Search This Blog

Monday, January 2, 2023

CHOZI LA MAMA

 




SIMULIZI FUPI - CHOZI LA MAMA





KILA mmoja alimpa jina alijualo yeye. Wengine wakimuita kichaa mgeni, wengine chizi freshi na mengineyo mengi kulingana na wakati. Hakuna aliyejua wapi anatoka, lakini alikuwa katika kundi la vichaa pale mjini. Aliokota makopo na kuzurura nayo, alikula majalalani akigombea chakula na mbwa koko, Mungu alimwepusha na magonjwa na kumfanya acheke peke yake kila mara. Alipokasirika aliponda watu mawe, lakini licha ya hasira hizo baada ya miezi kadhaa akagundulika kuwa ni mjamzito.



Ikawa skendo mjini kumfahamu ni nani muhusika wa dhambi ile kwa mtu asiyekuwa na akili timamu. Hakupatikana!! Maisha yakendelea. Ilingojewa miezi tisa ifike aweze kujifungua ili atafutwe mchawi nani. Lakini hata miezi tisa haikufika ile mimba ikatoka, huku dhahiri shahiri yule kichaa akionekana kupitia maumivu makali. Wananchi wakanong’ona kimya kimya kuwa aliyemjaza mimba, amemvizia na kumlisha madawa makali hatimaye ile

mimba imetoka.



 Hilo nalo likasahaulika. Ikapita miezi mingine miwili, akapata mimba tena yule mwanamama ambaye nyumba yake ilikuwa popote pale pasipofaa kukaliwa na mwanadamu wa kawaida. Kama ilivyokuwa awali watu walilaani kitendo hicho alichofanyiwa kichaa mgeni. Mimba ikaanza kukua, lakini hata hii haikufikisha miezi tisa, ikatoka kama ile mimba ya awali. Lakini hii ilikuja katika mtindo wa aina yake. Kichaa mgeni alizungumza kitu kwa sauti isiyokuwa ya kwake. Alizungumza mambo ambayo kila mmojaalibaki na maswali lakini wengi wakipata majibu.



MWAKA MMOJA NA NUSU ULIOPITA. MARIA akiwa amejipumzisha na mume wake asiyekuwa wa ndoa wala wa kutambulika popote bali waliishi uhawara na hatimaye kuzoeana. Wakaitana mume na mke lakini wakiwa hawana mtoto. Ugeni ukawajia siku hiyo, mwanamke mnene mfupi mweusi mwenye macho mekundu alikuwa akingoja nje baada ya mlinzi kumwambia subiri hapo. Maria alitoka akiwa ameongozana na mume wake wakiwa wameshikana viuno katika mtindo wa mahaba. “Nikusaidie nini?” aliuliza Christian ambaye ni mume wa Maria. Yule mama mwenye macho mekundu alijaribu kutabasamu na mdomo wake kufunguka, alikuwa na mapengo, meno ya mbele yote hayakuwa kinywani. Maria alimtazama kwa makini huku akiizuia hali ya kutaharuki iliyotaka kumtwaa. Mama yule mzee alikuwa na mtoto mgongoni. Bila shaka hakuwa mtoto wake labda mjukuu tu. “Wankuru haujambo..” alizungumza yule mama huku akimtazama usoni. “Wankuru nd’o nani tena..” Chris aliuliza huku akimtazama Maria. “Hata mimi nashangaa, ama amekosea nyumba.” Alijibu Maria kwa hofu!! “Wankuru umependeza wee mwanangu, yaani nilijiuliza kama ningeweza kukupata. Tangu nipoteze namba yako basi nimeshindwa kabisa kukweleza lolote. Hivi ukimuona Gilbert utamkumbuka kweli Wankuru wangu.”



Alizungumza kwa furaha na hakuona haya kuyaonyesha mapengo yake, wakati huo uso wake ulikuwa unavuja jasho. Miguu iliyopauka na nguo zake hazikuwa safi. “Maria unamjua…” Chris aliuliza. Maria akakana kwa mara nyingine. Lakini mama yule aliendelea kuzungumza kwa furaha akisimulia mambo kadha wa kadha. “Mama samahani..kwani unamtaka nani?” aliuliza kwa ghadhabu kidogo Chris. Mama yule akamtazama kwa mshangao. “Mama nimekuuliza unataka tukusaidie nini?” alikazia sasa. “Nimekuja kwa mwanangu, nimemleta mjukuu wangu amwone mama yake. Kwani kuna ubaya…..” akamgeukia Maria, “Wankuru eeh kuna kosa nimefanya mwanangu eeh” aliuliza kwa kubembeleza huku akijitoa katika hatia. “Huyu ni nani Maria na huyo mtoto ni wa nani.” Alihoji Chriss. Maria akajitoa utimamu wake na sasa akawa mbogo. “Kwa hiyo Chris unadhani namjua huyu mwanamke ama. Hivi hujui unaweza kurogwa hivihivi, unamuona mtu wa kawaida huyu!! Chriss unamuona wa kawaida huyu, mtazame macho yake mekundu na hicho kitoto maskini sijui amekirogea wapi kakichukua…ametolewa kafara meno yake na bado watamtoa na huyu mtoto maskini weee!!” alifoka. Maneno yakamwingia Chriss.



Yule mama akapigwa na butwaa macho yakamtoka na akazidi kutisha kumtazama. Chriss akaingiwa na maneno ya Maria akamwamuru mlinzi amwondoe yule mama nje. Mlinzi akatii, Maria na Chriss wakakokotana kurejea ndani. Nafsi ya Maria haikuwa katika utulivu hata chembe, alimtambua yule mama ipasavyo, alikuwa ni mama yake mlezi baada ya mama yake mzazi kufariki, mama huyu alimfanyia mengi sana yasiyostahili malipo yale. Maria alitambua kuwa kwa kukiri kuwa yule alikuwa ni mtoto wake wa kumzaa basi ule ulikuwa mwisho wa mahusiano na mwanaume yule ambaye anatambua kuwa Maria hajawahi kuzaa na hana ndugu wa karibu sana baada ya wazazi wake kufariki na yeye kukimbilia jijini Mwanza kutafuta maisha. Wakati akiwaza hayo Maria kwa mbali kabisa akakisikia kilio cha yule mama aliyekuwa anaomboleza. “Wankuru…Wankur u, unanikana mimi mbele ya hadhara, unanikana Wankuru, yaani umesahau nilivyokulea mimi, macho yangu mekundu haya si ni kwa sababu yako Wankuru yaani nimepika pombe za kienyeji ili usome Wankuru, nimechochea kuni na kujiharibu ngozi, kifua na macho yangu leo hii unasema mimi mchawi nataka kukuroga Wankuru, uuuuwi!!!



Wankuru ukabeba mimba huko kila mtu akakukimbia nimekutunza kwa shida, mume wangu akanipiga hadi kunitoa meno Wankuru leo hii nimekuwa kituko, unasema nimetolewa meno yangu kafara kweli Wankuru. Wankuru ukazaa mtoto, ukanidanganya kuwa unaenda nje mara moja kumbe unamkimbia mwanao, nimekukuzia mtoto Wankuru, nimemtunza kwa mapenzi yote mimi. Si nilikwambia mama yako alitaka atoe mimba yako kutokana na shida, nikamwambia nitamuhudumia asikutoe na akuzae ukue, nimekulindia uhai wako tangu upo tumboni mwa mama yako, nikakupenda kuliko mama yako mzazi leo hii nimekuwa ombaomba, unanikana mimi na damu yako unaikana Wankuru. Wankuru uuuwi!! Chozi langu la mwisho nilidondosaha siku ile yule mwarabu aliyekupa mimba alipokupiga na kusema hakujui, nilitoa chozi hilo kwa sababu ya kukupenda Wankuru, nikalia na kumlaani yule mwarabu kama kweli anaikana damu yake Wankuru. Ulikuwa shahidi wankuru, tulipolala njaa ulinisikia nikikimbilia kwa Mganga, niliwahi kukufunga hirizi Wankuru!!



Watu waliponiita mchawi nilikwambia Mungu atatulinda na malipo ni hapahapa. Yule mwarabu yupo wapi sasa! Wankuru muogope Mungu we mtoto, Wankuru majibu ya Mungu ni ya kweli hayaongopi. Nimemtumikia tangu usichana wangu hadi leo haongopi, hajanipa mamilioni ya kung’ara ili unipokee katika nyumba yako nzuri lakini amenipa moyo wa huruma moyo wa mama. Wankuru sio kwamba nilikupenda kisa tu sijapata mtoto, nilikupenda kwa sababu ulikuwa umetengwa na kila mtu. Sasa umempata mtu wa kukupenda umesahau kila kitu na leo kwa mara nyingine nadondosha chozi. Namlilia Gilbert kwa uchungu kwa sababu atakutana na akina Wankuru wenye roho mbaya na akili nyepesi ya kusahau. Watamkana na kumnyanyasa, lakini hatakuwa kama wewe Wankuru, hatakuwa mwepesi wa kusahau. Atamtegemea Mungu na utakuja kumkumbuka.



Chozi hili halitatua chini na kumezwa na ardhi burebure, Mungu ninayemuamini si Mungu wa kisasi lakini atanisuuza moyo wangu na kunionyesha uwepo wake tena. Chozi hili na litue katika utosi wa kichwa chako!! Kichwa chenye nywele bandia zinazoogopa maji ya kijijini kwetu, maji ya chumvi. Chozi hili langu la mwisho hapa duniani liwe chozi lako kwa lolote utakalopitia. Yaani unamkana mwanao uliyemzaa, Wankuru yaani mimi nilivyolilia mtoto miaka arobaini yote na nisimpate wewe umempata huyu mtoto mtiifu wa kiume unamkana, unamkataa katakata mbele yangu. Wankuru usipomkumbuka Gilbert, Mungu wangu hayupo hai!!!! Naondoka na Gilbert, kama nilivyojikongoja hadi kufika huku, nikitukanwa na wakati huohuo nikikutana na wachache wa kunifariji, nikiitwa mchawi na wapumbavu kama wewe, lakini wapo wachache walioniita mkarimu.



Narejea nikiamini wale wanaoutambua ukarimu wangu watanipokea, sitaishi miaka mingi lakini walau nimeishi umri wa kukukuza na kumkuza mwanao. Naenda Wankuru naenda ..” kilio kilikomea pale, Maria alijiwekea tabasamu bandia lakini moyo ukiteketea. Alitambua kuwa ni yeye aliyeitwa wankuru, Maria ni jina lake la mjini tu ambalo Chriss alilitambua. Chris pasi na hili wala lile akamliwaza mkewe huku akimwomba msamaha kwa yote yaliyotokea. Maria akapitiwa na usingizi. Siku iliyofuata akafunga safari kuelekea kijijini kwao, alitegemea kumkuta mama huyo kule, amwombe msamaha na kujirudi. Lakini mwangu wa kilio chake ukamvuruga, akapanda basi asifahamu linakwenda wapi, alijitahidi kuiweka akili yake sawa lakini hakujielewa hadi akajikuta mjini Dodoma. Alishuka kama Maria, lakini baada ya masaa kadhaa akageuka kuwa KICHAA MGENI. Hakuna aliyemjua.



 Akajazwa mimba ya kwanza na haikudumu kuzaa kiumbe chochote, akajazwa ya pili na mtu asiyefahamika. Ni katika mimba hii alizungumza mambo mengi sana yaliyomfanya hadi afike hapo. Labda alipewa akili ndogo ya mwisho ya kusema ili watakaojifunza na wajifunze. Wasamaria wakahitaji kumsaidia, wakajipanga kwa ajili ya siku iliyofuata wamchukue Maria. Lakini hakuwa Maria tena…..alikuwa hayati Maria. Alikuwa mfu!! Na hakupatikana ndugu wa kumzika. Maiti yake yakazikwa na manispaa!! Aliishi maisha magumu, akampata mwenye upendo akamtunza, watu wabaya wakamjaza mimba bado yule mtu mwenye upendo hakumtelekeza, akazaa na kutelekeza mtoto lakini mtu mwenye upendo akatunza kiumbe. Maria akageuka na kulikana jina lake alipokuwa mjini, akamkana hata yule mtu mwenye upendo akamkana na mtoto wake!!! CHOZI LA MAMA likaishi katika utosi wake, Mungu akamwadhibu Maria kadri ya kilio cha mama yule!!



 Mama mkarimu hakufa mapema aliishi!! Akakitunza kiumbe kinachoitwa Gilbert kwa hekima zote, kikakua wasamaria wakasaidia kikasoma. Na hata kilipofikisha umri wa kujitambua, kikiwa darasa la tano. Mama mkarimu akatokwa na uhai huku akitabasamu!!!



UJUMBE:

1. MAMA ni kiumbe cha kipekee, hupaswi kumsaliti mama yako….

.itunze ahadi kama yeye aliyekutunza kwa miaka mingi bila kuvunjika moyo.



 2. STAREHE ZA MUDA MFUPI zisikufanye uwasahau uliosota nao kwa miaka lukuki.



3. MUNGU hujibu!! Muamini yeye sasa.



 MWISHO!!!!

0 comments:

Post a Comment

BLOG