tu wa sehemu ile kwani muda mfupi uliopita walikuwa wameomba kuitiwa mtu wa chakula, basi wakaamini kuwa ni yule.
“Mimi si muhudumu hapa….” Mage alimweleza yule dada na hapo hapo akausukuma ule mlango, yule dada kwa kuwa hakutegemea tendo hilo akapepesuka taulo ikamtoka Mage akaingia na kisha akaufunga ule mlango.
Macho yake yakamtazama Roman mpenzi wake akiwa uchi wa mnyama.
Jamaa akakodoa macho huku akitetemeka waziwazi……
“Sikuja kwa ajili ya kukufumania Roman, na sikuja kwa ajili ya shari yoyote binti nisamehe kwa kukusukuma….” Alisita akiwa wima vile vile….
“Roman, ni wewe kweli ninayekuona mbele ya macho yangu. Roman mwanaume wa maisha yangu, mwanaume unayedai kuwa mimi ni baba na mama yako na hauna mtu mwingine wa kukujali zaidi yangu. Ni wewe Roman ambaye ulinipakata katika mapaja yako ukasema kuwa siku ukinisaliti na mauti ikukumbe….uko wapi eeh Mungu mbona hukusikia kiapo hiki? Roman nilikwambia mara ngapi kuwa ukisikia kuna kitu unakihitaji katika mwili wangu useme ila kiwe halali tu…..mbona ulinikuta sina utaratibu wa kubadilishana ndimi lakini nikafanya kukufurahisha, Roman nilikuwa siwezi kufanya ngono kwa staili zako ngumu ulizoniambia lakini mbona nilifanya kwa ajili yako, ni lini nimewahi kukutoa machozi hata kwa bahati mbaya Ramon. Ulinikuta nikiwa sipo tayari kuwa na mpenzi lakini kwa ajili yako na huzuni uliyokuwa nayo ya kubaki yatima nikakupatia moyo wangu, sikukwambia Roman mapema kabisa kuwa nina matatizo ya shinikizo la damu nd’o maana sitaki kujihusisha na mapenzi wakati nipo chuo, Roman yaani mguu ambao ulitakiwa kukatwa huo nikajitoa na kuwalaghai wazazi na ndugu zangu wengine nikapata pesa na kukunusuru na jambo hilo unautumia kutembea hadi katika maficho haya ili kunisaliti.
Hivi ukifumba macho hauioni picha yangu ukaona aibu, haunioni nikiwa nalia kwa sababu yako wewe….huyaoni hayo Roman. Kumbuka wewe sio mwanafunzi mimi ni mwanafunzi nakuhudumia kila kitu kwa pesa kidogo ninayotumiwa na wazazi wangu…kipi sijakupa Ramon…..” akasita kisha akamgeukia yule binti.
“Dada, wewe ni msichana kama mimi….sijui kama unampenda Roman, ama niseme sijui kama alikwambia kuwa ana msichana anaitwa Mage. Kama hakukwambia basi huna kosa lolote lakini kama alikwambia na ukaamua kushiriki bila kunijali kwa lolote umenikosea sana yaani umefanya kosa kubwa sana na hata nafsi yako inajua kuwa umenikosea.
Sikia dada, mwanaume wa kwanza nilimpenda haswa na hata Roman nilimwambia, nilijitolea figo moja kwa ajili yake ili tu kuokoa uhai wangu, lakini akiwa na figo ileile niliyompatia bila kinyongo. Nikamkuta akifanya uzinzi nyumba ambayo naishi naye, wala sikuleta ugomvi. Nikajishusha tu ili yaishe lakini akageuka mbabe akanitukana sana. Akanitusi mno, kuwa sijui lolote katika mapenzi. Akaondoka na figo yangu kwenda kuchezea mioyo ya wadada wengine.
Nilimwambia hayo huyu mwanaume uliyelala naye kitanda kimoja…nilimwambia huku nalia. Na ni siku hiyo aliniahidi kuwa kamwe hatanisaliti…nikajivika ujasiri nikampatia moyo wangu. Tazama alichonifanyia, simama katika nafasi yangu dada simama sasa, umepoteza figo unaukabidhi moyo kwa mwanaume anakufanyia mambo haya.
Ni kipi kinanifaa mimi, siwezi na kamwe sitapigana tambu. Kinanifaa nini sasa kama sio uhai utoweke nijue nimekosa kila kitu duniani. Naam! Bora nife kabisa kuliko fedheha kama hii.” Akasita huku machozi yakimbubujika, akamgeukia Roman.
“Roman mpenzi wangu…nilikupenda sana na nilijitoa kwa kila kitu kwako, nasisitiza kuwa nilijitoa kwa kila kitu kwako……”
Roman akabaki kuduwaa aibu tele zikimjaa usoni, yule dada aliyekuwa amejihifadhi katika taulo tena alikuwa akilia kilio kikuu sana.
Mage akaufungua mlango na kutoka nje!!!
Roman alikosea kumwacha atoke peke yake!! Ni heri angefanya maamuzi ya kumfuata kuliko kungoja aende kumwomba msamaha nyumbani!!!
Yule binti aliyefumaniwa alivaa nguo zake akatoweka huku akiwa katika kilio kikubwa kabisa. akamuacha Roman ambaye hakujua nini afanye.
Baada ya muda akaamua kumwendea Mage amlilie na kumwomba msamaha.
Alipofika nyumbani kwake mlango ulikuwa haujafungwa…
Akausukuma na kukutana na karatasi kubwa mezani ikiwa na maneno machache tu.
“KUKUPENDA KOTE KULE ROMAN”…akaanza kuita jina Mage bila kupata majibu yoyote.
Baadaye aliukuta mwili wa Mage ukiwa katika kitanzi bafuni.
Roman akapoteza fahamu palepale!!
Majirani waliosikia makelele yake baada ya kuuona mwili wa Mage kitanzini nd’o waliomfikisha hospitali.
Baada ya siku mbili alirejea na fahamu lakini hazikuwa fahamu sahihi alikuwa amerukwa akili…..
Mzimu wa Mage ulikuwa umemvuruga haswa!!!!
Amakweli KUKUPENDA KOTE KULE bado ukamsaliti!!
Unastahili maisha hayo Roman!!!
MWISHO!!!
SHARE SHARE SHARE
0 comments:
Post a Comment