SIMULIZI FUPI: SIMAMA
HALI ya maisha ilikuwa imekataa kuwa nilivyokuwa nahitaji mimi kuwa, nikiwa na umri wa miaka ishirini na saba basi niweze kuwasaidia wazazi wangu ambao umasikini uliwafanya washindwe kunipa elimu bora.
Nilikuwa ninayo miaka ishirini na saba lakini hata uwezo wa kumnunulia mama yangu kanga sikuwanao sembuse kumnunulia baba yangu suti ama baiskeli!!
Jambo hili liliniumiza sana kichwa, kama ni kilimo nilifanya kwa bidii sana lakini kilichopatikana kilikuwa ni chakula tu na wala si utajiri kama nilivyokuwa natarajia.
Nilijikuta nakata tamaa na zile jitihada zangu katika kilimo zikapungua imani yangu kuwa Mungu anatuona masikini nayo ikatoweka!!
Nikakufuru kwa kuamini Mungu ana upendeleo....
Acheni wazazi waitwe wazazi jama!! Unaweza kuficha siri, kujifanya haujakata tamaa lakini wao upesi tu wanajua kuwa mtoto wao amebadilika. Ni wao waliokuzaa na kukulea, vipi wasikujue?
Siku moja baba aliniita chumbani kwake. Alikuwa yu pamoja na mama. Mshumaa ulikuwa unawake katika hali ya uhafifu lakini walau kidogo uliweza kuniwezesha kukiona kigoda na kuketi.
Baba alikaa kitako kisha akanitazama na kunieleza kuwa usiku ule ameniita yeye na mama kuna jambo anahitaji kunieleza. N a hapo akaanza kuzungumza...
“Mwanangu Bryan, macho yetu sisi wazazi wako yameona kitu machoni kwako. Umekata tamaa mwanetu, umekata tamaa ya maisha. Ni haki yako yako mwanetu kuyatazama maisha kwa jicho lako. U mtu mzima sana Bryan, lakini si haki yetu wazazi wako kukutazama ukiyaangalia maisha ambayo sisi tuliyaona kabla yako.
Mwanangu!! Sikiliza maneno yangu na kama mama yako akiwa na la kuongezea atakueleza na baada ya hapo ujifikirie upya.
Bryan! Kabla ya kukata tamaa fikiria juu ya utukufu wa Mungu! Aliyekupa wewe mikono, miguu na macho vyote vikiwa imara.
Mwenyezi Mungu hakukupa hayo macho ili uyatazame maisha kama magumu, bali uzitazame fursa kisha miguu itembee na mikono itende.
Haya yote huwezi kuyafanya pasipo na akili, huyo Mungu ambaye umekata tamaa ya kumtegemea akakupa akili!!
Na ili uone maajabu yake akakuumba wewe mwanaume, maana ungekuwa mwanamke ungeshaolewa na kuondoka nyumbani labda ungekuwa mjini huko na ungekuwa haujui nini maana ya maisha magumu!! Sina maana kwamba wanawake hawajui maana ya ugumu wa maisha ila wao wana afadhali wakiolewa...
Bryan!! Unayo miaka 27 tu na mimi baba yako ninayo miaka zaidi ya sitini, mama yako anayo miaka arobaini na kitu. Lakini tunatabasamu!!!
Wewe unakata tamaa hata kabla haujaoa Bryan!! Ama hauna hata mpango wa kuoa siku moja nawe uitwe baba? uhudumie familia?
Hebu kidogo tusahau kuhusu Mungu lakini kumbuka utake usitake ni yeye anayebaki kuwa mkuu.
Bryan baba yako nilisoma lile darasa la nne la zamani. Kuna mwalimu wangu mmoja aliwahi kunipa usemi mmoja, alisema kuwa 'IKIWA HAUWEZI KUPAA BASI JITAHIDI UKIMBIE NA KAMA KUKIMBIA BADO NI MTIHANI MGUMU JITAHIDI UTEMBEE, UKICHOKA KUTEMBEA BASI HATUA A MWISHO NI KUTAMBAA LAKINI YOTE JUU YA YOTE KAMWE USIJE KUSIMAMA' fanya lolote ambalo litakupeleka mbele na si kukurudisha nyuma ama kukusimamisha hapo ulipo.
Vijana wengi wamesimama na wengi zaidi wanarudi nyuma...
Wewe umewahi kuwaza kupaa, ulivyoshindwa kupaa yaani kuwa na maisha mazuri ya rahisi rahisi ukaamua kukimbia kwa kufanya kilimo. Kilimo kimekushinda umeamua kukaa!! Yaani haujajaribu kutembea wala kutambaa!! Bryan una deni mwanangu!! Deni kubwa sana!!!
Dunia inakuda, mimi na mama yako pia tunakudai.
Hakuna maisha rahisi Bryan mwanangu, kila maisha yanakuja kwa hatua!!!
Kilimo kiliposhindikana, je umejaribu uvuvi, ama haya mabwawa kijijini kuna watu maalumu waliundiwa ili wafanye uvuvi humo??
Je ulijaribu ufugaji? Kuhusu hili utaniuliza mtaji wa kufanya ufugaji utautoa wapi??
Sitakujibu lakini nitakuuliza tu!! Kwani ndama wa ng’ombe na yule wa mbuzi wanauzwa milioni moja??
La! Bei zao ni sawa na ileile uliyotumia kununua jembe lako la kwanza!!
Namaanisha kuwa kila kitu huanzia kuwa kidogo na kisha kuja kuwa kikubwa. Hakuna kitu kinachoanza kikiwa kikubwa tu!!!
Na usipende kutamani vikubwa bila kujua wale waliovikuza walipitia ugumu gani!!
Bryan najua hata mama yako angeweza kusema haya ninayoyasema na hapa ninasema kwa niaba yake. Unamfahamu bwana mmoja anaitwa Bakhresa, yule ambaye hata jana asubuhi tumekula mkate alioutengeneza na juzi ile tulikula maandazi anayotengeneza
Nimetolea mfano huo nikimaanisha kuwa watanzania wengi na wewe ukiwa mmoja wao tuna tabia ya kudharau fursa na baada ya hapo anatokea tajiri anazitumia zile fursa na sisi tunakuwa wateja wake!! kile kidogo tulichonacho anakichukua tena!! Kihalali...
Ungeweza kunitukana mwanangu ningekwambia uanze kukaanga maandazi hapa kijijini, lakini ungenikumbatia ikiwa ningekwambia kuanzia leo kile kiwanda cha kutengeneza maandazi ni cha kwako!!
Maisha hayana muujiza mwanangu, kama ni muujiza basi baba yako nimeisubiri sana na sasa ni mzee na sijapata muujiza wowote. Nilichelewa sana kugundua kuwa katika maisha ni jitihada na sio muujiza lakini nilichelewa sana!!! Isiwe kwako mwanangu, wewe haujachelewa una miaka 27 sasa. Yaliyonitokea baba yako yawe funzo kwako!!!
Vijana wengi wa sasa wameketi vijiweni wakiweza kuhimili kununua pakiti za sigara lakini bado wanalalamika maisha magumu sana na zaidi wanaitukana serikali eti haiwajali hata kidogo!!
Huwa najiuliza hawa vijana walitaka ikulu ijengwe kijiweni ndo watambue kuwa serikali inawajali ama walitaka yule mbunge wao aanze kushindia vijiweni pamoja nao wakipiga soga wiki nzima ndo wajue kuwa wanajaliwa?? Mwanangu simaanishi kuwa eti serikali yetu imekamilika kwa asilimia zote. Lakini sasa ukishajua serikali haikujali basi hebu wewe jijali mwanangu!!!!
Umeteleza mwanangu na umeanguka lakini nakuona kijana unayejitambua sana, mimi na mama yako tunakuomba sana SIMAMA…… SIMAMA mwanetu simama sasa!!! Anza upya, jifunze kutembea. Ukimaliza hilo utaweza kukimbia na hatimaye utapaa kama unavyohitaji!!!
Nakutakia usiku mwema mwanangu! Tambua kuwa mimi na mama yako tunakutegemea sana na tutasikitika sana ukikata tamaa.
Simama mwanangu!!!
***SAMBAZA SIMULIZI hii kwa KU-SHARE ili iwafikie marafiki wengi. Hili ni somo kwetu vijana, tujifunze kupitia maneno ya busara ya baba yake Bryan katika simulizi hii fupi.
SHARE SHARE SHARE....
0 comments:
Post a Comment