Search This Blog

Sunday, January 1, 2023

NJIA PANDA YA KUZIMU

 






SIMULIZI FUPI : NJIA PANDA YA KUZIMU



Umasikini wa kutisha, majukumu yaliyonizidi umri na dharau zisizomithirika kutoka kwa watu waliotuzunguka zilinifanya nijisikie mpweke sana, mama yangu aliniambia kuwa licha ya yote hayo yanayotutokea nijitahidi sana kupambana na jinamizi la tamaa.

Mama alinionya kabisa nijiepushe na tamaa.

Maneno ya mama yaliniingia na kunikaa japo kuna muda nilijikuta nikitamani vitu ambavyo vilikuwa nje ya uwezo wangu.

Nilitamani kuwa na msichana mrembo anizalie mtoto naye mama apate mjukuu wake wa kwanza kabisa. Tena si mjukuu kwa njia za mkato la. Nilihitaji mama apige vigelegele harusini nikiwa naveshana pete na mke wangu.

Lakini yangewezekana vipi haya pasi na pesa.

Pepo za pesa zilivuma na kuwafuata wenye nazo ili utimie ule usemi kuwa ‘mwenye nacho ataongezewa’.

Umasikini wetu ukanifungua akili na kukitambua kipaji changu, nikatambua kuwa nilikuwa nao uwezo wa kuandika tungo za hadithi ambazo zilivutia kusomwa na rika lolote lile.

Mama yangu hakuwa shabiki wa kusoma, si kwa sababu hakupenda nilichokuwa naandika bali kwa sababu hakuwa akijua kusoma.

Nilipokuwa namsimulia nilichokiandika alinitia moyo na kuniambia kuwa siwezi kujua huenda ni maajabu ya Mungu kunitunuku kipawa kile ili nije kuibeba familia yangu.

Siku zikakatika huku nikijikatia tamaa na kile kipaji changu.

Na hatimaye nikiwa katika dakika za mwisho kujihesabia kuwa kipaji kile si mali kitu. Nililetewa taareifa na rafiki yangu ambaye alipenda sana kuzisoma kazi zangu, aliniambia kuwa kuna shindano limetolewa magazetini, gazeti lile linatafuta mtunzi na mwandishi wa hadithi.

Nilizipokea taarifa zile katika namna ya kawqaida sana, kwa sababu nilitambua wazi kuwa matangazo mengi ya kazi huwa washapatikana wafanyakazi na pale wanatoa tangazo ili kutimiza wajibu tu.

Rafiki yule akanisihi sana nishiriki.

Nikamwambia kuwa nitajaribu, akanieleza kuwa kule wanahitaji simulizi ambazo zimechapishwa tayari. Akanitoa hofu kuwa atanisaidia kufanya kazi ile.

Ikaanza kwa kukata tamaa lakini mambo yakaanza kuwa kama yanavyotakiwa.

Tulishiriki watu mia mbili na zaidi katika shindano lile.

Sikuamini pale walipokatwa watu mia walioshindwa eti mimi nikabaki katika ile orodha ya washiriki waliofanya vizuri na nilikuwa nafasi ya saba kwa ubora kati ya watu mia moja.

Ni hapo ari ikarejea, katika kuendelea na shindano ikatakiwa simulizi nyingine mpya na sio ile iliyoshindanishwea awali.

Nikajikunja na kuandika simulizi nyingine tena.

Ikaingizwa katika mashindano nikafanikiwa kuingia katika hamsini bora safari hii nikiwa nafasi ya kumi kati ya washiriki wote.

Mama yangu alikuwa akiniombea sana dua kila siku, na kunitia moyo kuwa nifanye kwa akili zote na ikiwa nitashinda basi umasikini tutaupungia mkono wa kwaheri.

Baada ya kubaki watu hamsini kwa mara ya kwanza tukakutana na mmiliki wa gazeti lile ambaye alikuwa mtu mkubwa sana hapa nchini Tanzania.

Lilikuwa jambo la kipekee sana kuzungumza naye ana kwa ana, akatueleza kuwa kati ya watu hamsini alikuwa akihitaji watu watano tu.

Akaelezea kuwa safari hii ni yeye ambaye atazisoma simulizi zote hamsini na kutambua ni nani bora kati ya wote.

Akatutamanisha zaidi kwa kutueleza kuwa hao watu watano watakaoshinda basi watapata kazi moja kwa moja katika ofisi yake, watapangishiwa nyumba jirani na ofisi na gharama zote zitakuwa juu yake. Na kubwa zaidi ni mshahara mnono.

Mate yalinitoka mpenzi msomaji, nilikuwa naihitaji sana pesa kuliko kitu kingine kwa wakati ule. Nilikuwa nina haja ya kuifanyia kitu jamii na familia yangu.

Bwana yule akatueleza aina ya simulizi ambazo anazipenda.

Akasema anavutiwa na simulizi zinazobeba uhalisia zaidi. Akasema hapendelei simulizi ambazo ni dhahania zaidi ambazo hata ufikirie vipi ni kitu ambacho hakiwezi kutokea katika nchi yetu.

Akatusihi tujitahidi kuandika vitu ambavyo vina uhalisia na nchi yetu, matukio ambayo yanatokea katika jamii zetu na kadhalika nchi jirani.

Baadaye alitoa fursa ya kupiga picha ya pamoja, kwangu mimi ile ilikuwa hatua kubwa sana katika maisha yangu.

Picha zikaoshwa kidigitali na kila mmoja kupatiwa yak wake.

Niliifikisha picha ile kwa mama yangu kana kwamba ni mshahara, tulipatiwa pia fulana zenye tangazo la shindano lile.

Mama alinikumbatia kwa nguvu sana na kisha kumshukuru Mungu kwa muujiza ule anaoutenda.

Nilimweleza mama juu ya simulizi ambayo inatakiwa katika fainali ile.

‘’Simulizi zipo nyingi mwanangu, tatizo huwezi kujua mwenzako atakuwa ameandika simulizi kuhusu nini, pale bondeni kwa mzee Hoja kuna binti anasemekana ana historia hiyo nasikiaga tu juu juu yaani kama ungempata yule ingekufaa lakini sikushauri kabisa uende huko maana sina uhakika lakini kuna tetesi za ajabu ajabu..huko usiende. Tafuta machokoraa andika kuhusu wao, wana mengi sana watoto wa mitaani, tena ikiwezekana unaiita simulizi hiyo CHOKORAA….’’

‘’Hapana kuna mwandishi tayari ameandika kitabu kinaenda kwa jina hilo….’’ Nilimkatisha mama kuhusiana na hilo, ‘’kwani huyo binti sijui kuna nini nikizungumza naye si ninamwambia kama nikishinda nampatia pesa kidogo au..’’

‘’Martin wewe yule nimekwambia achana naye, kama na hao machokoraa ni ngumu kaandike kuhusiana na wagonjwa wa kansa ama wenye ukoma…..’’ mama alitoa wazo jingine.

‘’aah mi mambo ya hospitali sitaki mama najua huko kila mmoja ataenda…’’

‘’sawa kama hautaki mambo ya hospitali chagua mengine ila sio kwa mzee hoja na binti yake yule, achana naye tuheshimu waswahili waliosema lisemwalo lipo… sawa mwanangu..’’

Mama alimaliza kisha akanipongeza tena na kunitakia heri. Nikaingia jikoni nikajipakulia chakula nikala kisha nikaingia chumbani kwangu kulala.

------

WANASEMA kuwa ni heri usimkanye mtu jambo kwa sababu utampa shauku ya kulijua. Na hapohapo wanasema mtu mzima dawa.

Mimi nilitamani kufanya kitu kizuri, nilizitamani zile pesa alizoahidi mkurugenzi yule.

Bila kumshirikisha mama nilienda maeneo ya nyumbani kwa mzee Hoja nikiwa na lengo la kumuona huyo binti.

Kweli nilimuona na kusalimiana naye nikizuga kuwa namtafuta mtu fulani pale, yule binti wa kuitwa Nasra akanieleza kuwa nimekosea nyumba labda.

Nikaingilia pale alipoishia yeye na kisha nikamueleza bayana kuwa nilikuja kumtafuta yeye na si kitu kingine pale.

Alipigwa na bumbuwazi, nikamtoa hofu na kumueleza kuwa mimi ni mwandishi chipukizi na nilikuwa nimekuja kuzungumza naye ikiwezekana tufanye biashara.

‘’biashara gani tena kaka yangu’’

‘’Nahitaji simulizi ya maisha yako, siijui hata kidogo lakini kama inafaa niipeleke katika mashindano. Ikifanikiwa kushinda mimi nitakupatia pesa kiasi nami nitabaki nazo kiasi. Halafu kila mwezi nitakuwa nakulipa…’’ nilimweleza kwa pupa kana kwamba tayari nimezipata zile pesa.

Nasra akanitazama kisha akatabasamu kidogo.

‘’Kweli unayoyasema ama unataka kitu kingine tu…’’

‘’Sihitaji kitu kingine dadangu we kama inawezekana hata sasa hivi nisimulie tu…’’

‘’Hapana kwa sasa hivi, tufanye kesho jioni tukutane kisimani nitakusimulia kidogo halafu keshokutwa nitamalizia, ujue mama hapendi nimsimulie mtu kilichonitokea lakini nahitaji pesa kwa sasa ikiwa hautaniongopea utakuwa umenisaidia sana. Ila sharti moja tu kabla sijaanza kukusimulia unanilipa pesa kidogo..’’ alizungumza kwa sauti ya kunong’ona. Sasa hapo pa kumlipa mi sikuwa na kitu chochote lakini nililazimika kumkubalia tu.

Tukaagana nikaenda kwa yule rafiki yangu na kumweleza juu ya siri ile. Sikumficha kitu kuhusu Nasra.

Na yeye akasema kuwa aliwahi kusikia tetesi kuwa kuna historia pale ya ajabu.

‘’Hayo maajabu nd’o nayataka.. Ramso nataka ushindi kumbuka nikishinda mimi, umeshinda wewe, ameshinda maza na watu wengine wengi tu. Na ili kushinda inabidi kuandika kitu cha kipekee…’’

‘’Sawa sasa hapo kinahitajika nini zaidi’’ akaniuliza swali nililokuwa nikihitaji.

‘’Nasra anahitaji kifuta jasho kabla hajaanza kunisimulia.’’

‘’Duh sawa sipo vizuri lakini chukua hii elfu thelathini utampatia ilimradi tu asimulie ukweli mtupu….’’ Alizungumza huku akinipatia kiasi kile cha pesa. Nilimshukuru sana na kumuahidi kuwa kesho yake nitamtafuta baada ya kuzungumza na Nasra ili nimpe mustakabali wa simulizi ile….

Tukaagana huku tukicheka kwa furaha sana, tuliuona ushindi ukiwa unakaribia.

Sikumweleza kitu chochote mama yangu, nilimpatia shilingi elfu kumi kwanza. Akaduwaa ni wapi nilikuwa nimetoa nikamweleza kuwa muda utafika zitakuwa zimezagaa humo ndani pesa za kutosha. Nikamweleza kuwa nimeandika simulizi moja nzuri sana najua nitashinda.

‘’Isijekuwa ulienda kwa mzee Hoja we mtoto…’’ aliniuliza bila kutilia maanani. Nikatikisa kichwa kukataa.

Nikalala huku nikimuwaza Nasra.

Niliwaza ahadi nilizompatia na kuhisi utekelezaji wake utakuwa mwepesi tu, nitamlipa hadi atafurahi mwenyewe. Kwa tetesi nilisikia kuwa mshahara tutakaopewa washindi si chini ya milioni moja na laki mbili, hapo laki ya kwake halafu nabaki na milioni moja, au nampa hata laki mbili… ujue milioni parefu sana.

Ndugu msomaji nilijipigia mahesabu makali sana hakika, nikasahau kuwa si vyema kupigia mahesabu pesa ambayo haijaingia katika mkono wako.

Hatimaye usingizi ukanipitia nikiwa namuwaza Nasra na jinsi alivyokuwa akienda kunipatia ushindi.

Siku iliyofuata sikucheza mbali na kisima, nikiwa na daftari langu tayari kabisa na kalamu.

Hatimaye Nasra alifika akiwa na ndoo yake ya maji.

Tulisalimiana na kisha tukakaa chini ya mti ni hapa alipoanza kunisimulia mkasa wake.

Mkasa ambao sikujua kabisa kuwa utanichota mtama na kisha kuanza kuniburuza kuelekea nisipopajua.

Naam wanasema pia USILOLIJUA halitofautiana hata kidogo na ule usiku mnene wa kiza.



 Niliona kama Nasra alikuwa akiteka maji taratibu sana nikaona ni heri nimsaidie upesi upesi ili nianze kuusikiliza mkasa wake aliotaka kunisimulia mkasa nilioamini kuwa utakuwa mkasa wa aina yake ambao utaniwezesha kushinda lile shindano na hatimaye kupata kazi inayoingiza kipato kikubwa.

Hatimaye nilichokingoja nilikipata….. nasra akaanza kuusimulia mkasa wake kwa sauti tulivu kabisa huku uso wake ukitawaliwa na tabasamu hafifu sana.

‘’Nitakuwa muongo nikisema eti mume wangu hakunipenda, hakika alinipenda na kunijali haswa.

Kila nilichotaka alikuwa ananipa kadri ya uwezo wake, ambacho hakuweza kunitimizia basi alinieleza wazi kuwa hawezi lakini atajaribu kunitimizia.

Sijui wanawake tuna matatizo gani, tuna tatizo la kutoridhika yaani likiisha hili jema tunataka jema jingine.

Baada ya yote yaliyotokea nikajikuta nikianza kumlalamikia mume wangu kuhusiana na suala la ndoa isiyokuwa rasmi, yaani yeye aliwajua wazazi wangu lakini mimi hakuwahi kunitambulisha kwao. Na kamwe hatukufunga ndoa iliyotambulika….. nililalamika sana lakini alikuwa anatabasamu na kunieleza kuwa ni kitu gani nilikuwa nakosa…’’ mwanadada Nasra alianza kuusimlia mkasa wake katika maneno yale nami nikawa makini sana kumsikiliza. Nikatikisa kichwa kumaanisha kuwa nilikuwa nimeelewa aendelee kusimulia. Nilikuwa ninayo haraka ya kujua ni kitu gani kilimsibu katika mkasa huu.

‘’Wanawake tukiamua jambo fulani liwe hivi kutokana na hisia zetu basi jambo hilo huwa, sisi sio wepesi wa kupuuzia mambo kama ilivyokuwa kwenu wanaume… ndo maana ni rahisi sana wanawake kugombana kuliko wanaume kwa sababu tunaloliwaza tunataka liwe….. basi nikanuia kuwa nitaenda kuwaona wazazi wa mume wangu kilazima. Na dawa pekee ilikuwa chumbani, kila siku ambayo nilipanga kuchota siri kadhaa kwa mume wangu basi nilikuwa nakiandaa chumba vizuri, nisijisifu ndugu mwandishi lakini japokuwa sikuzaliwa Tanga lakini nilikuwa mkorofi sana pale linapokuja suala la chumbani, nilijua kukiandaa chumba nacho kikaandalika, nilijua namna ya kumfanya mwanaume afanye lile ambalo awali hakukusudia. Na wanasema kuwa wanawake huhisi waume zao wanatoka nje ya ndoa lakini kwa tiba niliyoitoa chumbani nikiwa na mgonjwa wangu yaani mume wangu hakika wasiwasi ulikuwa mbali nami najua wapo wengi wataalamu kunizidi lakini hawapatikana kirahisi hadi kumfikia mume wangu. Nilikuwa najiamini sana, basi kila tukiwa watupu nilifanya namna zote za kumchimba mume wangu hadi pale nilipoipata ramani rasmi juu ya wapi ni kwao na ni kwa jinsi gani naweza kufika… nilijiona mjanja sana kwa kufanikiwa kule sikujua kama nilikuwa najiingiza katika matatizo makubwa. Ni bahati yangu sana eti leo naongea nawe unaandika mwandishi……’’ akavuta pumzi na mimi nikamsogezea ile ndoo ya maji akachota kwa kutumia kikombe alichotumia kuteka maji, kisha akapiga mafunda kadhaa na kushusha pumzi. Kisha akaendelea

‘’Nikafanikiwa kumlaghai mume wangu kuwa ninaenda nyumbani baba yangu mdogo anaumwa, kwa jinsi alivyonipenda aliniruhusu huku akinibusu shavuni na kunieleza kuwa ananipenda sana na hapendi baya lolote liweze kunitokea.

Maneno yake hayakuyabadili maamuzi yangu, nikapanda gari na kuondoka kuelekea wilaya ya Kilindi mkoani Tanga ni huku ambapo mume wangu wakati tukiwa katika faragha aliropoka kuwa wazazi wake wote wawili walikuwa wakiishi…. Tena akaongezea ambalo hajaulizwa akasema ana muda sana hajaenda kuwasalimia. Sikuitilia uzito kauli hii mimi nilitaka kuwaona wazazi wa mume wangu, eheee kabla sijasahau mwandishi. Wakati huo nilikuwa nina mimba ya miezi miwili. Niliona si heri kuzaa bila wazazi wa upande wa pili kunitambua, hakuna kitu nilikuwa naogopa kama kurudi nyumbani kwa baba na mama yangu huku nikiwa nina mtoto waanze kunilea mimi na mwanangu. Nadhani hili lilinisukuma zaidi, mama yangu mzazi nilimuaga kuwa naenda kwa wakwe zangu lakini kisirisiri asimuulize mume wangu… mama akanikubali mtu mwingine niliyemuaga alikuwa ni rafiki yangu Rahma, huyu alikuwa mstari wa mbele kunikejeli kila siku kuwa mimi ni mjinga ninaishi na mwanaume nisiyepajua kwao.

Nikaondoka….. ndugu mwandishi umewahi kusafiri na kisha ukafikia njia panda…’’ aliniuliza, nikatikisa kichwa kumkubalia kuwa nimewahi na ninazifahamu njia panda nyingi tu.

Akainama na kisha akafunua kichwa chake, nilishtuka kukiona. Naye alijua kuwa nitashtuka, akakifunika kisha akanitazama huku akitabasamu.

‘’Hujaona nywele hata moja katika kichwa changu na unaona makovu ambayo ni mabichi, hayo hayatakauka kamwe na ninajua hujaamua kutema mate chini lakini najua kuwa ninanuka sana tu. Najua hili kiuwazi…. Haya yote niliyafuata mwenyewe nilipojikuta katika njia panda ya kwenda kuzimu….. nikajiuliza wapi ni sahihi na wapi si sahihi kumbe pote kusini, kaskazini, mashariki na magharibi zilikuwa njia za kuelekea kuzimu. Nikachagua njia mojawapo nikaifuata eti njia ya kwenda kwa mama mkwe wangu na baba mkwe, watu walionielekeza waliniuliza mara mbilimbili, una uhakika bibi Shuku ni mama mkwe wako nikawajibu kiujasiri huku wengine nikiwaletea nyodo. Kuna mwanaume mmoja alinisihi sana eti nisiende kwa bibi Shuku bali niende kulala nyumbani kwake, aisee nilimtukana sana mwanaume yule yaani nilimtusi sana nilihisi amenichukulia kiwepesi sana kuwa mimi ni msichana nisiyekuwa na uelekeo. Baada ya matusi yale yule mwanaume aliguna kisha akaniambia ‘asante sana dada yangu ila sikuwa na nia mbaya kabisa’ sikujibu lolote nikamsonya na kuondoka zangu.

Nikatembea na kwa mbali nikaliona lile jumba la kifahari ambalo nilielekezwa kuwa ndipo nyumbani kwa bibi shuku. Nikatabasamu na kutambua kuwa kumbe wote walikuwa wakinionea wivu kwa sababu ukweni kwetu wana uwezo kifedha, nikapiga hatua hadi nikafika. Nikapokelewa mizigo yangu na watoto wadogo. Nikaambiwa kuwa mama mkwe yupo ndani, wakaniongoza nikaingia.

Nilipoingia nikasikia nikiitwa jina langu huku nikikaribishwa, nikashangaa wamenijuaje hawa wakati sijawahi kufika, au Mohamed aliwatumia picha zangu, nilijiuliza. Mohamed ni jina la mume wangu ndugu mwandishi.

Lakini nilipogeuka nikakutanisha macho yangu na Rahma, huyu alikuwa rafiki yangu kipenzi jijini Dar es salaam ambaye alikuwa akinisisitiza kila siku kuwa nisiwe mjinga nifanye nijuavyo nifike ukweni kwetu ajabu sasa namkuta ukweni hakunishangaa, aliendelea na mambo yake na hapo yule mama mkwe ambaye alikuwa amegeuka upande mmoja na kunipa mgongo aligeuka.

Mwandishi niliishiwa nguvu, nikataka kukimbia nilipogeuka kutazama wale watoto wawili wanaofanana walionisindikiza pale ndani zilikuwa ni paka mbili nyeusi zikinitumbulia macho kwa ghadhabu. Nikapiga mahesabu lipi ni jambo jepesi kuendelea kutazamana na yule kiumbe wa kuitwa mama mkwe wangu ama kukabiliana na wale paka ili nipite pale mlangoni.

Nikaamua kuwakabili paka, ile napiga hatua moja mbele paka akaruka juu na kunitia kucha katika uso wangu huku akitoa milio ya ajabu kama kitoto kichanga.

Maumivu yale yakanifanya nipoteze uelekeo nikakimbilia upande ninaodhani kuwa ni sahihi kumbe la.

Nikahisi kukumbatiwa na kitu chenye joto sana, nilipofumbua macho vizuri nilikuwa mikononi mwa kiume wa ajabu kabisa ambaye niliambiwa kuwa ni mama mkwe wangu…. Mwandishi nikatamani nipoteze fahamu lakini sikupoteza fahamu. Niliendelea kutambua nilichokuwa nakiona, kile kiumbe kilikuwa kina sura mbaya na kilikuwa kikitokwa na harufu kali ya mkojo, kinywa chake kilikuwa kinatoa harufu mbaya wakati huo kiumbe kile kilikuwa kinacheka…….’’ Alisita Nasra akatazama juu kama anayekumbuka kitu.

Na hapo akaanza kutetemeka huku akinyanyua mikono yake juu kama mtu anayejizuia asipigwe na kitu fulani.

Hofu ikaanza kuniingia na mimi nikatazama nisione kitu chochote kile.

‘’Wanakutaka wanakutaka….wewe’’ Alianza kuzungumza yule dada huku akiwa na hofuu kuu, nikajikuta namuuliza.

‘’Wanamtaka nani na wanamtaka wapi’’ niliuliza kiuoga

‘’Wanakutaka wewe.. wanakutaka NJIA PANDA YA KUZIMU….’’ Alinijibu huku akitetemeka.

Jibu lile liliniogopesha sana, nikajikuta naachia kalamu na daftari ili niweze kukimbia maana hali haikuwa shwari kabisa.

Ile napiga hatua kukimbia mara Nasra akaidaka suruali yangu kwa nguvu sana, nilijaribu kurusha rusha miguu ili aniachie lakini hakuniachia alikuwa anaunguruma sana muungurumo wa ajabu.

Nikafanya kuufungua mkanda wa suruali ili initoke nikafanikiwa lakini sikuweza kwenda mbali. Sana yule Nasra ambaye nilikuwa najitoa katika mikono yake nilishangaa kumuona akitoweka akiwa amebeba ndoo ya maji kichwani.

Nikageuka nitazame ni kitu gani kilikuwa kimenishikilia kama sio Nasra.

Nikakutana tena na sura ya Nasra.

Nasra amenishika nisiondoke na Nasra anaondoka akiwa amebeba ndoo ya maji.

Nilikuwa nimepatikana jamani, haya mambo nilikuwa nikisimuliwa tu na kuyaona katika filamu sasa nilikuwa matatani.

Huyu nasra aliyenikamata nisiondoke alikuwa anatabasamu tu. Na mara upepo ukavuma na kichwa chake kikawa wazi kile kitambaa alichokuwa amejitanda kikatoweka.

Mamaaa macho yangu ambayo awali yaliona majeraha tu katika kichwa cha nasra sasa hayakuwa majeraha tupu bali kuna wadudu walikuwa wakiibuka na kutoweka, nilisisimka vibaya mno.

Na nikiwa nimeishiwa nguvu kabisa, nasra aliyebaki alizungumza.

‘’karibu sana mwandishi njia panda ya kuzimu.. tunakuhitaji sana huko.’’ Sauti ilikuwa ile ile ya nasra.

‘’Nasra… nisamehe, naomba unisamehe…’’ nilimsihi lakini badala ya kujibu sasa alifyatuka na kunichabanga kofi kali usoni.

Sikuona nyota nyota badala yake niliona vitu kama vichwa vya mbwa mwitu, na akili iliponikaa sawa niliona fisi wawili wakiwa mbele yetu. Hakuwa amenishikilia tena dada yule.

‘’tunaenda au unabaki…’’ aliniuliza.

‘’nabaki siendi huko siendii niache..’’ nilimjibu huku hamaniko likiwa limenishika vibaya mno.

‘’haya mi naondoka nakuacha na hao hapo rafiki zetu…’’nasra alinijibu huku akiondoka na kuwaendea wale fisi.

Nikageuka ili niwaone wale marafiki alioniambia, nikakutanisha macho yangu na mto si mto ziwa si ziwa lakini kikubwa zaidi niliwaona mamba wakisogea taratibu kuja eneo ambalo tulikuwepo.

Ndugu msomaji, sikusubiri nasra anielekeze nini cha kufanya nilikimbia nikampita nisijue hata ni wapi nilikuwa naenda.

Nasra akaniambia nipande juu ya mgongo wa fisi mmoja. Nilikuwa muoga lakini alipopanda na mimi nikapanda.

Kukosa kwangu umakini wa kuiga kila alichokuwa akifanya nasra nikajikuta nakaa tu utadhani ile ni taksi. Fisi akakimbia nikaanguka chini vibaya mno na wakati huo mamba wakizidi kusogea, nilipoanguka na wao wakaanza kukimbia kwa kasi kunifuata pale nilipokuwa.

Nasra alikuwa anaondoka zake akiwa ameshikilia masikio ya fisi wake.

Mamba wale walionyesha waziwazi kuwa walikuwa na njaa kali walikuwa wakisukumana huku na kule ili kuniwahi….

Nikapiga kelele kumuita mama yangu mzazi nikisahau kumuita Mungu wangu…..

Nilipofumbua macho mamba walikuwa wamebakiza mita chache tu kunifikia……

Na hapo likatokea jambo la ajabu kabisa lililonimaliza nguvu zaidi…..



Nikageuka ili niwaone wale marafiki alioniambia, nikakutanisha macho yangu na mto si mto ziwa si ziwa lakini kikubwa zaidi niliwaona mamba wakisogea taratibu kuja eneo ambalo tulikuwepo.

Ndugu msomaji, sikusubiri Nasra anielekeze nini cha kufanya nilikimbia nikampita nisijue hata ni wapi nilikuwa naenda.

Nasra akaniambia nipande juu ya mgongo wa fisi mmoja. Nilikuwa muoga lakini alipopanda na mimi nikapanda.

Kukosa kwangu umakini wa kuiga kila alichokuwa akifanya Nasra nikajikuta nakaa tu utadhani ile ni taksi. Fisi akakimbia nikaanguka chini vibaya mno na wakati huo mamba wakizidi kusogea, nilipoanguka na wao wakaanza kukimbia kwa kasi kunifuata pale nilipokuwa.

Nasra alikuwa anaondoka zake akiwa ameshikilia masikio ya fisi wake.

Mamba wale walionyesha waziwazi kuwa walikuwa na njaa kali walikuwa wakisukumana huku na kule ili kuniwahi….

Nikapiga kelele kumuita mama yangu mzazi nikisahau kumuita Mungu wangu…..

Nilipofumbua macho mamba walikuwa wamebakiza mita chache tu kunifikia……

Na hapo likatokea jambo la ajabu kabisa lililonimaliza nguvu zaidi…..

Yule fisi alinigeukia na kisha akanikazia macho. Nilipomtazama nikawa naona ile sura ya fisi ndani yake ni kama palikuwa na sura ya mtu. Na kabla sijajiuliza zaidi mara yule fisi akafungua mdomo wake.

‘’We fala si upande tuondoke au unataka kuliwa na mamba…’’

Mama yangu, nilihamaki, yaani fisi ana sura ya mtu nab ado anaongea. Yule fisi alinisogelea kisha akanikanyaga teke kwenye mbavu zangu halafu akaongea tena, sasa alinitukania mama yangu.

Ebwana eeh duniani kuna mambo ndugu msomaji lakini baadhi ya mambo uyasikie tu yaisikukute wewe.

Nilipanda katika mgongo wa yule fisi mtu nikamshika masikio akatoka mbio kali sana hadi tukampita fisi wa Nasra, hata sikujua ni wapi tunaenda ila nilikuwa juu ya usafiri wa fisi mtu.

Kadri tulivyozidi kwenda tulizidi kuingia gizani na hali ya hewa ilizidi kubadilika na kuwa joto sana.

Hatimaye yule fisi alisimama na kuniamrisha nishuke upesi huku akilalamika kuwa mimi ni mzito sana. Ipo siku na mimi nitambeba yeye.

Kusikia kauli ile nikatambua wazi kuwa sasa nilikuwa nipo katika hatua za mwisho kabisa za ubinadamu wangu na muda si mrefu nitakuwa mnyama tena mnyama mwenyewe fisi.

Mapigo ya moyo yalipiga vibaya sana, na nilikuwa najutia kutosikiliza maneno ya mama yangu mzazi juu ya hofu yake katika familia ile.

Nilishuka nikawa nimechutama nikitazama huku na kule katika giza lile, ile fisi ikaondoka zake lakini haikufika mbali mara ikarudi kwa kasi na kuniparamia pale nilipokuwa ikaniangusha chini.

‘’mpumbavu wewe umeniumiza mgongo yaani, umenirukia utadhani mimi chuma, shenzi kabisa..’’ fisi ile iliendelea kuniralua ikanichania nguo zangu nikabakia na nguo za ndani tu, ikaning’ata huku ikinipiga matteke, sikuweza kukabiliana nayo kutokana na hofu niliyokuwanayo lakini hali ilivyokuwa tete nikajisemea kuwa nisipokuwa makini yule fisi ataniua tena ataniua vibaya kwa sababu alikuwa ananing’ata kwa nguvu na mateke aliyorusha hayakuwa na masihara hata kidogo.

Nikajikaza nikasimama wima na kusema kama kweli nakufa basi nitakufa na shingo ya yule fisi, nilikuwa nimekasirika na nilijiona kuwa muda wowote ule nitakuwa mfu.

Nikamtegea yule fisi alete mdomo wake, pale chini nilipokuwa nilifanikiwa kuokota jiwe.

Kweli fisi akajileta, aisee nikamtandika jiwe moja la mdomo.

Fisi mtu akatowa yowe huku akikimbia kuelekea alipojua yeye mwenyewe. Na hapo mwanga ukatokea na kujikuta kumbe nilikuwa nimezungukwa na lundo la viumbe wa ajabu. Viumbe hawa nimewahi kuwaona katika filamu za kinaijeria na katika masimulizi ya kutisha.

Bila shaka hawa walikuwa ni misukule. Walikuwa wakinipigia makofi na nisijue katika nyuso zao walikuwa wanatabasamu ama vipi.

Na mara msukule mmoja uliofanania kwa mbaali na jinsia ya kike ulianza kunisogelea huku ukiwa umetanguliza mikono yake mbele. Mikono myeusi michafu yenye kucha chafu pia.

‘’Ni mimi nimekupatia lile jiwe, naomba uwe mume wangu..’’ kiumbe yula alizungumza huku akitetemeka na akizidi kunikaribia. Nikaanza kusogea nyuma, ilikuwa afadhali fisi anayezungumza kuliko kiumbe huyu aliyetaka eti niwe mume wake.

Nilichanganyikiwa sana. Wakati narudi nyuma nilijikuta naanguka chini na kiumbe yule akanifikia.

‘’Naitwa Manka’’ akajitambulisha jina lake huku akitokwa na mate machafu mdomoni.

‘’Mwachee’’ mara sauti kali ya kike ikaamrisha, yule binti akakimbia na kuniacha pale, wale wenzake wakawa wanamzomea.

Nilipogeuka nikakutana na mwanamke mweusi sana lakini huyu akiwa na mavazi ya kawaida.

Akanipungia mkono na kuniita, nikasimama na kumsogelea huku nikiwa katika hofu bado. Nikamfikia akanielekeza mahali nikaketi, akamaliza akaita jina ambalo sikulikamata mara moja.

Akajongea pale msichana mmoja ambaye hakuwa kama wale viumbe wengine.

‘’Utaongozana naye na kumfundisha biashara yetu….’’ Alimweleza kisha akaondoka na kuniacha nikiwa na binti yule.

Bila kuzungumza lolote yule binti alichukua maji maji na kuanza kunimwagia kichwani, nilipojaribu kujitikisa akasonya kisha akanitandika kwenzi kali kichwani. Nikashtuka na kutaka kusogea pembeni akaninasa kibao kikali usoni na hakuonekana kujali lolote kabisa.

Yaani ananipiga huku akiendelea kunimwagia yale majimaji ya baridi sana.

Baada ya hapo akanishika mkono na kisha akanipeleka hadi mahali palipokuwa na sufuria likiwa na mifuko laini ya plastiki.

Akaleta ndoo na kuanza kuchota maji yaliyofanana na damu akawa anbajaza katika ile mifuko na kufunga huku mimi nikitazama na baada ya hapo akaanza kunifundisha namna ya kufunga mifuko ile.

Nilijitahidi huku nikiwa naogopa sana. Hatimaye tulimaliza kujaza maji yale yaliyofanana na damu katika mifuko ipatayo hamsini.

Akanipatia sufuria moja nikajitwisha kichwani na yeye akachukua sufuria jingine, tukatembea hadi mahali fulani. Akanishtukiza kofi kali mgongoni. Na wakati nashtuka nikajikuta katika eneo lililonifanya niduwae.

Nilikuwa Kariakoo mtaa wa shule.

‘’utafanya kile ambacho nafanya, hayo uliyobeba ni maji ya kandoro… utauza kama ninavyouza ole wako usite kuuza…’’ alizungumza dada yule huku akiendelea kupiga mdomo watu wanunue maji yake….

Nilikuwa namfuata nyuma tu, mara abiria mmoja akaniita. Nikaenda akachukua mfuko mmoja.

Akanilipa shilingi mia moja, Mungu wangu eeh yule mtu alikunywa yale maji yanayofanania na damu kabisa, alikunywa huku akinilalamikia kuwa huenda yale maji hayajachemshwa.

Akanywa ule mfuko mmoja akamaliza akaongeza mwingine, nilitamani kusema neno lolote lakini huwezi amini kila nikitaka kusema sauti inakwama kabisa. Na sauti inapokwama yule dada ananigeukia na kunitazama kwa jicho kali sana.

Tulizunguka kule Kariakoo kwa takribani masaa manne kama sikosei tukawa tumemaliza kuuza yale maji ambayo si maji bali uchafu unaofanana na damu.

Hapa naomba niseme kitu mpenzi msomaji, yaani tangu nifanikiwe kuwa huru tena haya maji yanayoitwa ya kandoro siwezi kunywa nipo radhi kubaki na kiu lakini sio kunywa maji yale. Simaanishi na wewe hapo usinywe la hasha lakini wanasema kuwa usiloliona huwezi kuliogopa.

Mwenzenu niliona…

Wale watu ambao mchana walinunua uchafu ule na kunywa kama maji ndio haohao ambao usiku walikuwa wanaletwa kwa ajili ya kulima mashamba. Na walikuwa wanalima kweli.

Kidogo kidogo nikazoeana na yule dada na hapa ndipo nilipoyajua machafu mengi ambayo yananikera hadi leo kwa sababu hayataki kutoka katika kichwa changu.



Kule tulipokuwa hapakuwa na saa hivyo nitakuwa muongo nikielezea tukio kisha niseme ilikuwa saa fulani, yaani ile ilikuwa ni dunia ya wenyewe siku ambayo wa kujiita malikia ambaye bila shaka alikuwa ndiye yule mama mkwe wake Nasra akiamua tu hakuna kulala basi siku hiyo hamtaliona giza. Na siku watu wakimkera analeta giza hata siku tatu.

Kuna siku tulienda kariakoo kuuza yale maji mfanowe damu, tukarejea na maji kama pakiti tano hivi tukamueleza kuwa watu hawajanunua sana maji siku hiyo kuna mvua kubwa ilikuwa imenyesha.

Akatuuliza kwa upole sana ikiwa tunafahamu nini maana ya mvua, tukakubali kuwa tunaifahamu mvua vizuri.

Akacheka kidogo kisha akatuuliza nini maana ya mvua.

Tukabaki kimya tusijue ana maana gani kutuuliza lile swali, tulipokosa jibu akatuambia atatupa jibu baada ya muda mchache.

Akaondoka na kuingia ndani akaufunga mlango wake wa maajabu ambao unaonekana wakati wa kufunguliwa na kufungwa tu. Nyumba haionekani wala vilivyomo ndani. Yule dada aitwaye Adella ambaye ndiye ali9kuwa mwalimu wangu katika maisha yale mapya aliwahi kunieleza kuwa ndani ya ile nyumba kuna vito vingi sana vya thamani na samani zenyewe pia ni nyingi.

Baada ya kuingia ndani anga ilianza kutanda na kuwa nyeusi, tukadhani kuwa kama kawaida alikuwa ametupa adhabu ya kuleta giza siku tatu. Lakini hili halikuwa giza, mara ngurumo zikasikika na hapo mvua kubwa ikaanza kushuka.

Cha kushangaza mvua hii ni kama ilikuwa ikinyesha na kuingia katika beseni, yaani9 kila ilivyokuwa inanyesha maji yalizidi kuongezeka kwa kasi. Na wakati huo ile anga ikisogea taratibu ili ikutane na maji yale, Adella hakuwa vizuri sana katika kuogelea lakini mimi nilikuwa mtaalamu nilijitahidi sana kumsaidia Adella ili asinywe maji yale ambayo yangeweza kumsababishia kifo ikiwa angekunywa sana. Nilijaribu sana lakini baadaye tulikuwa tunaikaribia anga iliyokuwa inatema maji kwa wingi.

Sasa hapo sikuwa na namna yoyote nilifumba macho kukisubiri kifo, Adella naye alikuwa kimya akitumbua macho kuitazama ile anga ilivyokaribiana na uwepo wetu.

Ilikuwa hali ya kutisha sana.

Ghafla yale maji yakaanza kukauka tukaanza kushuka chini kwa kasi.

Tulipotua ardhini palikuwa pakavu kabisa na pembeni alikuwa amesimama yule malkia akiwa na beseni dogo tu.

‘’hiyo ndo maana ya mvua, je imenyesha mvua kubwa na ya kutisha kama hiyo…’’ alituuliza huku akitabasamu na kuondoka zake.

Ndugu msomaji, uchawi upo kama hauamini ni bora uamini tu lakini kamwe usijiingize katika shirki kwa sababu haimpendezi Mungu hata kidogo.

Yaani ardhi ile ilikuwa kavu kabisa na wenzetu walikuwa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.

‘’alituweka kwenye beseni’’ yule dada akaniambia likiwa ni neno lake la kwanza kunieleza kisha akaendelea.

‘’asante sana kwa kuniokoa wewe ni rafiki yangu kuanzia sasa..’’ aliniambia kwa sauti iliyojaa upole.

Na neno lile ndilo lililozua kizaazaa.

Neno lile likaujenga ukaribu zaidi baina yetu akaniahidi kuwa ipo siku tutatoka na kuishi duniani kama mtu na mke wake.

Mapenzi yakanza katika ardhi nisiyoielewa.

Adella alikuwa akinieleza mambo mengi sana ambayo amewahi kuyafanya, yalikuwa ya kutisha sana lakini aliniambia kuwa wanaotakiwa kutishika ni wale ambao wanaishi duniani sio mimi kwa sababu muda wowote ule nitatumwa kufanya kazi. Na nisijidanganye kuwa itakuwa rahisi kutoroka.

‘’Hivi wewe unadhani kwa nini ukiwa kariakoo haukimbii ukatoroka au huwa hauzioni gari za kwenda Temeke zimejaa pale shule ya uhuru… nikupe onyo yaani usije ukathubutu kutoroka kwa njia nyepesi kama hizo utajikuta matatani sana… acha kabisa Martin…’’ alinipa maonyo ya ajabu ajabu.

Ni kama vile alikuwa amenitabiria kuwa kuna kazi naenda kupewa katika siku hizo za karibuni.

Tulikuwa kama pacha vile na yule malkia alionyeshwa kupenda tunavyofanya kazi kwa ushirikiano.

Siku hiyo alituita na kutueleza kuwa kuna sherehe kubwa sana inatarajiwa kufanyika ndani ya siku saba zijazo akatueleza kuwa kila kitu kipo lakini hakuna msanii mzuri ambaye atatumbuiza katika hizo sherehe.

Na hapo akatuagiza kwenda kutafuta msanii ama wasanii wawili ambao watatumbuiza katika hiyo sherehe. Nilistaajabu sana lakini kwa sababu yule ADELLA alikuwa mkongwe hakustaajabu.

Na siku hiyo alinieleza kuwa ukiwa mzembe tu na usiyejishughulisha unaishia kuwa msukule ama unauzwa na ukiuzwa unaweza kuishia kuliwa nyama ama kufanywa kiti.

Maneno ya adella yalinichanganya sana kwa sababu yalikuwa mengi na yalikuwa yanatisha.

Usiku tuliondoka kama kawaida tulipofika mahali akanizaba kibao kikali sana mgongoni na kujikuta tupo katika ukumbi ambao nilikuwa naufahamu vyema na msanii aliyekuwa anatumbuiza pale jukwaani nilikuwa namfahamu, nilishtuka sana kujikuta ndani ya ukumbi ule na nilihisi kuwa muda si muda nitakutana na watu ambao nilikuwa nawafahamu.

Adella aliniacha nikiwa katika kona moja ya ukumbi, akajichanganya na baadaye nikamuona akimtuza yule msanii, alimrushia matawi matawi watu wakawa wanapiga kelele kumpongeza.

Hatimaye yule msanii akamuamuru adella apande jukwaani.

Adella akageukia upande niliokuwa nimesimama na kunifanyia ishara ya dole gumba, yule msanii alimkumbatia adella huku mapigo ya muziki yakiendelea.

Sijui ni mimi pekee niliyeliona tukio lile ama kila mtu aliona, huenda niliona mimi mwenyewe maana wangeona watu wengine lazima wangepiga kelele tu.

Wakati anamkumbatia adella alimfunga msanii yule kitu kama hirizi nyekundu kiunoni. Walipoachana akabaki na ile hirizi.

Akili zangu ni kama zilikuwa zinarejea hivi, nikajiona mjanja sana kuwa siwezi kuendelea kuishi maisha yale.

Nikajichanganya na kutoka nje ya ukumbi, huko nikaanza kuzubaa ni wapi nielekee kwa sababu sikuwa na nauli na pale nilipokuwa paliwa ni umbali mrefu sana hadi kufika nyumbani.

Siku hii ndipo nilizidi nkukiri kuwa ikiwa wewe ni mjanja basi kuna mjanja zaidi yako.

Nilizurura hapa na pale naingia hapa natokea kule na kujikuta nikiwa palle nilipoanzia awali.

Muda ulizidi kwenda hadi pakakucha, naziona gari najishauri kupanda lakini sipandi, natembea hadi huko na kurudi palepale,.

Kama ni adhabu basi ile ilikuwa ni adhabu kubwa sana, nawaona watu ninaowafahamu nikiwaona nakimbia na kujificha wakiondoka najishangaa ni kwanini sikiwakimbilia na kuwaeleza yote yaliyonitokea.

Hatimaye njaa ikaanza kuniuma, mchana jua kali akili inakuwa nzito kufanya maamuzi. Ilikuwa baada ya siku mbili nikiwa naishi kama kivuli nazurura huku na kule na hakuna anayenijali. Hatimaye baada ya siku mbili nikapata mwanamke wa kwanza kabisda kunisaidia.

Huyu alinichukua na kuniuliza nilikuwa nina matatizo gani, alikuwa ni mama mtu mzima anayejiheshimu, alinieleza kuwa amekuwa akiniona pale kwa siku mbili. Akanipeleka hadi nyumbani kwake, nikasema kuwa hatimaye nilikuwa nimepata msaada thabiti, alinipatia nguo nikabadilisha na kisha akanipatia chakula, baadaye akanieleza kuwa yeye ni mjane na watoto wake wote wameenda shule hivyo kwa wakati huo alikuwa akiishi mwenyewe.

Nilimpa pole na kumsihi kuwa anisaidie nauli niende nyumbani kwetu akaniahidi kuwa siku inayofuata nitaenda nyumbaji. Nyumba yake ilikuwa nzuri ya kupendeza sana hakika alikuwa amejipanga mama yule.

Usiku alinionyesha chumba ambacho ningelala ili siku ifuatayo niende nyumbani.

Nikaingia na kujifungia nikasinzia.

Baadaye usiku mnene nikahisi joto kali sana, nikatoa shuka, bado joto kali, nikatoa nguo nikaona si vibaya nikilala mtupu.

Ndugu msomaji katika hili uwe makini, hali kama hii ikikutokea usiku muite MUNGU wako akusimamie. Mimi nilichukulia kuwa hali hii ilikuwa ya kawaida sana kumbe nilikuwa nawekewa lile joto ili nivue nguo kwa hiari.

Nilipobaki mtupu nikasinzia, eti bila sababu nikaanza kumuota yule mama aliyenisaidia, nikamuona akinikumbatia huku akiwa yu uchi wa mnyama, nikawa naifurahia hali ile joto nalo likazidi. Baadaye nikajikuta nipo katika kuzini na mama yule.

Nilipokuja kushtuka nilihisi kuna harufu kali ya marashi pale chumbani. Na nilikuwa natokwa jasho haswa…..

Nilitapatapa huku na kule kisha nikalala tena hoi.

Asubuhi na mapema nilimsikia yule mama akiniita, nikavaa nguo zangu na kutoka nje hadi alipokuwa.

Alinipokea kwa tabasamu zito kisha akanieleza kuwa yeye alikuwa anataka kutoka akanipatia nauli na kunieleza kuwa nikifika nyumbani nimsalimie mama yangu.

Nikaipokea nauli, akanifungulia mlango nikatoka nje.

Ebwana eee, ukisikia wabaya watu wanyama wanasingiziwa ndo hii.

Nilijikuta nipo katika ardhi ileile ya maajabu.

‘’ulienda kwa huyo mama kufanya nini siku mbili zote hizi..’’ ilikuwa sauti ya adella akiniuliza kwa hasira kali. Nilikuwa nimepigwa na bumbuwazi nisijue ni kitu gani cha kujibu.

Yaani akili haikuwepo kabisa, yaani kumbe kumuamini kote kule yule mama alikuwa ndo yule malikia.

Nilitamani kusema neno lakini kabla sijaongea lolote adella aliita jina la kitu nisichokijua, kisha yeye akaondoka zake.

Mama yangu, akaja yule fisi mtu alikuwa amevimba kwa hasira.

Kumbe adella alimwamrisha aje kunisulubu.

Fisi akafanya kweli, safari hii haikuwa kama mwanzo, sikuona jiwe wala fimbo ya kumchapia.

Fisi akanirukia na kupitisha meno yake kwenye paja langu… maumivu makali yakanipitia.

Nilipagawa sana………

Akanifuata tena na kuniangusha chini kisha akanibamiza na kichwa chake katika mbavu zangu.

Nikashindwa kupumua vizuri.

Yule fisi akarudi nyuma tena kisha akanifuata kwa nguvu sana, nikajua kuwa kwqa namna yoyote ile alikuwa anakuja kunimalizia…

Nikafumba macho huku nikiuma meno kwa nguvu..



NIKIWA nimetulia pale nikikisubiri kifo changu mara nilisikia kilio kikali sana cha mwanaume ambaye alikuwa katika maumivu makali sana. Nikajikuta nikifumbua jicho langu kutazama. Nilimuona yule fisi mtu akigalagala chini huku akijitupa huku na kule.

Na baada ya hapo akatulia tuli huku akianza kuvimba kwa kasi kubwa na kelele kubwa zikiendelea kupigwa na yule fisi mtu.

Uvimbe ule ukaanza kuisababisha ngozi yake ianze kutatuka kana kwamba hapo awali ilikuwa imeshonwa na uzi wa kawaida.

Ilitatuka na baadaye kikasikika kishindo kikubwa sana wakati fisi yule akipasuka na kusambaratika vibaya mno.

Matone mazito ya damu ya moto kabisa yalinirukia, na hapo nikasikia tena mluzi mkali sana ukipigwa.

Ghalfa zikasikika shwangwe na hapo ukawa uwanja wa kugombania vilivyogombaniwa, misukule wale wachafu kabisa wakaingia katika ukumbi wa kuwania mabaki ya kupasuka fisi yule.

Walifika kwanza kwangu na kunigombania huku wakinilamba zile damu kwa matamanio, kucha zao zilikuwa zinaniumiza lakini nilitulia tuli kwa sababu sikujua naweza vipi kujiokoa kutoka katika hali ile.

Niliwaona misukule wengine wakigombania utumbo, wengine waligawana ngozi. Na baadaye msukule mmoja ukapita na kichwa cha yule fisi, kichwa ambacho kilikuwa na sura ya mtu kabisa.

Nikiwa nimeganda pale kama barafu mara alifika mbele yangu yule mama mweusi ambaye alikuwa akiitwa kwa cheo cha malikia.

‘’hicho kisichana chako kinachojifanya kukupenda kilitaka ufe leo nimekuokoa naomba utambue hilo….’’ Alizungumza vile kisha akatoweka.

Dakika mbili mbele ADELLA akasimama mbele yangu akitokea anapojua yeye mwenyewe.

‘’Martin nina ujauzito wako….’’ Alinieleza. Nikatumbua macho na kujiuliza ni lini mimi nilishiriki zinaa na binti yule. Lakini hakuonekana kutania kabisa alikaa akisubiri nijibu alipoona kimya akaendelea.

‘’Tambua kuwa mimi ni mzazi mwenzako…na utaniona Martin utake usitake…’’ alimaliza kusema hayo akaondoka zake. Akarejea alipotambua yeye mwenyewe.

Nilibaki kustaajabu ni kitu gani kile, huyu mama anadai kuwa ameniokoa yeye Adella alitaka nife sasa anakuja Adella anasema ana ujauzito wangu na anaenda mbali zaidi na kusema iwe isiwe lazima tutaoana. Niliduwaa sana.

Baada ya hali ya hewa kutulia, aliagizwa mtu kuja kunipa majukumu na hili jukumu la sasa nilitakiwa kwenda nikiwa mwenyewe bila kuambatana na Adella.

Niliagizwa kwenda kumpa motisha yule msanii wa mziki ili aweze kuhudhuria tamasha katika siku ile maalumu ambayo ilitajwa bila mimi kuitambua.

Alikuwa yule msanii ambaye Adella alianza kumwandaa tayari.

Nilijiuliza nitaanzia wapi bila adella lakini ilikuwa na sikutegemea nikapewa masharti yote ya kufuata. Niliona kuwa ni masharti magumu. Lakini nilipopigwa kibao na kujikuta natokea nyumbani kwa yule msanii ndipo niligundua kuwa mwanadamu ni kiumbe hatari sana, ishi na Mungu kila wakati ili kupambana na mambo haya, lakini bila nguvu zake jamani huko majumbani kwetu kuna mengi sana yanatokea.

Nilifika nyumbani kwa yule msanii, sijui nilikuwa naendeshwa na akili ya nani jamani. Haikuwa akili yangu kabisa, nilikuwa ninalo dumu lililokuwa na maji yale yanayofanania na damu. Nilifika kama nilivyoagizwa nikaliendea jokofu na kulifungua kisha nikaweka lile dumu ndani yake.

Nilikuwa nahofia sana yule mwandishi akisimama itakuwaje. Nilidhani ataniona lakini nilihakikishia kuwa hataamka mpaka nitakapoamua….

Baada ya kuweka maji yale kwenye jokofu nikawasha jani fulani hivi likafuka moshio kidogo kisha nikalizima.

Hivi umewahi kupatwa na kiu kikali sana usiku, ukakurupuka na kwenda kunywa maji.

Binafsi sijui kama ni kila tukio la aina hii linakuwa na maana mbaya ama la lakini naelezea ambacho nilishuhudia tu.

Baada ya moshi ule yule msanii alianza kuhangaika, wakati huo nimesimama nyuma ya mlango ambapo mimi namuona na yeye hanioni. Alisimama na kwenda katika jokofu, akachagua lile dumu langu.

Akafungua na kuweka katika glasi na kugida kwa fujo maji yale yafananayo na damu. Aligida kwa wingi mno, kisha akarejea kulala. Nikaliendea jokofu na kuchukua dumu lile likiwa limesalia na damu ile kiasi.

Kisha nikatoka nje nikapokelewa na fisi mtu mwingine, safari hii sikuuliza nikapanda mgongoni nikamshika masikio tukaondoka kwa kasi hadi kambini.

Na huko nikakuta nimeandaliwa sherehe fupi kwa kufanikiwa zoezi lile.

Nilipokuwa na adella nilikuwa nakula ugali na mboga za majani lakini siku hii nilikaribishwa chakula ambacho kwao wanakiita chakula bora sana.

Zilikuwa nyama nisizozielewa kabisa, na pia palikuwa na maji yafananayo na damu.

Nilikaribishwa kwa shangwe lakini sikuweza kula. Zile sura zilikuwa ngeni kabisa machoni pangu sikuwa na yeyote niliyekuwa namfahamu.

Mara bila mimi kusema neno lolote walianza kucheka kwa sauti ya juu na kisha mmoja wao akawanyamazisha wenzake na kuanza kuzungumza na mimi.

‘’NDUGU mwandishi, yaani ukakosa vitu vyote vya kuandika katika ulimwengu wenu mchafu huo ukaona uanze kutupekua na sisi ili utuandike…. Unajiamini kitu gani wewe kijana….’’ Alinipiga piga begani. Na hapo akaendelea.

‘’ukaona kutuandika haitoshi umekuja huku hata mwezi mmoja bado umempachika mimba binti yetu mchapakazi, hizo gharama za kule mtoto utaziweza mwandishi… ama una uwezo wa kumlipia mahari……’’ alinisanifu na wala hakuwa ameniuliza, akaendelea kunitazama machoni huku akichukua pande la nyama, ni hapo nikaliona lilikuwa limeambatana na sikio la mwanadamu, akarusha lote mdomoni huku akijilamba mikono yake akatafuna na kumeza kisha akatabasamu na kuendelea.

‘’unaotuona hapa sisi ni wazee wa huu ufalme na tumezipata taarifa kuwa umemjaza mimba malikia mtarajiwa wa ufalme huu…. Kwa hiyo wewe umetoka zako huko duniani na ghafla unataka uwe mfalme huku usipopajua.. una jeuri gani wewe……’’ akacheka kidogo na kuendelea, ‘’tumeipanga zawadi yako kwa hiki ulichoamua kufuata huku, tunataka tukupe zawadi ya mengi ya kushuhudia ili ukirejea huko ulimwengu dhaifu uwaandikie na wao wayasome na kutambua kuwa hawawezi kukabiliana na sisi ikiwa wataendelea na huo udhaifu…… kazi uliyoianza ni nzuri sana lakini kuna ugumu fulani, yule msanii amegoma kuja kwenye tamasha letu. Tunahitaji umlete kinguvu sasa maana tumejaribu kistaarabu imeshindikana…… tunahitaji umtumie mama yake mzazi…… na shughuli hiyo ifanyike ndani ya siku nne utuletee majibu, tunakurudisha duniani kwa siku hizo nne kwa ajili ya kuifanya hiyo kazi.. usijidanganye kuwa utatutoroka kwa sababu ulimwengu wenu dhaifu upo katika mikono yetu, ni wapi utakimbilia. Pia tutakuwa nawe kwa ajili ya kukupa maelekezo, sherehe yetu haitanoga bila kuwa na msanii. Ukimaliza hili tutafikiria namna ya kukupunguzia adhabu kwa sababu tangu uje huku haujaadhibiwa ujue… hebu’’ akasita na kisha akazungumza kabila nisilolijua. Na hapo akaletwa bwana mmoja asiyekuwa na mikono na mguu mmoja. Nilikuwa namfahamu kabisa sura yake haikuwa ngeni, aliwahi kuwa mwanasiasa maarufu.

‘’huyu hapa tumekula mguu na mkono na tutamla hadi amalizike kwa sababu alijifanya mbishi na mjanja mjanja’’ alinieleza. Halafu akaletwa mwanamke.

‘’unamuona huyu na mimba yake, hii mimba ina miezi thelathini hadi sasa, hatutamuachia kirahisi azae anajua alichotufanyia, ataumwa uchungu lakini hatajifungua…..’’ alinieleza na kisha akarejea tena katika mazungumzo.

‘’tunakuagiza kuifanya kazi, kaifanye kazi na hautakuwa na ugomvi na sisi lakini ukileta kujua sana hakika utateseka sana na huo si mkwara tupo makini na tunachokifanya.. tunakurudisha duniani uende kwa mama mzazi wa huyo msanii, ni kipi utamfanya ama kipi utatakiwa kufanya ukifika duniani tutakutumia majibu…. Simama ‘’ aliniamrisha nikasimama………

Kama nilidhani mambo magumu yalikuwa kumuona mwanadamu akimla mwanadamu mwenzake, nilikuwa najiongopea kuna mengine magumu zaidi yaliyokuwa yakinisubiri.

Kuna jambo moja tu msomaji nilikuwa nalisahau kila siku, nilikuwa namsahau ama sikuwahi kumtegemea Mungu. Ni vile sikukuzwa katia misingi hi indo maana niliteseka sana, na huenda haya yalinitokea ili nije kukuandikia wewe usome kisha ujifunze……









Katika kipengele kimojawapo katika masimulizi haya nilisema kuwa wabaya watu jama wanyama kama paka na fisi hawa wanatumwa tu hawana ubaya wowote.

Na hawa watu wabaya hawazaliwi na roho mbaya bali mazingira na matukio yanayowatokea maishani husababisha wawe na roho mbaya.

Mimi nilishiriki kutimiza matakwa ya watu hawa wenye roho mbaya.

Nilifungwa akili jamani, hadi sasa hivi sijui ilikuwaje hadi nikashindwa kabisa kutoroka. Acha niamini kuwa nilifungwa akili katika kiwango cha juu sana…

Nilitupwa duniani, nikajikuta nipo katika chumba kimoja kilichokuwa na meza na viti viwili huku pia pakiwa na kitanda na godoro.

Kwa kifupi kilikuwa ni chumba ambacho angeweza kuishi kijana ambaye bado hajaoa. Sikuwa nafanya kazi yoyote, lakini kila siku nilikuwa nakuta chakula pale ndani, kilikuwa chakula kizuri sana kwa kutazama, wakati mwingine kuku, pilau, nyama ya mbuzi na kadhalika.

Ilikuwa baadaye sana nilipoambiwa kuwa zile hazikuwa nyama za kuku wala mbuzi bali nilikuwa nalishwa mizoga ya fisi na wakati mwingine nyama za watu ili niwe na roho mbaya.

Naam, ile roho ikajipandikiza na nikajikuta nayazoea maisha yale kwa juma moja tu.

Na hapo nikaingia kazini.

Mama wa yule msanii alikuwa ni mjamzito, ujauzito ule ulikuwa una miezi ipatayo nane na nusu. Muda wowote ule alitakiwa kujifungua.

Ni hapo ndipo nilipofanya nilichoagizwa, nilimfuatilia yule mama alipokuwa akifanya maozezi ya kutembea, nikapishana naye na kisha nikachota mchanga katika hatua alizoacha barabarani. Nikaenda na ule mchanga ndani kwangu, usiku wakaja wazee kuuchukua huku wakiniambia kuwa nimefanya kazi nzuri.

Ni hapo yalifuata mateso makali kwa yule mama, wanasema uchungu wa mwana aujuaye mzazi, sasa jiulize ule uchungu unakuja lakini mtoto hatoki.

Walimwengu wana mapana jama.

Niliagizwa niende kumshaurti yule msanii ambaye alikuwa ni mtoto mkubwa wa mama yule. Niliamriwa nimshawishi aende kwa waganga kwa sababu hospitali pekee haitoshi.

Kweli nikaenda kumsalimia yule mama pale hospitali nikijifanya mimi ni jirani mwema, baadaye nikamvuta yule bwana na kisha nikamuelezea kuwa hata mimi mama yangu aliwahi kupatwa na tatizo kama lile, nikamsihi sana kuwa lile si tatizo la kawaida na asipokuwa makini basi mama yake ataaga duniani.

Nani kama mama……. Kusikia kuwa mama atapotea akanishika mkono na kuniuliza ni kipi anatakiwa kufanya.

Kitendo cha kunishika mkono likawa ni kosa kubwa sana kwake.

Akajikuta akinisikiliza kila nilichokuwa nasema.

Hatimaye baada ya siku mbili nikamfikisha kwa mganga ambaye alikuwa mwenzetu pia.

Akamchanganyia madawa, akampa na maelekezo.

Ile tunarudi hospitali mama alikuwa amejifungua tayari mtoto wa kike.

Yule msanii akanishukuru sana lakini nikamwambia kuwa aende kumshukuru yule mganga.

Kweli akaenda na huo ukawa mwisho wake kuishi duniani.

Niliumia sana mpenzi msomaji, kwani nilikuwa duniani wakati wakitangaza kuwa msanii yule amekutwa akiwa amekufa kitandani kwake bila kuwa na kovu hata moja.

Siku ninayopata taarifa hiyo ndipo ikawa pia siku yangu ya mwisho kuwa katika nyumba ile nikarejea kule kambini.

Sikujua nini kilikuwa kinaendelea huku lakini kumbe kuna jambo moja baya sana lilikuwa linaendelea chinichini.

Kwanza nilimkuta yule msanii kule akiwa anateseka sana, niliogopa kumtazama machoni kwa sababu nilishiriki kumfikisha hapo.

Ukiachana na hili, jambo ambalo lilinishangaza na kisha kuniweka katika wakati mgumu zaidi katika maisha ya huko. Ni suala la Malkia na Adella kugombana, kisa kikuu ni baada ya malikia kusikia kuwa Adella ameshika mimba.

Vilikuwa ni vita baridi ambavyo vilikuwa vinanisubiri nifike ili viwake rasmi.

Wote walikuwa wamejipanga, wanasema kuwa wapiganapo mafahari ziumiazo nyika.

Niligeuka nyika katika hili.

Wa kwanza kuzungumza na mimi alikuwa ni Adella punde tu baada ya kurejea, alinieleza kuwa kuna vita inaibuka hivyo nijiandae lengo lake ni kunitorosha ilimradi tu nitoweke wakose wote.

‘’mkose wote, unamaanisha nini’’ nilimuuliza.

‘’malikia anakuhitaji na mimi nakupenda martin, malikia anataka kukupeleka njia panda ya kuzimu na mimi sihitaji uende huko..’’

‘’Mamaa weee njia panda ya kuzimu ni wapi kwani, Adella nisaidie nisaidie sitaki kwenda huko…’’ nilimsihi wakati hata sijapajua njia panda ya kuzimu.

Alipotaka kunieleza mara upepo ulivuma akanyamaza kimya.

Upepo ulipopita akanieleza kuwa malikia amejipitisha pale ili aweze kusikia ni kitu gani walikuwa wanazungumza.

Ile adella anataka kuendelea kuzungumza tena, mara wakafika watu watatu na kunieleza kuwa nilikuwa ninaitwa na malikia, hawakuwa na subira wakanivuta na kunipeleka nilipohitaji. Wakanisukuma ndani nikajikuta mbele yangu nikitrazamana na yule mwanamke anayeitwa malikia.

‘’acha kuwa mpumbavu kijana, yule binti anataka akupeleke njia panda ya kuzimu, epuka tamaa za muda mfupi ukiingia huko hautoki. Lengo langu nataka uishi vizuri hapa.. maana huko njia panda ya kuzimu, utakatwa ulimi nab ado utalazimishwa kuongea, utatobolewa macho yako na utalazimishwa kutambua rangi, hautapewa chakula nab ado utalazimishwa kufanya kazi. Ikiwa upo tayari muendekeze yule binti na hapatakuwa na muda wa kujuta’’ alimaliza kisha akanisukuma nikajikuta nipo nje.

Nilikuwa nimechanganyikiwa vibaya sana jamani, hasahasa maneno ya malkia yalinifanya nipagawe maradufu.

Kutobolewa macho, kukatwa ulimi…. Ama kweli hapo ndo palikuwa njia panda ya kuzimu…..

Sikujua ni kitu gani nifanye kwa wakati ule…..

Nikiwa bado palepale chini nilianza kuusikia mwili wangu ukiwa mzito na giza likaanza kutanda, wakati nazidiwa na usingizi ule niliwaona watu wawili wakiwa na ghadhabu kuu wakinikaribia, upandfe mmoja alikuwa ni malikia na upande mwingine akiwa ni adella.

Waliponifikia nikamwona adella akimkaripia malikia, malikia naye akamjibu adella sikuweza kusikia walichokuwa wakisema lakini kila mmoja alikuwa akijiamini nkuwa yeye ni mbabe kuliko mwenzake.

Mara wakatimua mbio na kunifikia, hapa sasa nikayasikia maneno yao machache.

‘’kama ni hivyo basi kila mmoja achukue nusu’’

Malikia akanishika miguu yote miwili na adella akanishika mikono, kila mmoja akaanza kuvuta kuelekea upande wake, walinivuta nikawa napiga makelele, lakini wao hawakujali waliendelea kunivuta, na baada ya muda kila upande ukaongeza wavutaji, hapa sasa niliipata joto ya jiwe.

Sauti haikutoka tena tumbo likawa linaniuma sana na upande wa uti wa mgongo pia.

Nikaanza kuhisi ngozi yangu ikianza kuachana, hapa sasa sauti haikutoka tena na nilikuwa naumia sana, waliendelea kuvuta hadi nikaliona tumbo langu likifunguka.

Nilitamani kusema neno lakini sikuweza kusema.

Nilitambua kuwa muda wowote ule kuwa mwili wangu unatengana nusu kwa nusu na hapo historia ya maisha yangu inafika ukomo.

Nikajaribu kupambania uhai wake katika dakika ya mwisho…. Nikajigeuza kwa nguvu sana huku nikiwasihi wasiniue.

Mara wakaniachia, na hapo nikaweza kufumbua macho yangu. Nilikuwa nipo pale chini nikigalagala huku tumbo likiniuma vibaya sana. Jasho lilikuwa linanitoka, lakini tumbo halikuwa limechanika kama nilivyoona katika maluweluwe yale.

Nilijaribu kusimama nikaanguka chini.

Nikasikia sauti ya kicheko kikali, nikageuka na kukutanisha macho yangu na malikia, nilipogeuka upande mwingine nikakutanisha macho na adella.

Kisha wote wakapotea….

Huo haukuwa mwisho bali mwanzo wa kuteseka.





Usiku mnene ulinikuta katika mtihani mwingine.

Nimesema ni usiku japokuwa sina uhakika, awali niliwaeleza kuwa huku usiku ulikuwa wa kufikia tu, akiamua malkia kuleta giza analeta, akiamua iwe mwanga analeta pia.

Nilishtuka kutoka gizani nikataka kuuliza ni nani anayenitikisa lakinmi nilishtukia nikiwa nimezibwa mdomo.

‘’nifuate Martin’’ sauti tulivu ya kike ilinisihi. Nikaitambua kuwa ilikuwa sauti ya Adella, akanivuta na kunisogeza pembeni.

‘’Martin, unatakiwa kuchukua maamuzi magumu sana ama la sivyo kuna jambo baya sana linaenda kutokea. Nilidhani ni mimi na malkia pekee tunaokuwania lakini kuna watu duniani wanakupigania urudi huko. Hii sasa ni vita, sikuangalia kwa makini sana lakini kuna mwanamke nimemuona kama anafanana na wewe sijui iwapo ni dada mama ama mama mdogo’’ alisita, sasa niliweza kuiona sura yako kwa mbali macho yalikuwa yamelizoea giza.

Maneno aliyozungumza sikuwa nikiyaelewa bayana, akanivuta karibu yake akachukua vitu fulani nisivyovitambua akavitafuna na kisha akanipaka chini ya macho yangu na kisha akanizaba kibao kikali usoni, nilitaka kupiga kelele kwa maumivu niliyopata lakini aliwahi kuniziba mdomo na hapo sasa akaniwekea mkono wake, mkono wake ukaanza kutanuka na hapo nikaiona sura ya mama yangu nikamuona Nasra yule mwanadada ambaye naweza kusema alikuwa daraja la mimi kufikia pale nilipo na pia nikamuona mwanaume fulani ambaye sikuwa namtambua sura.

‘’wote hao wanatakiwa kuuwawa mara moja kuna ambao wanafanya maombi lakini ni dhaifu katika imani, wapo wanaojaribu kwenda kwa waganga lakini bado hawajatimiza masharti ya waganga. Hawa wote ni maadui wa ufalme huu, kanuni ya ufalme huu ni kwamba tunakuleta sisi na sisi tutaamua wewe kurudi huko… sasa Martin ikiwqa ningeamua kukaa kimya basi hawa watu watatu wote wangeuwawa na siku ungeletewa miili yao hapa ili uwale nyama wasije wakaonekana tena duniani, maana bila wewe kula nyama yao watakuwa wakionekanba mara kwa mara na kuzua utata….’’ Alinizungumza kwa sauti ya chini huku akiwa amenikazia macho yake.

‘’sasa Martin ni kitu gani wahitaji zaidi nifanye ujue kuwa ninakupenda. Nimeamua kufanya jambo la hatari kama hili kwa manufaa yako lakini bado hauamini kuwa nahitaji kuwa mke wako…’’ alizungumza Adella kwa masikitiko.

‘’Adella, naomba unisaidie sana wasimuue mama yangu… mimi nitawapa chochote wanachotaka ilimradi wamuache mama yangu…’’ nilimsihi Adella.

Akacheka kidogo kisha akaniambia, ‘’hakuna wanachohitaji kwako zaidi ya roho yako, na hii sio kwamba wewe ndo unaamua la, wakiamua wanaichukua tu….. jambo la kufanya sasa Martin simama kama mwanaume, simama upigane….’’ Alinisihi huku akionekana kunitia ujasiri.

‘’mimi nipigane na malkia…’’ nilimuhoji huku nikiwa katika mshangao.

‘’kama haupo tayari kupambana basi uwe tayari kumla mama yako nyama…’’ alinijibu kwa hasira.

Jibu lile likaniingiza katika mtihani mgumu sana.

‘’sikia Martin nimemua kusimama kwenye upoande wako moja kwa moja… na wewe uwe upande wangu hasa… nahitaji ufanye jambo moja tu ili tuweze kuingia katika hii vita na kuokoa watu wasiokuwa na makosa……’’

‘’niambie lolote na nitafanya Adella niambie…’’

‘’nahitaji unywele walau mmoja tu wa malkia… utajua jinsi ya kuupata najua roho itaniuma lakini nakuruhusu kama ni kulala naye fanya hivyo lakini uje na uywele wake walau mmoja …..’’ alinieleza na hakungoja jibu, akapotelea gizani akiniacha nimeketi bila msaada wowote.

Sijui yalipita masaa ama dakika ngapi mwanga ukachukua nafasi yake, wale misukule wakaingia mashamabani wakisaidiwa na wafanyakazi wapya ambao walikuwa wakipatikana kwa kunyweshwa yale maji ambayo kwa macho yao waliona ni maji lakini ilikuwa ni damu.

Mashamba yalilimwa na kwa bahati nzuri mimi nilikuwa napewa nafasi ya kusimamia hii ilikuwa ni kwa sababu ya ukaribu wangu na malkia kimahusiano.

Siku hii nilishtuka na kumuona malkia mwenyewe akiwa anasimamia yale mashamba, nikakumbuka kuwa Adella alinieleza kuwa ninatakiwa kuupata unywele wa malikia, nilimuona jinsi alivyokuwa amejitanda kichwa chake hakuonekana nywele zake hata kidogo.

Nikasimama kutoka pale nilipokuwa na kujongea hadi alipokuwa amesimama.

‘’shkamoo mama.. malkia..’’ nilimsalimia huku nikiwa natetemeka, mwanamama yule alinigeukia na kunitazama jicho kali sana, jicho lake ni kama lilikuwa lina miale fulani ya moto.

Nilitishika sana.

‘’hiyo shkamoo hapa si mahali pake…..’’ alinijibu kwa kiburi.

Nikataka kuondoka akaniita, safari hii jicho lake halikuwa kali kama mwanzo. Alikuwa akinitazama tu na kisha kana kwamba ana umri sawa na mimi akaanza kuniomba msamahga ikiwa amezungumza vibaya.

Nikatumia fursa ile kujaribu kumlalamikia malkia kuwa hanitendei haki hata kidogo.

Mtego ukaenda sawa, akaniambia ni kweli hanitendei haki kwa sababu mimi namtesa.

Nikaduwaa, yaani hapo na hapo ninamtesa mama huyu.

Lakini sikutaka iwe mshangao wa muda mrefu nikamwambia nahitaji kuzungumza naye.

Akaniambia kuwa ataniita nyumbani kwake tutaketi na kuzungumza.

Akaendelea kusimamia shamba lile ambalo sijui lilitarajiwa kupandwa zao gani.

Nikajiweka kando kidogo hadi pale kilipovuma kimbunga cha ajabu, kimbunga kile kilivuma kuja upande wangu, nikajaribu kukikwepa kikawa kinanifukuza kwa nguvu, na kisha kikanipiga gwala nikaanguka chini, kikaendelea kuvuma huku kikininyanyua.

Kilipokuja kutulia nilikuwa ndani ya nyumba ile ya kifahari nba nilikuwa nikitazama na mwanamke mrembo wa kiarabu.

‘’karibu sana laazizi wangu…’’ sauti nyororo kabisa ilisema nami.

‘’wewe ni nani..na hapa ni wapi’’ nilihoji huku natweta kwa hofu.

‘’umehitaji kufanya mazungumzo na mimi…. Nipo hapa Martin sema nami kipenzi changu…’’ alizungumza binti yule mrembo katika maana halisi ya urembo.

Nilijisahau kabisa kuwa pale sikuwa katika dunia ya kawaida, nikajikuta nazipata zile hisia za kimatamanio kabisa ya waziwazi.

Nikajisahau kabisa kuwa nilikuwa nimeagizwa unywele wa malkia. Binti yule akanisogelea akinyata hadi akanifikia katika kochi ambalo nilikuwa nimetulizwa pale na kile kimbunga, akanishika mkono na kunivuta kuelekea nisipopajua.

Aliniingiza katika chumba kikubwa kilichokuwa na godoro kubwa sana akanisihi nilale pale. Nikatii amri yake na kujilaza pale.

‘’nahitaji kukupeleka katika dunia yap eke yako, nahitaji ukitoka hapa usimguse mwanamke mwingine bali mimi tu malkia wako’’ alizungumza kwa sauti nyororo sana iliyojaa mahaba tamanishi.

Nilipolala yeye akasogea kando na kisha akapiga makofi mawili.

Mama yangu wee….. lile godoro likaanza kubonyea na kisha taratibu likaanza kupotea na sehemu ile pakawa maji.

Kama hiyo haitoshi nilipojaribu kupiga mbizi nikahisi mguso fulani mgumu katika mbavu zangu.

Nikageuka kutazama ni kitu gani kilikuwa kimeniguza ni hapo nikakutana na domo kubwa la mamba…..

Hakuwa mmoja bali huo ukawa mwanzo wa kuwaona mamba wengi katika godoro lile la kimauzauza lililogeuka kuwa majki tena maji yenye mamba.

Nilipiga mayowe jamani, nililia sana huku nikiomba msamaha.

Nikimkwepa mamba huyu ninakutana na mamba mwingine……

Mara nikasikia kitu laini kabisa kikipenya katika mapaja yangu nikaingiza mkono na kukitoa.

Lahaula alikuwa ni nyoka mrefu mweusi.

Kitendo cha kumshika akavimba vipasa kisha akarusha kichwa chake kunifuata mimi…

Kifo nikakiona kikiwa katika mdomo wangu…..

Nyoka yule akanigonga katika mikono yangu, na hapo kimya kikatanda na matone ya damu yakaanza kuvuja kutoka katika dari pale ndani, damu ile ikawa inanimwagikia mimi.

Mamba wakaanza kunilamba kwa fuko…

Mamba ana ulimi mgumu jamani.

Hivi ni sayansi inasema kuwa mamba hawezi kutoa ulimi nje, mbona hawa mamba walikuwa wanbanilamba kwa fujo vile sasa……

Nguvu zikawa zinaniishia kadiri walivyokuwa wakinishambulia…

Kicheko cha yule malkia kiliendelea kutawala…..

UTATA…….



 Kitu cha kushangaza ni kwamba licha ya wale mamba kuwa na sura za kutisha lakini nilijikuta nikifurahia namna ndimi zao zilivyokuwa zikiulamba mwili wangu, hapo awali nilikuwa nahisi kuumia lakini sasa ilikuwa ni raha ya ajabu sana. Nilitamani waendelee kunilamba vilevile, kweli wakaendelea hadi nilipofumba macho yangu.

Nilipofumba macho yangu nikawa katika ulimwengu mwingine kabisa nikiwa na yule malkia ambaye alikuwa amejiweka katika umbile la binti mrembo wa kiarabu.

Nikisema mrembo namaanisha haikuwa rahisi kumtoa kasoro, hata kile kicheko chake kikubwa kilikuwa kinasisimua bado.

Nilikuwa naye kitandani na ni yeye aliyekuwa akinilamba huku na kule.

Baadaye akaanza kuchojoa nguo zake.

Hatimaye akabaki mtupu na hapo nikaziona nywele zake jinsi zilivyomwagika mgongoni, palepale ikanijia ile kumbukumbu kuwa adell alaikuwa ameniagiza unywel wa malkia yule.

Nikatii alichotaka nifanye binti yule nikiwa katika mahaba mazito nikazifikia nywle zake na kukata kiasi cha nywele kwa kutumia meno yangu, nikaziacha mdomoni huku nikijipa tahadhari kubwa sana nisije nikazimeza.

Kweli mahaba yakachukua nafasi yake huku akinipa ahadi nzuri nzuri ambazo kwa mwenye tamaa angeweza kuingia mkenge, lakini mimi nilitaka kurejea duniani tu huku nikiwahi lisije likamkuta baya lolote mama yangu.

Baadaye akapotea yule malkia, kisha nikajikuta nipo katika kukimbizana na mamba. Nilikimbia kwa kasi hadi nikawa mbali na upeo wa wale mamba, na hapo fahamu zikanikaa sawa tena.

Nilikuwa nje ya kile chumba, nikiwa hata sijavuta pumzi zangu vizuri nikamsikia adella, alikuwa pembeni yangu na aliniuliza iwapo nilifanikiwa.

Hapo ndipo nikakumbuka kuwa niliagizwa nywele, nikakumbuka nilifanikiwa kuzihifadhi mdomoni.

Ila katika kukimbia ile dhahama ya mamba nahisi kuna kitu kilitokea.

Nilizimeza zile nywele bila kufahamu kama nilikuwa nazimeza.

Nilimueleza adella, akanieleza mara mbilimbili niseme ukweli nisimdanganye akajihangaisha bure.

Nilimsisitiza kuwa hakuna hata chembe moja ya uongo katika maelezo yangu.

Sikujua ni kitu gani alichokuwa anamaanisha dada yule.

‘’haya nikija unikaribishe usifunge mlango wako sawa…….’’ Aliniambia kauli tatanishi nikabaki kujiuliza huyu dada ana matatizo gani.

Hata kabla sijahoji zaidi akaondoka na kilichotokea baada ya dakika chache kila nikikumbuka huwa nasisimka na kusema kuwa duniani kuna vimambo vidogovidogo tu ila huko nilipokuwa ndio kuna mambo katika maana halisi ya mambo.

Nikiwa nimesimama pale mara alikuja nje usoni kwangu, ilikuwa mara ya kwanza kukutana na nzi kule lakini sikujali nikatumia mkono wangu kumpunga ili akae mbali nami, yule nzi akaondoka na kurudi tena usoni kwangu, nikampunga tena akaenda akarudi. Alikuwa anaunguruma kwa sauti iliyokuwa inanikwaza sana.

Nilipompunga kwa mara ya tatu alinigeuzia kibao nzi yule sasa akahamia upande wa masikio. Alilazimisha kupenya katika masikio yangu, nikaendelea kumpunga huku sasa hofu ikiongezeka.

Nikipunga sikio hili mara anahamia sikio la huku, nikipunga huku anakuja upende aliotoka awali.

Baadaye akatoweka zake nikajua ndio mwisho wa karaha ile, nikamngoja adell arejee nimuulize alikuwa ana maana gani aliposema kuwa akija nisiache kufungua mlango.

Nikiwa katika kuwaza vile nikamsahau yule nzi.

Hilo likawa kosa, nikashtukia ghafla katika sikio langu yule nzikapenya.

Ebwana eeh akatambaa upesi hadi kweli ngoma ya sikio huku akiendelea kuunguruma, nilikimbia jamani, usiombe kutokea na jambo kama hili. Kuingiliwa na mdudu sikioni. Hata akiwa mdogo hisia zinakuja kuwa ni mkubwa sana… mimi nilikimbia lakini sasa nikamsikia kabisa akipenya shingoni akawa anashuka chini huku akiunguruma. Niligalagala huku napiga mayowe. Nzi anazidi tu kupenya.

Ninasisimka mpaka leo nikikumbuka tukio lile, hakuna aliyekuja kunipa msaada nilikuwa mimi mwenyewe kwa asilimia zote.

Nilitapataba, hatimaye nikamsikia akitawala tumboni nzi yule.

Na baadaye akanza kupanda juu tena. Nilihisi kufa….

Safari hii hakupita sikioni bali alitokea mdomoni, upesi nikaachia mdomo akatoka.

Nikabaki nahema juu juu nisijue hata ni kitu gani hiki kimenitokea.

Nikiwa katika hali ile mara adella akafika, nilianza kumwelezea mkasa ulionikuta.

Adella akatabasamu kisha akaniambia.

‘’wewe nilikueleza kuwa uache mlango wazi ukaziba, nikaona nipitie mlango wa dharula..’’ alisema huku anatabasamu.

‘’adella… una unamaanisha nini wewe…..’’ nilimuuliza.

‘’niliingia kuchukua nywele, nilidhani umenidanganya, dah ulichukua nyingi zitatufaa sana…..’’ aliniambia. Sikutilia maanani kauli ya mwisho, nilitilia maanani kauli kuwa ni yeye alikuwa katika tumbo langu na ni yeye aliyepita sikioni kwangu.

Ilitisha sana kuamini katika tukio lile, lakiniu lilitokea na mimi ndiye mtokewa mwenyewe na hapa nafanya kukusimulia tu.

Usiombe ukakutwa na tukio kama hili.

‘’kesho tunaanza safari ya kuondoka, unatakiwa kuwa jasiri sana martin, tena jasiri sio kidogo yaani…. Kuna mambo magumu ukilemaa tu unakuwa katika mwisho mbaya. Utaishi njia panda ya kuzimu kwa mateso sana hadi kufa kwako…’’ alinieleza adella huku kwa mara ya kwanza kabisa nikiona ametawaliwa na hofu kuu.

‘’najua unawaza kuhusu yule nzi…. Hizo njia tunazitumia mara nyingi sana huku katika ulimwengu wetu.. sema mara nyingi tunaingia mwanadamu akiwa amelala, lazima tu ataacha masikio wazi lakini wale wanaolala midomo wazi tunawapenda zaidi maana ni rahisi sana kupitia mdomoni kuliko sikioni. Huwa tunaingia kwa akina mama kwa ajili ya kuzinyofoa mimba zao na kuzipachika mimba zetu feki, tunaingia kwa akina baba na kuvunja vizazi vyao….. huwa tunaingia katika namna hii martin. Ni njia hatari sana mfano mimi nilipokuwa napita mdomoni, ungesema unitafune tu basi kwisha habari yangu, na wewe pia ungekufa…. Ndo maana huwa tunaingia usiku wakiwa wamelala midomo wazi…..’’

Adella alinisimulia jambo lile kana kwamba ni jambo la kawaida sana katika maisha.

Kwangu mimi lilikuwa jambo linalosisimua na kutetemesha sana.

‘’kwa hiyo huwa mnaingia kwa yeyote mnayemtaka…..’’ nilimuuliza.

‘’mh hapana sio popote kuna watu wanazo kinga kali sana, ukimsogelea umekwisha, kwenye kinga hapa wapo ambao wametibiwa na kuwekewa kinga na mchawi ambaye anao utaalamu kupita sisi, na kuna wale wanaolindwa na Mungu…..’’

‘’hata nyie mnamjua Mungu kwani…’’ nilimuuliza nikiwa nimestaajabu.

‘’ni nani asiyemjua Mungu martin wangu, natambua kuwa haya tunayofanya sio sahihi nataka mimi na wewe twende duniani tukaombe radhi dunia na kisha tumtegemee Mungu…. Sasa hawa wanaolindwa na Mungu wapo katika madaraja tofauti, wale dhaifu kiimani huwa tunaingia bila wasiwasi, wale moto hatugusi hata nyumba yake, wale vuguvugu wasioelewa wapi pa kuegemea yaani wanategemea Mungu pamoja na waganga hawa ndo wepesi kupita wote katika kuwaingia….. maana wanaowategemea kila mmoja anategea kwa sababu hawapi imani wanayotaka….. unamtegemea Mungu na umefungwa hirizi nne….. hauna kitu wewe…’’ aliendelea kusema nami adella.

Na baadaye akaachana na mada hiyo, akanieleza kama nipo tayari kwa safari. Nikamjibu kuwa nipo tayari sana na ninamtegemea yeye kwa asilimia zote.

‘’twende kwa kutegemeana martin, usinitegemee mimi tu maana itafikia hatua hata mimi nitakutegemea wewe…’’ adella alizungumza kwa sauti ya chini iliyokuwa katika kitetemeshi cha wasiwasi….

‘’nitakuja kukushtua tuanze safari….’’ Aliniambia kisha akaondoka huku akiniachia pale chakula ambacho alikitoa katika mizunguko yake alipoagizwa duniani.

Kilikuwa chakula kizuri japokuwa kilikuwa kimepoa sana.



ITAENDELEA


0 comments:

Post a Comment

BLOG