Search This Blog

Monday, January 2, 2023

NENDA 2013

 https://pseudepigraphas.blogspot.com/2019/11/nenda-2013.html





SIMULIZI FUPI - NENDA 2013





Mshale wa mrefu wa saa uligota katika namba sita huku ule mfupi ukiwa katikati ya ya kumi na moja na kumi na mbili.



Ilikuwa saa tano na nusu usiku na ilikuwa tarehe thelathini na moja mwezi wa kumi na mbili mwaka 2013.



Ilikuwa imebaki nusu saa tu mwaka mpya wa 2014 uweze kuingia katika utawala.



Joseph Mateso alinyanyuka kutoka katika kitanda chake, akasimama wima kisha akaanguka sakafuni kwa kutumia magoti. Chumba kilikuwa kimya kabisa na kitandani alikuwa amelala mtoto mchanga. Ambaye alikuwa na umri wa miezi mitatu.



Mama yake hakuwepo wakati huo alikuwa ameenda katika mkesha wa mwaka mpya kanisani.



Joseph aliyafumba macho yake kisha akaanza kuzungumza peke yake, lakini kama aaminiye kuwa kuna mtu anamsikiliza.

“SIWEZI kusema nakuchukia ewe 2013. Ila nenda na kamwe usirudi tena na kama utaamua kurudi usirudi kwangu.



Nilikupokea kwa shangwe, nikapiga magoma na filimbi nyingi usiku. Ni uthamani gani zaidi ulitaka nikuonyeshe ewe 2013, licha ya kukupokea vile hata ukiwa hujanizoea ukanishawishi ninywe pombe, wakati mwenzako 2012 nalitambua vyema kuwa ninaichukia pombe kupita vitu vyote, kwani hakukwambia….



Nikalewa nikaingiwa na tamaa za kimwili. Ukamlaghai na Maria akajumuika nami katika ulevi mwishowe tukatamaniana kingono, ulivyokuwa na tabia mbaya kupindukia, ukamlaghai Mangi akalifunga duka mapema nikashindwa kupata kondomu.



Nikafanya ngono zembe ukafurahi ewe 2013!!



Ni kweli nilikuwa mjinga sana kufanya tendo lile, lakini hivi hukuridhika, mbona akina Japhet nao walikupokea kwa shangwe lakini majanga yote ukanisukumia mimi, nilikukosea nini 2013?



Baada ya siku tatu Maria akanijia akidai kuwa ana ujauzito.



Ukacheka meno yote nje 2013 kuwa Jose mimi naumbuka. Na kweli niliumbuka maana wewe ni mnafiki hukutaka kuificha hii siri ukamnong’oneza Vicky mchumba wangu ambaye alikuwa akiniweka mjini. Vicky akaachana na mimi kimahusiano…..



Na wakati huohuo hukutaka nijipange upya, ukamtapisha Maria mbele ya baba yake, kesho yake mzee yule mwenye imani kali ya kidini na mkoloni wa zamani akampeleka Maria hospitali na kufichuka kuwa ni mjamzito.



2013 usiye na huruma ukamtuma mzee wake kumfukuza nyumbani eti aje kuishi na mwanaume aliyempa mimba.



Mimi kwa kazi gani ningeweza kuishi na mwanamke sasa, kazi ya kulipwa shilingi elfu hamsini ningeweza kweli kulilea tumbo lile 2013? Eeh!! Mbona hukunionea huruma, au nilifanya makosa kukupokea 2013?



Haya Maria amekuja kuishi na mimi akiwa na mimba yake, baada ya miezi mitatu nikadhani 2013 umepata na wengine wa kuwatembelea. Kumbe bado umening’ang’ania





Yule mwajiri wangu sijui nini kilimsibu maskini wee!! Akajipiga risasi na kufa palepale. Sikulia sana kwa sababu alikufa la! Nililia kwa sababu ulikuwa mwanzo wa kuikosa ajira hiyo ndogo.



2013, kwani 2007 hakukueleza bayana kuwa alinipa janga la kukosa ada na kushindwa kuendelea na masomo, au we ni mnafiki na huwa huzungumzi na wenzako. Ungeenda basi umuulize kwanza labda ungepata huruma kidogo.



Mimi sina vyeti ningeishi vipi.



He! Una roho gani wewe 2013, mimi nikajua basi umeninyima ajira utaondoka zako ukawatembelee watu wengine, lakini bado ukanifitini kwa mama mwenye nyumba.



Akanipa notisi eti Maria anatapika tapika hovyo anaweza kusababisha kipindupindu dah! Na kisha akaongezea kuwa nyumba yake huwa hapangishi watu wenye familia.



Najua ni wewe 2013 ulimkumbusha tu juu ya hili!!



Nikatimuliwa Jose mimi, 2013 ukinicheka kicheko cha dharau. Na ulivyo mbaya hata kumpunguzia hasira baba yake Maria ili amsamehe mwanaye hukuwaza.



2013 wewe ni wa kunifanyia hivyo kweli, yaani ukanisababisha hata nauli ya kwenda kumuuguza mama yangu nikakosa. Hakuna aliyekuwa tayari kunikopesha…ni kosa gani kubwa niliwahi kuwafanyia ndugu zako hadi ulipize kisasi hiki, nani kati ya wadogo zako, 2011, 2010, 2009, 2008.,…. Nani mimi nilimkosea hadi ukanitenda hivi.



Mbona niliishi nao vizuri tu.



2013 ukaamua kunitoa machozi, ukamwondoa mama yangu duniani halafu ulivyokuwa katili na mnafiki eti akapatikana mtu wa kunipa nauli ya kwenda kumzika mama.” Jose akasita akajifuta machozi kisha akaendelea.



“Nasema toka 2013 tena usirudi kwangu kamwe, ondoka karibu nami labda huyu kaka yako aliyeingia anaweza kuwa na huruma. Sio wewe ambaye ulinidhalilisha kiasi kile, nikaitwa mwizi, chokoraa, ombaomba yote haya majina ulisababisha wewe. Ndio ulisababisha wewe sio kwamba nakulaumu, hivi unadhani nisingekuja kukupokea wewe ningekuwa hapa…mgeni gani wewe usiyekuwa na shukurani….mgeni gani wewe wa kunitia uchungu tu. Nikabadili njia nikawa sipiti kwa Masawe tena, nilikuwa nimekopa sa, Muha naye alikuwa hanielewi na hakuwa tayari kunikopesha.



Sema kuna kitu kimoja ulinifurahisha katika unafiki wako, ulikuwa unanikomoa ukiona nimezidiwa kabisa unalegeza, mshenzi sana wewe 2013. Maria hakuwa akiugua hovyo, asante kwa huruma hiyo maana dah! Sijui tu ingekuwaje angekuwa anaugua hovyo.



Ila kwa upande mwingine pia nakushukuru maana uliifanya akili yangu ikatanuka ukanifanya nikaitwa mwanaume, maana kazi ngumu zote nilifanyaq bila kuchagua. Nikawapata marafiki wa kaliba yangu, nikajifunza nini maana halisi ya maisha bila elimu ya darasani.



Na hatimaye mwezi wa tisa nikawa baba rasmi.



Ukanipumzisha kidogo 2013. Nadhani ulimwonea huruma yule malaika aliyezaliwa.



Ukanipa tabasamu kidogo, baba yangu mdogo akanipa kazi yenye kipato kizuri kiasi. Naam! Maria akapata ahueni kumuona mume wake akienda kazini na kurudi jioni na chochote kitu.mwanangu nikamuita Masumbuko ili akikua aniulize juu ya jina lake nami nimsimulie juu yako 2013.



Na kama unadhani nitamficha kitu, ng’o umechemsha. Nitamweleza kila kitu juu yako ili siku ukirudi tena hata kama mimi nimekufa yeye na vizazi vijavyo wasikupokee we bwana mwenye roho mbaya.



Nimepiga goti leo ewe 2013, nakuhakikishia kuwa huyo wa kuitwa 2014 siendi kumpokea atanikuta hapahapa kitandani….akinuna anune tu mi sitajali maana nyie hamueleweki asije kuwa na tabia kama zako akaniulia mke wangu Maria. Na kunitesea mwanangu.



Nipo hapa nasubiri uondoke, nakufokea leo kwa sababu najua huna mamlaka tena ya kunisumbua….ondoka zako ushanitia aibu sana wewe…



Ushanitesa sana wewe!!



Ondoka aingie kaka yako



Kama wengine uliwatendea vyema wakusindikize haohao….mimi sijisikii kukusindikiza hata kwa kinafiki… ondoka peke yako halafu…” akataka kuendelea kuzungumza mara akasikia mabaruti yakilipuka huku na kule na mawe yakirushwa katika mabati.



Na hapo kitoto kitandani kikaamka na kuanza kulia.



“Huyu naye kaingia kwa fujo eeh!! Mwenyezi Mungu saidia 2014 asiwe kama mdogo wake. Sio kwangu tu hata kwa rafiki na ndugu zangu…….” Jose alijisemea kwa sauti huku akimnyanyua mtoto mnchanga na kuanza kumbembeleza.



Maria alikuwa ameenda katika mkesha kanisani!!





MUNGU AWABARIKI MARAFIKI ZANGU!!!





MWISHO!!

0 comments:

Post a Comment

BLOG