Search This Blog

Sunday, January 1, 2023

GEGO LA MATANUZI

 






SIMULIZI FUPI : GEGO LA MATANUZI



KUNA waliokata tamaa, kuna waoga na kuna majasiri walioamua kupigana hadi mwisho. Lakini kwa nini ukate tamaa? Unaaswa: Pigana Kufa na Kupona! Labda utashinda, labda utashindwa, lakini pigana! Kupigana ni jambo moja. Matokeo ya kupigana ni jambo jingine. Hadithi hii ilipata tuzo katika shindano maalumu lililoandaliwa na Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (UWAVITA) kwa ushirikiano na shirika lisilo la kiserikali la Peacefriend la Korea Kusini. Shindano hilo lilifanyika kwa minajili ya kuanzishwa jarida maridhawa la Kiswahili; Rafiki wa Fasihi. Ni hadithi fupi, yenye mafunzo ambayo ni vyema ukamsimulie yule ambaye hakubahatika kuisoma. Ni hadithi inayogusa kila familia katika vita vinavyoutikisa ulimwengu katika karne hii ya ishirini na moja. Fuatana na mtunzi wako katika mtiririko huu ili ujue kilichojiri



**********



KWA kawaida, Jumapili hii ingetarajiwa kuwa siku njema na ya furaha, siku ambayo ingetawaliwa na shmrashamra za ngoma, nyimbo na mambo mengine yafurahishayo. Aidha, shamrashamra hizo zingeambatana na vyakula kochokocho. Hivyo ndivyo ilivyokuwa ikitokea pale Siamini na mumewe, Matanuzi walipotembelea kijijini hapo.



Mara zote walikuja na zawadi kemkem zikiwemo nguo, vitabu na kadhalika. Na kila walipofika, Mzee Nshinze, baba yake Siamini alichinja mbuzi au ng'ombe ambaye aliliwa na pilau, huo ukiwa ndiyo ukaribisho rasmi wa mwanawe, Siamini na mumewe, Matanuzi.



Majirani pia walinufaika kwa mlo huo na ukarimu wa Matanuzi ambaye aliwanunulia soda na togwa, hali iliyowafanya watu wachangamke na kuanza kuimba nyimbo zao za asili na hatimaye kucheza ngoma.



Lakini Jumapili hii hali ilikuwa tofauti kabisa. Kwanza , dada Siamini na mumewe hawakuleta zawadi yoyote. Pili, nyuso zao zilionyesha kugubikwa na majonzi mazito. Zaidi ya yote, walionekana kutokuwa na nia ya kuzungumza na mtu yeyote isipokuwa baba na mama.



Ilikuwa ni wiki moja kabla ya sikukuu kubwa duniani, sikukuu ya Krismasi. Ni kipindi ambacho watu wengi walirejea makwao kwa ajili ya kusherehekea sikukuu hiyo. Matanuzi na mkewe pia walikuwa na utaratibu huo siku za nyuma, na kila walipofika nyumba ilichangamka. Ni wakati ule siyo Jumapili hii ambayo haikuwa ya kawaida.



Mara tu walipofika, baada ya salamu za harakaharaka walielekea sebuleni ambako waliomba watu wote waondoke, isipokuwa Mzee Nshinze na mkewe, Mama Siamini.



Waliokuwa nje hawakuambulia chochote kuhusu maongezi yaliyokuwa yakiendelea huko sebuleni zaidi ya kusikika minong'ono na miguno. Na ghafla, muda mfupi baadaye kilio kikali kikasikika. Kilikuwa ni kilio cha mama yake Siamini.



“Maskini mwanangu!” aliomboleza. “Nimemkosea nini Mungu mie?...Jamaniii…mwanangu...! Hapana! Nitakufa na mwanangu...!”

Kilio hicho kilipokewa na mwanaye, Siamini. Yeye alilia kwa kwikwi, japo kwa sauti ndogo. Hata hivyo, sauti za Mzee Nshinze na Matanuzi zilisikika zikiwasihi waache kulia. Baada ya muda walinyamaza kama walivyoanza.



“Kuna nini?” kila mmoja aliyekuwa nje alijiuliza.



Hakuna aliyekuwa na jibu.



Baada ya maongezi yaliyochukua takriban saa mbili walitoka nje. Uso wa Mama Siamini ulikuwa bado umelowa machozi. Hakuweza kumtazama yeyote machoni. Vivyohivyo, Siamini naye hakuwa katika hali ya kawaida. Yeye alijiinamia, akiepuka kutazamana ana kwa ana na mtu yeyote. Mzee Nshinze, yeye alijaribu kutabasamu, lakini tabasamu lake lilionekana wazi ni la kulazimisha.

Kwa upande wa Matanuzi, yeye alionekana kusitasita. Alikuwa kama mtu anayetaka kusema jambo fulani lakini sauti ikakataa kutoka. Akamfuata mziwanda wa Mzee Nshinze, mtoto wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 15. Aliitwa Festo.

Akaingiza mkono mfukoni na kutoa noti ya shilingi 5,000 na kumpatia. Kisha, kwa sauti ambayo haikuonekana kama yake, akasema, “Shemeji yangu, Festo nalazimika kurudi mjini mara moja. Tutaonana Jumapili ijayo.”

Baada ya maneno huyo aliwaaga watu wengine waliokuwa pale nje. Akaingia kwenye gari lake na kuondoka. Akarudi mjini.

Mara tu gari lilipotokomea, ndiyo kwanza Festo akakumbuka kuwa dada yake, Siamini alibaki. Akamkimbilia na kumuuliza, “Dada, mbona shemeji kakuacha?”

Swali lake lilisababisha Siamini atokwe machozi kwa mara nyingine.



**********

'SIRI' ya kikao kile cha siri, baina ya Mzee Nshinze, mkewe, Siamini na Matanuzi iligundulika siku kadhaa baadaye. Ni upekupeku wa mtoto Festo uliokuwa chanzo cha siri hiyo kuwa hadharani. Ilikuwa ni baada ya Jumapili ya pili kupita bila ya Matanuzi kuonekana hapo kijijini kama alivyoahidi. Siku zote hizo Siamini alikuwa hana raha. Hata kula, alikula kwa taabu sana, jambo lililoufanya mwili wake mnene uanze kudhoofu. Mama yake pia alikuwa mkimya kupita kiasi huku Mzee Nshinze akiwafariji mara kwa mara.

Festo aliyagundua mabadiliko hayo. Ikatokea siku akamshupalia mama yake. “Mama, kwani kuna nini?” alimuuliza.

“Kuna nini wapi?” mama yake naye alimhoji.

“Hapa. Hapa nyumbani.”

“Kwani wewe unaona kuna nini?”

“Hatuko katika hali ya kawaida,” Festo alijibu. “Tumepatwa na nini? Tangu dada arudi hali imebadilika sana. Kwani amepewa talaka?”

Mama yake alimtazama kwa mshangao. “Talaka! Yametoka wapi hayo ya talaka?” alihoji huku kwa mara ya kwanza kwa wiki mbili hizo, sasa tabasamu la mbali lilichanua usoni pake.

Hata hivyo halikuwa tabasamu lililochukua hata sekunde kumi. Lilikatika ghafla. Akaukunja tena uso wake na kusema kwa huzuni, “Ni kheri hata ya hiyo talaka, mwanangu. Yaliyotukuta hayasemeki.”

“Yapi hayo?!” Festo alimbana.

Mama yake alimtazama kwa makini zaidi. Kisha akamwambia, “Festo, wewe ni mtoto mdogo. Bado ni mdogo sana, mwanangu. Huwezi kuelewa.”

“Hapana,” Festo alimpinga mama yake. “Mimi siyo mtoto mdogo, mama. Nina umri wa miaka kumi na mitano sasa. Niko darasa la saba. Nina udogo gani mimi? Tafadhali n'ambie mama.”

Mama alinyamaza kwa muda, kana kwamba anatafakari uzito wa yale aliyokusudia kumwambia. Hatimaye akasema, “Sikia, mwanangu. Haya nitakayokwambia ni siri kubwa. Usimwambie mtu mwingine yeyote.”

“Sawa, mama.”

Kimya kifupi kilitawala, kisha mama yake akasema kwa upole na masikitiko, “Dada yako anaumwa.”

Festo alimsikia lakini hakumwelewa. “Umesema dada Siamini anaumwa?” hatimaye alimuuliza kama vile asiyeyaamini masikio yake.

“Ndiyo, anaumwa,” mama yake alisisitiza.

Akilini mwa Festo, mtu yeyote anayesumbuliwa na maradhi yoyote lazima afya yake idhoofu. Na hilo huwa bayana machoni mwa watakaomwona. Lakini Siamini hakuwa hivyo. Alionekana yu bukheri wa afya. Alikuwa na mwili mnene, wenye ngozi laini, iliyomeremeta.

Ni hilo lililomshangaza Festo. Akambana zaidi mama yake. “Mbona Siamini ana afya njema tu, mama?”

“Dada yako anaumwa!” mama yake alirudia kwa msisitizo, safari hii akimtazama Festo kwa macho makali. Kisha akaongeza, “Anaumwa haya maradhi ya kisasa! Isitoshe ni mjamzito!”

“Nini?” Bado Festo alikuwa kizani. “Mama mbona una mafumbo? Kwa kweli sijakuelewa!”

Mama yake alimtazama kwa muda kabla hajashusha pumzi ndefu na kusema, “Anaumwa UKIMWI!”

Nusura Festo aanguke chini kwa mshtuko. “Dada! Hapana, haiwezekani! Dada ana UKIMWI? Ameupata wapi?” aliropoka.

Haikumwingia akilini Festo kuwa dada yake, Siamini Nshinze angeweza kupatwa na masaibu hayo. Hakuamini.



**********



AKIWA ni mtoto wa mwisho katika familia hii, Festo alikuwa ameshuhudia jinsi ndugu zake wote walivyolelewa kwa nidhamu huku wakifuata maadili mema. Walizaliwa katika kijiji hiki cha Simbo, ambacho kiko kilometa chache kutoka mjini Kigoma, na walizijali sana mila zao, wakayafuata mafundisho na kanuni dini yao na wakawaheshimu wazazi wao.



Akiwa ni mtoto pekee wa kiume, kamwe hakuwahi kumsikia dada yake yeyote akizungumzia suala la kwenda kwenye starehe. Hakuna aliyekuwa akizungumzia suala la disko, dansi, kunywa pombe au kuwa na rafiki wa kiume.



Dada yake mkubwa, Naila, aliolewa miaka mitano iliyopita huko jijini Dar es Salaam ambako anaishi vizuri na mumewe. Aliyefuata, Sikujua, alikuwa masomoni nchini Uingereza akichukua shahada ya Sheria.



Huyu Siamini, yeye aliolewa mwaka jana tu, baada ya kumaliza kidato cha nne. Mume wake, Matanuzi alihitimu elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka kadhaa iliyopita, na sasa alikuwa ni mkurugenzi wa shirika fulani la kimataifa lililokuwa na ofisi zake mjini Kigoma.

Kwa jinsi walivyoishi kwa amani, furaha na upendo, haikumwingia akilini Festo kuwa mmoja wao angeweza kupata UKIMWI. Pamoja na elimu yake ndogo ya msingi, suala la UKIMWI halikuwa jambo geni masikioni mwake.



Kampeni mbalimbali zilizokuwa zikiendelea nchini kote dhidi ya UKIMWI shuleni, mitaani na katika vyombo mbalimbali vya habari zilimfanya auelewe fika mkasa huu ulioikumba dunia.

Alielewa kuwa UKIMWI ni kifupi cha 'Upungufu wa Kinga Mwilini' ugonjwa unaotokana na virusi ambavyo huitwa VVU. Kirefu cha VVU ni Virusi Vya Ukimwi. Virusi hivyo vinapoambukizwa kwa binadamu, hushambulia chembechembe ambazo hupambana na maradhi. Baada ya kuzidhoofisha chembechembe hizo ndipo mhusika huingia katika hatua ya kuugua UKIMWI. Sasa mwili wake huwa dhaifu na kutoweza kupambana na magonjwa nyemelezi.



Kwa ujumla, elimu ya msingi kuhusu UKIMWI haikuwa ngeni sana kwa Festo na kwa watu wengine kijijini hapo. Hata hivyo, katika familia ya kina Festo, na pengine hata kwa watu wengine kijijini hapo waliichukulia elimu hiyo kama jambo lisilowahusu. Waliuchukulia ugonjwa wa UKIMWI kama tatizo la watu wengine hususan watu wa mjini.



Kwa nini? Kwa sababu waliamini kuwa kati yao hakuna aliyetumia sindano za mitaani, hakuwepo mama mwenye UKIMWI anayenyonyesha, na wala ufuska wa kujamiiana ovyo halikuwa jambo la kawaida kijijini hapo.



Ni majuzi tu hali halisi ya UKIMWI ilipoanza kujitokeza hapo Simbo. Ni pale Sheila, mtoto wa Mzee Sukununu aliporudi kutoka mjini huku akiwa amekonda sana. Pia alikuwa akikohoa mara kwa mara na kuharisha, huku mwili wake ukiwa umejaa vipele.



Msichana huyu aliugua kwa muda mrefu, mara homa, mara majipu, mara Kifua Kikuu na kadhalika. Sheila alifikia hatua ya kujisaidia palepale kitandani! Hata kula, alikula kwa taabu. Kila aliyekwenda kumwona na kumshuhudia jinsi alivyobadilika, alijua na kuamini kuwa asingepona. Uvumi ukaenea kuwa Sheila ana UKIMWI.



Hata hivyo, wazazi wake walikanusha vikali uvumi huo. Wakadai kuwa Sheila kalogwa na watu waliomwonea wivu kwa ajira yake nzuri huko mjini. Ajira gani? Hakuna aliyejua. Baadaye ilibainika kuwa huko mjini hakuwa na kazi yoyote ya maana zaidi ya ufuska. Ikafahamika pia kuwa hata madaktari walithibitisha kuwa alikuwa mwathirika wa VVU.



Sheila alifariki baada ya mwaka mmoja wa kuugua kwa mateso makubwa. Kila mtu aliamini kuwa alikufa kwa UKIMWI. Kila mtu, isipokuwa wazazi wake ambao hadi sasa wanasisitiza kuwa alilogwa.



Huyo ni Sheila, Sheila binti Sukununu. Leo hadithi hiyo mbaya, ya kusikitisha, imepiga hodi nyumbani kwa Mzee Nshinze! Tena mhusika mkuu akiwa ni bintiye, Siamini Nshinze! Siamini kaupataje UKIMWI? Ameupata wapi? Festo alijiuliza swali baada ya swali. Majibu hayakupatikana.



Akamgeukia mama yake na kumuuliza kwa sauti iliyotoka kwa shida, “Mama...una hakika na unachokisema? Dada yangu ni mnene na ana afya nzuri. Alikua vizuri, amelelewa vizuri na kuolewa kwa heshima zote. Hawezi kupata UKIMWI! Haiwezekani!”



Wakati Festo akiyasema hayo, hakujua kuwa alikuwa akilia hadi pale mama yake alipomkumbatia na kumfuta yale machozi yaliyotiririka mashavuni.



“Usilie, Festo,” mama alimbembeleza. “Wakati wa kulia ulishapita. Huu ni wakati wa kufanya kila jitihada za kuokoa maisha ya dada yako na mtoto wake.”



Ndipo ikafuata hadithi kamili.



Ni kweli kabisa kuwa Siamini alilelewa na kukua vizuri, akifuata maadili yote mema. Aliolewa kwa heshima zote. Alikuwa mwaminifu sana kwa mumewe. Pia, aliamini kuwa mume wake alikuwa mwaminifu kwake. Waliishi kwa upendo, amani na furaha siku zote za ndoa yao.



Ni majuzi tu ilipobainika kuwa Siamini alikuwa mjamzito. Alipokwenda kliniki walimpima na kuthibitisha kuwa alikuwa na mimba ya miezi miwili. Kisha walichukua damu yake na kuifanyia vipimo mbalimbali kwa faida yake na ya mtoto wake. Afya yake ilikuwa nzuri, lakini damu yake iligundulika kuwa ina virusi vinavyosababisha UKIMWI. Ni majibu hayo yaliyomfanya atahayari sana. Alitahayari zaidi pale alipomweleza mumewe taarifa hiyo na akakuta hawaelewani.



Kwa mujibu wa maelezo ya mama, Siamini alimtaka mumewe, Matanuzi pia akapimwe damu yake ili kuthibitisha iwapo tatizo hilo lilikuwa lao wote au la. Matanuzi alikataa kupima. Badala yake alianza kumshuku Siamini kwa kutokuwa mwaminifu katika ndoa. Ni ugomvi huo uliowafanya Jumapili ile waje nyumbani kwao Siamini kusuluhishwa.



Siamini alisisitiza madai yake ya kutaka Matanuzi naye apimwe. Hata Mzee Nshinze na mkewe walimshauri hivyo, lakini alikataa katakata. Kilichofuata ni Siamini naye kukataa kurudi mjini. Akabaki nyumbani kwao hadi atakapopata ukweli juu ya afya ya mume wake.



“Kosa la dada yako,” mama aliendelea, “ni pale alipokubali kufunga ndoa na Matanuzi kabla ya wote hawajapimwa damu zao. Siku hizi dunia imebadilika, mwanangu. Binadamu hatuaminiani tena kwa sura au kauli isipokuwa kwa uthibitisho wa daktari.”



Festo aliyatafakari maneno hayo kwa muda mrefu. Aliona yalijaa ukweli. Siku zote madaktari na wataalamu wengine huasa; HUWEZI KUMTAMBUA MWATHIRIKA WA UKIMWI KWA KUMTAZAMA USONI. Siamini alikosea kumwamini Matanuzi kwa kuwa tu alionekana mwenye afya njema, ana elimu kubwa, ana gari zuri, kazi nzuri na anakaa mjini!



Hata hivyo, baada ya kutafakari sana, aliona kuwa ni makosa kumshutumu Siamini peke yake. Baba na mama walikuwa wapi? Wanafamilia wengine walikuwa wapi? Wote walikuwa na wajibu wa kusisitiza haja ya wachumba wale kupimwa damu kabla ya ndoa. Tatizo la UKIMWI katika familia siyo la mwathirika pekee bali familia nzima.



Kwa unyonge alimuuliza mama yake, “Kwa hiyo mama tutafanya nini?”



“Hatuna la kufanya kwa sasa,” mama yake alijibu. “Mara nyingine vipimo vinaweza kukosea. Hivyo, wiki ijayo tutarudi hospitali na kumwomba daktari ampime tena. Majibu yakiwa yaleyale, tutaanza jitihada za kuwaona wataalamu wa ushauri.”





Siku iliyokusudiwa ilipowadia, Siamini na mama yake walijiandaa kwenda mjini. Walikwenda katika Hospitali ya Mkoa, Maweni ambako walimwona daktari mhusika. Siamini alipimwa tena. Majibu yalipotoka hayakuwa tofauti na yale yaliyotangulia; HIV Positive, kwamba, virusi vya UKIMWI vilionekana katika damu yake.



Lakini siku hiyo, tofauti na siku ya kwanza alipotaarifiwa juu ya hali hiyo, Siamini hakuonekana kusononeka na kujawa na hofu. Wala hakulia. Badala yake alitabasamu kidogo kisha akasema, “Yamenikuta. Sasa ni lazima nipambane nayo.”



Mara akamtazama daktari na kumuuliza, “Nitapata wapi ushauri nasaha?”



Daktari alivutiwa na ujasiri wa Siamini. Akasema, “Dada, umenitia moyo sana. Virusi vya UKIMWI si ugonjwa. Wala UKIMWI wenyewe si ugonjwa. Kinachomfanya mtu aathirike si virusi ila magonjwa mengine yanayoweza kumpata asipofuata ushauri wa kitaalamu. Hivyo, mtu akiondoa hofu, awe mwelekevu, akafuata maelekezo ya wataalamu, ana uwezo wa kuishi vizuri na afya yake tele, kwa muda mrefu kuliko hata wale ambao hawajaathirika. Hata wewe ambaye ni mjamzito, usihofu. UKIMWI si kifo, ni mtikisiko tu wa maisha.”



Nasaha hizo fupi zilimchangamsha zaidi Siamini. Hata hivyo, kwa mzaha kidogo naye akasema, “Najua unajaribu kunifariji...najua nitakufa...”



“Sisi wote tutakufa,” daktari alimkata kauli. “Kifo kipo kwa mtu yeyote. Ukishazaliwa, kaa ukijua kuwa lazima utakufa.”



“Ni kweli,” Siamini alisema. “Lakini siyo kifo cha aibu na mateso kama kifo cha UKIMWI.”



“Hilo ndilo kosa ambalo jamii inalifanya,”daktari alisema kwa msisitizo. “Neno aibu linatoka wapi? Aibu aione kibaka anayekufa kwa kuchomwa moto! Aibu aione mtu anayejimaliza kwa kutumia dawa za kulevya! Siyo maradhi ambayo hakujitakia. Aibu aione anayepigwa na kuuawa baada ya kufumaniwa ugoni.”



“Labda nilijitakia,” Siamini alidakia kwa unyonge. “Kwa nini sikuhakikisha mimi na yule mwanamume ninayemwita ‘mume wangu’ tunapimwa afya zetu kabla ya ndoa?”



Daktari alikohoa kabla hajamjibu, “Tunaweza kusema kuwa hiyo ni ajali, lakini siyo ajali ya kujitakia. Kamwe hali hiyo haihalalishi mtu ajionee aibu mbele ya watu. Kwa hili, madhara ya aibu hayatofautiani na yale ya hofu. Na ndiyo maana ninasema, na ninasisitiza kuwa UKIMWI ni mtikisiko wa maisha. Usichukulie kuwa na UKIMWI ndiyo tayari umekata tiketi ya kifo. La msingi ni kujiandaa kupambana na athari zinazoweza kujitokeza.





“Na hili linajibu hoja yako ya pili ya mateso. Watu wengi wanafikia hatua hiyo ya mateso kwa ajili ya aibu au hofu tu ya kutafuta ushauri. Nadhani ulitaka nikuelekeze wapi utapata ushauri huo kwa uhakika zaidi.”



“Ndiyo, daktari.”



“Sawa, twendeni.”



Wakatoka.

**********



KITENGO cha nasaha kilikuwa na wataalamu wawili. Mzee Nshinze na familia yake walikaribishwa vitini na kupewa vijarida, makabrasha na vitabu mbalimbali vilivyohusu UKIMWI na maambukizi yake, kinga dhidi ya UKIMWI na lishe bora kwa mwathirika. Kisha yakafuata maelezo marefu kutoka kwa mtaalamu huyo, maelezo yaliyomtia faraja na matumaini Siamini. Kitu muhimu zaidi alichosisitizwa ni kuzingatia lishe bora.



“Mwili wa binadamu huhitaji mafuta na sukari,” mtaalamu wa ushauri alisema. “Mafuta ya wanyama kama vile samli na siagi; mafuta ya mimea kama vile ufuta, mawese, karanga, alizeti na mengineyo yanafaa sana. Hali kadhalika, sukari pamoja na vyakula kama asali na miwa vinahitajika. Hata hivyo, vitu hivyo vinapaswa kutumiwa kwa kiasi. Vyakula vyenye vitamini A kwa wingi kama maini, mayai, maembe, mapapai, mboga za majani, karoti, viazi vitamu vya njano, mboga na mawese pia ni muhimu sana.”



“Maji pia ni sehemu muhimu ya mwili na ni muhimu kwa uhai,” aliendelea. “Ni muhimu kunywa maji ya kutosha angalau glasi nane kwa siku. Unywe maji yaliyochemshwa, hata vinywaji vingine vilivyothibitishwa ubora wake na wataalamu. Vinywaji hivyo viwe katika hali ya usafi. Pia, ni vyema kutumia viungo kama vile mdalasini, tangawizi, vitunguu saumu au mimea mingine inayotumika badala ya chai. Maji ya madafu na maji ya matunda pia yanafaa sana.



“Yote haya tunayozungumza hayatakuwa na maana iwapo usafi hautazingatiwa,” mtaalamu aliendelea. “Ni lazima kunawa mikono kwa sabuni au majivu kabla au baada ya kutayarisha chakula. Kila mtu katika familia anawe mikono kwa sabuni au majivu baada ya kwenda msalani na kabla ya kula. Kila mara vitumike vyombo safi wakati wa kutayarisha chakula na wakati wa kula. Pia, sehemu ya kupikia iwe safi.”



Wakati mtaalamu akitoa maelezo, alikuwa akimwonyesha Siamini ni wapi yalipo maelekezo hayo katika vijitabu alivyowapa.



“Kuna faida kubwa kwa mwathirika kutumia lishe bora,” mtaalamu aliendelea. “Chakula bora huupa mwili kinga ya magonjwa. Huupa mwili virutubisho vyote muhimu kwa afya bora,. Huongeza nguvu na uwezo wa kufanya kazi na pia huburudisha.”



Siamini na wazazi wake waliondoka hapo baada ya nusu saa, wakiwa wameshiba ushauri mzito. Wakapata faraja ambayo hawakuitarajia hapo kabla.



**********

“VIRUTUBISHO ni muhimu sana katika mwili wa binadamu na hasa mwathirika,” siku moja Siamini alimwambia mdogo wake, Festo. Ilikuwa yapata wiki moja hivi tangu walipotoka hospitali.



Awali, Siamini alikuwa mtulivu sana. Muda mwingi aliutumia kwa kusoma zile nyaraka za lishe bora. Alisoma kwa makini sana. Na somo lililofundisha namna ya kutengeneza virutubisho lilimvutia zaidi. Jioni hiyo alichukua kalamu nzito na kuanza kunukuu maelezo fulani kisha akayabandika ukutani, kando ya mlango wa jikoni.



Festo aliyasogelea maandishi hayo na kuanza kuyasoma. Siamini alitulia akimtazama. Akafurahi kumwona mdogo wake huyo kazama katika somo hilo.

Dakika kama tano hivi baadaye, Festo alishusha pumzi ndefu na kumgeukia tena dada yake.



“Vipi, umemaliza?” Siamini alimuuliza.



“Ndiyo.”



“Kwa ufupi,” Siamini aliendelea kumhubiria. “Tunachofundishwa hapa ni kutumia vitunguu saumu, kutumia mbegu zilizooteshwa (kimea) na kujifunza kupika mboga kwa mvuke. Pia tunaelekezwa kutumia viungo mbalimbali kama vile hiliki, tangawizi, mdalasini, karafuu, bizari na kadhalika. Lakini ni pale tu viungo hivi vinapokuwa havituumizi. Hilo ni la kwanza.



“La pili, vyakula vinavyochachushwa, kwa mfano togwa au maziwa ya mgando pia ni muhimu kutumia. Ikiwezekana, badala ya chai au kahawa tunashauriwa kutumia vinywaji vinavyotengenezwa kutokana na viungo mbalimbali kama mchaichai au maji ya matunda.”



Festo aliguna. Akacheka kidogo. Kisha akamtania dada yake, akisema, “Dada, sasa unafaa kufungua shule ya elimu ya lishe.”



“Kwa nini?”



“Naona umekomaa sana katika suala hilo.”



“Napaswa nikomae mdogo wangu,” Siamini alisema, uso kaukunja kidogo. Akaongeza, “Yameshanikuta ya kunikuta. Nifanyeje?”



Festo alimwelewa, akaukata utani wake, usoni akionekana kukumbwa na simanzi.



Kwa jumla Siamini alilivalia njuga suala la lishe bora katika kupambana na virusi vya UKIMWI. Wazazi wake nao hawakumwacha. Wao pia waliyasoma kwa makini machapisho aliyokuwa nayo na kumkosoa au kumwelekeza pale alipokosea.



**********

MIAKA miwili ilipita tangu Siamini alipopimwa na kugundulika kuwa ana virusi vya UKIMWI na kupewa ushauri nasaha. Tayari alikuwa amejifungua salama mtoto wa kiume. Mtoto huyo alikua vizuri, akiwa na afya tele. Mara tatu Siamini alimpeleka hospitali kupimwa damu, na mara zote hizo aliambiwa kuwa mwanaye huyo hakuwa ameathirika.



Siamini mwenyewe, bila ya kuambiwa, usingeamini kuwa ameambukizwa VVU. Aliendelea kuwa na afya yake ileile, ngozi yake ileile, laini inayomeremeta, hali iliyotokana na kufuata maelekezo ya wataalamu; kujiepusha na maambukizi ya maradhi mengine na kuzingatia kula vizuri.



Kivumbi kilikuwa kwa mumewe, Matanuzi. Tangu siku ile aliyomleta Siamini hapo nyumbani na mwenyewe kurudi mjini, hakuonekana tena. Hata salamu hakutuma! Na kwa vile Siamini naye aligoma kwenda kwake, hakuna aliyekuwa na taarifa zake sahihi. Ni fununu tu zilizofika kijijini Simbo, kwamba Matanuzi alikuwa na tabia iliyoonyesha kuwa kachanganyikiwa. Eti alikuwa ameanza kuwa mlevi, tabia ambayo hakuwa nayo.



Baadaye zikapatikana taarifa nyingine, kuwa ameomba uhamisho kwenda mkoani Mbeya ambako ilisadikiwa hakuwa na rafiki wala ndugu.



Kwa kiasi fulani taarifa hizo ziliisononesha sana familia nzima ya Mzee Nshinze. Hata hivyo, kwa watu waliomfahamu Matanuzi kwa muda mrefu, walilichukulia jambo hilo kama kutapatapa kutokana na hofu baada ya mkewe kupimwa na kukutwa na virusi. Zaidi, watu wenye akili timamu na walioijua elimu ya UKIMWI, walimshangaa. Hawakutarajia kuwa mtu mwenye elimu ya juu kama Matanuzi angeweza kuwa mbumbumbu wa elimu kuhusu UKIMWI kiasi kile.



Hata hivyo, wengi wao hawakuwa na muda mwingi wa kumzungumzia. Baadhi yao walimsamehe lakini hakuna aliyemsahau!



**********

SIKU moja muujiza ulitokea. Baada ya miaka hiyo miwili, kama ndoto vile, Matanuzi alizuka kijijini hapo. Lakini huyu hakuwa yule Matanuzi ambaye wanakijiji wengi walimfahamu. Ulikuwa ni mzimu wa Matanuzi. Naam, Matanuzi alitisha! Alibadilika nywele na ngozi. Alikondeana kama mkimbizi aliyeishi siku nyingi bila kupata malazi bora wala chakula. Macho yake yaliingia ndani huku midomo ikiwa imemkauka. Kila aliyemwona alishtuka, hali iliyomtia simanzi zaidi.



Akajikuta akiangua kilio mara tu alipoingia ndani ya nyumba ya Mzee Nshinze.

“Nimekosa...nimekosa sana baba mkwe,” alisema huku akibubujikwa machozi.



Familia yote ya Mzee Nshinze ilikuwa mbele yake, kila mmoja kaketi kitini, wakimtazama kwa mshangao.



“Nimekukoseeni wote,” aliendelea kuomboleza. “Nimemkosea mke wangu. Hata mwanangu mpenzi nimemkosea sana. Nimekuja kuomba radhi ili nimwone mwanangu kabla sijafa.”



Huruma ya kibinadamu iliwaingia wote. Huku bado wakiwa wamepigwa butwaa, mama aliamuru mgeni atengewe chakula. Kikatayarishwa chakula kizuri; wali kwa samaki. Lakini kama ilivyotarajiwa, Matanuzi alikula kwa taabu sana, tena alikula chakula kidogo tu.



Mama yake Siamini, na Siamini mwenyewe walitazamana. Mioyoni walikuwa wakiongea jambo moja tu; kuwa, wakati wa kuitumia ile elimu waliyopewa ulikuwa umewadia. Lakini haikuwa kabla ya Siamini kumshurutisha mumewe kueleza yote yaliyomkuta tangu walipotengana hadi wakati huo.



“Ni hadithi ya aibu,” Matanuzi alisema kwa unyonge, macho kamkazia Siamini. “Tangu siku ile ulipokwenda kupimwa na kupata yale majibu, mimi nilichanganyikiwa sana. Nilikuwa na hofu kubwa ya kupimwa kwa kuamini kuwa, kujua ukweli huo kungeharakisha kifo changu. Kumbe ilikuwa ni kinyume chake. Leo nakuona umebadilika sana, mke wangu. Umenawiri! Na nadhani kujua mapema ukweli kuhusu afya yako kumekusaidia.”



Aliendelea kueleza kuwa ni hofu ile iliyomfanya aanze kuwa mlevi na baadaye kuomba uhamisho. Ulevi ukiambatana na kutokula vizuri, haikumchukua muda mrefu afya yake kuanza kuzorota. Hali hiyo iliambatana na maradhi mbalimbali, kama homa za mara kwa mara, kuharisha, kuota majipu, kuugua mkanda wa jeshi na kero nyingine nyingi tu.



“Hali ya kuumwa kila mara, na ulevi, vilisababisha niachishwe kazi,” Matanuzi aliendelea. “Hapa nilipo sina mbele wala nyuma. Nilifikiria kujiua lakini nikaona ya nini, kama ni kufa si nitakufa hivi karibuni? Ndipo nikapata wazo la kurudi nyumbani kuwaoneni wazee, mke wangu na mwanangu kabla sijafa.”



Ilikuwa ni habari nzito na ya kusikitisha masikioni na akilini mwa wasikilizaji. Siamini alikuwa na hasira lakini sasa hasira hizo zilishuka. Akaingiwa na huruma dhidi ya mumewe, Matanuzi. Akakubaliana na wazo la wazazi wake kuwa Matanuzi apewe chumba hapo ili ahudumiwe, na afya yake iliyotetereka irekebishwe kwa lishe bora na matibabu kwa maradhi mengine.



“Tutakuelekeza namna ya kuandaa lishe sahihi,” Siamini alimwambia Matanuzi. “Ukiyafuata maelekezo hayo, afya yako itarudi kuwa nzuri kama zamani. Usipofanya hivyo utaendelea kuathirika zaidi.”



Kisha alionekana kukumbuka jambo. “Hivi, pamoja na maelezo yako yote umekwishapima damu yako?” alimuuliza.



“Vipimo vya nini? Hali yangu si inajionyesha wazi?” ndiyo iliyokuwa kauli ya Matanuzi.



“Hali gani?” Siamini alifoka. “Unataka kusema hiyo hali ya kuharisha? Au majipu? Magonjwa yote hayo si yalikuwepo kabla ya UKIMWI! Hapana, sikuelewi! Lazima ukapime, upate ukweli kuhusu afya yako. Kesho nitakupeleka hospitali. Ukithibitika kuambukizwa ndipo tutakuanzishia 'tiba' hii mbadala kwa mujibu wa wataalamu.”



Walikwenda hospitali.



Vipimo vikathibitisha.



Tiba ikaanza.



**********

TATIZO kubwa la Matanuzi, kwa mujibu wa maelezo yake lilikuwa la maumivu mdomoni wakati wa kula, kutokuwa na hamu ya kula, na chakula kutosagwa vizuri tumboni. Hali kadhalika haikuhitaji mizani kujua kuwa uzito wake ulipungua sana.



Mkewe, Siamini alidhamiria kupambana na matatizo hayo moja baada ya jingine. Akaanza na lile la kupoteza nguvu na kupungua uzito. Kabla hajaanza maandalizi yake, alijikumbusha tena maelezo ya mtaalamu wa lishe juu ya tatizo hilo.



NI VYEMA MWATHIRIKA AENDELEE KULA CHAKULA MCHANGANYIKO NA CHA KUTOSHA. ILI KUONGEZA UZITO, INABIDI KULA VYAKULA VYA KUJENGA MWILI NA VILE VYENYE KUTIA NGUVU NYINGI KAMA VILE KARANGA, MAYAI, MAZIWA YASIYOPUNGUZWA MAFUTA, SIAGI, SUKARI, MAJI YA MATUNDA, PARACHICHI, NYAMA NA KADHALIKA. PIA INABIDI AONGEZE KIASI CHA VYAKULA VYOTE ANAVYOTUMIA.



Siamini alianza kuandaa chakula cha aina hiyo kwa ajili ya Matanuzi. Kwa kufuata maelekezo ya kitaalamu alifanya yafuatayo katika upishi wake; aliongeza mafuta na sukari kwa kiasi kwenye vyakula alivyomwandalia Matanuzi. Akakamulia limao kwenye vyakula vyenye mafuta kama vile nyama nono, sambusa, karanga na kuku ili kusaidia usagaji wa chakula tumboni. Na ili kuwezesha mafuta kufyonzwa na mwili kwa urahisi, aliweka kiasi kidogo cha ganda la chungwa au limao lililosagwa kwenye vyakula vyenye mafuta mengi.



Maandalizi haya aliyafanya kwa nia ya kufanya Matanuzi aongeze uzito. Kwa kuzingatia pia kuwa mara nyingi alikuwa hana hamu ya kula, Siamini alipika kwa kutumia viungo mbalimbali ambavyo aliona kuwa havina madhara. Hali kadhalika, mara kwa mara alimtengenezea vinywaji vyenye viungo mbalimbali badala ya chai na kahawa.



Kwa lengo la kusaidia zaidi usagaji wa nyama tumboni alihakikisha kila mara anampa pia papai. Na vilevile alimshurutisha kutafuna chakula sawasawa ili iwe rahisi kusagwa tumboni. Matunda ya jitihada hizo yalianza kuonekana baada ya siku chache. Matanuzi alianza kumudu kula chakula chote alichotayarishiwa. Si hilo tu, bali pia alianza kuihisi njaa na kudai chakula. Hata uzito wake ulianza kuongezeka, jambo lililomtia matumaini kila aliyemwona.



Hata hivyo, tatizo jipya lilijitokeza. Na halikuwa tatizo dogo kama wengine wanavyoweza kufikiria. Wakati mwingine Matanuzi alipatwa na kichefuchefu na kutapika. Tatizo hilo lilimsumbua sana akili mkewe, Siamini. Aliumia moyoni kuona chakula kile kizuri alichomwandalia mumewe kikiishia katika matapishi au kutokuliwa, chakula ambacho wengi walikifurahia.



Kila mmoja alishangazwa na hali hiyo. Hivyo, siku chache baadaye, Siamini alimwomba mdogo wake, Festo amsindikize mjini, ili akapate ushauri zaidi kwa mtaalamu.



Mtaalamu alimpokea kwa furaha. Wakaongea kuhusu tatizo la Matanuzi. Mtaalamu akamwambia, “Kama kichefuchefu kinamsumbua, jaribu kumpa vyakula vichachu au vyenye chumvi. Jaribu pia vyakula laini au visivyo na viungo. Mshawishi ale vyakula vikavu kabla ya kuamka kitandani asubuhi.



“Mwepushe na vyakula vyenye mafuta mengi,” mtaalamu aliendelea. “Pia usimpe vyakula vyenye viungo na harufu kali. Usiache akae muda mrefu bila ya kula, na asile haraka haraka.”



Siamini alimtazama mtaalamu huyo kwa makini. Kisha akamuuliza, “Na kama anatapika?”



“Mpe chakula kidogo kidogo mara kwa mara. Pia anywe maji kati ya mlo mmoja na mwingine, badala ya kunywa maji wakati wa kula. Umenielewa?”



“Nakuelewa vizuri, dokta.”



“Vizuri,” mtaalamu alisema huku akitabasamu kwa mbali. Akaongeza, “Ajaribu kupumzika baada ya kula. Na ni vizuri akiweka kichwa juu ya mto. Asile haraka, ajipe muda wa kutosha.”



Siamini na mdogo wake, Festo waliusikiliza ushauri huo kwa makini. Mtaalamu akamwongezea Siamini makabrasha mengine yenye maelekezo zaidi.



Maandalizi ya chakula kwa ajili ya hali yake hiyo mpya yalianza. Lishe hiyo ilikuwa kama dawa. Kutapika kulikoma na kichefuchefu kilidhibitiwa. Lakini kama ilivyo tabia kwa mwili ulioathirika, matatizo hayakuishia hapo.



Matanuzi alianza kuharisha!



Siamini hakushangazwa sana na hali hiyo. “Mabadiliko ya chakula yanaweza kuendana na mabadiliko ya tabia kwa mlaji,” alisema na kuzama katika hazina ya machapisho ya lishe aliyoyapata Hospitali ya Maweni.



“KAMA UNAHARISHA,” alijikuta akisoma kwa sauti, “KUNYWA VITU VYA MAJIMAJI KWA WINGI KULIKO KAWAIDA KAMA MAJI YALIYOCHEMSHWA, MADAFU, SUPU, MAJI YA MATUNDA AU MAJI YA CHUMVI NA SUKARI.



“JARIBU VYAKULA VYA MAJIMAJI KAMA UJI ULIOCHEMSHWA (TOGWA), MTORI, SUPU AU MAJI YA MCHELE. PIA , KAROTI ZILIZOCHEMSHWA AU SUPU YA KAROTI. KULA KIASI KIDOGO CHA CHAKULA MARA KWA MARA. KULA VYAKULA VYENYE POTASSIUM KWA WINGI KAMA VILE UNGA WA MUHOGO, NDIZI MBIVU, MBOGA ZA KIJANI ZILIZOPIKWA, MKATE, WALI NA MABOGA. TUMIA VITUNGUU SAUMU VILIVYOPONDWA, CHANGANYA KWENYE SUPU AU VINYWAJI VILIVYOCHEMSHWA.



“KULA NYAMA NYEUPE KAMA VILE NYAMA YA KUKU NA SAMAKI BADALA YA NYAMA NYEKUNDU MFANO; NG'OMBE, MBUZI NA KONDOO KWANI HUCHUKUA MUDA MREFU KUYEYUSHWA TUMBONI. CHUNGUZA ILI KUJUA KAMA MAZIWA YASIYOCHACHUSHWA YANAKULETEA KUHARISHA ILI UYAACHE. BADALA YAKE JARIBU MAZIWA YA MGANDO. PIA, EPUKA VYAKULA VYENYE MAFUTA MENGI. EPUKA UNYWAJI POMBE...



Maelezo yalikuwa mengi na Siamini aliyasoma kwa utulivu, akizingatia kila lililoandikwa. Hatimaye akaanza utekelezaji wake. Akafuata hatua kwa hatua. Siku mbili, tatu tu baadaye, tumbo la Matanuzi lilifunga. Akaendelea kunawiri. Akachangamka. Ile sura ya makunyanzi na kukosa raha vikatoweka.



Siku moja Siamini, Matanuzi na mtoto Festo walikuwa wameketi sebuleni. Siamini akasema, “Huu ugonjwa ni hatari. Lakini ni hatari kwa mwathirika kama atajawa na hofu. Sisi hatukustahili kuhofia chochote. Japo nasikia siku hizi kuna dawa za kuongeza siku za kuishi, lakini naamini lishe bora ni dawa nambari moja.



“Sipingi kuwa haifai kutumia dawa za hospitali. Hapana. Dawa za hospitali nazikubali kwa asilimia mia moja. Hata dawa za kiasili pia nazikubali. Lakini dawa zote hizo bila lishe bora zitageuka kuwa sumu mwilini. Tutumie dawa, lakini tusiache kula chakula bora. Tuko vitani. Tuko kwenye mapambano makali. Tusikubali kushindwa!”



Festo aliyekuwa kimya muda wote naye alisema, “Ni kweli dada. Tupigane kufa na kupona. Naamini tutashinda. Elimu uliyopata kwa wataalamu hata mimi imenisaidia sana. Nitawafundisha na watoto wenzangu. Huu ni ugonjwa hatari. Watu wote, kwa rika zote tunapaswa kuwa makini.”



“Ndiyo, mdogo wangu,” Siamini alisema. “Nafurahi kwa kuwa umelitambua hilo. Najua hata wewe utachukua hadhari kuhusu maambukizi ya ugonjwa huu.”



“Ndiyo, dada,” Festo alikiri. “Nitahakikisha nawaonya vijana wenzangu kuhusu tatizo la ugonjwa huu. Nitawapa maelezo yote tuliyopata kwa wataalamu.”



“Utakuwa umefanya vizuri sana, shemeji Festo,” Matanuzi naye alisema. “Wakipatikana watoto kumi wa aina yako, naamini vita dhidi ya maambukizi ya UKIMWI vitashinda.”



“Nitajitahidi,” Festo alisema kwa kujiamini.



**********

“NIKUPE nini daktari wangu?” siku moja, Matanuzi alimtania Siamini. “Siyo siri, kwa kweli unastahili kuwa daktari bingwa. Tiba yako ni nzuri sana. Ni tiba sahihi. Ona nilivyobadilika.”



Siamini alicheka, lakini Matanuzi alicheka zaidi. Ukweli ni kwamba sasa Matanuzi alijisikia kuwa yu mtu kati ya watu. Ile hali ya kuumwa-umwa ilitoweka. Alijisikia kujawa na nguvu mwilini. Hata hiki kicheko chake kilikuwa kicheko halisi, chenye kujaa furaha. Ndiyo, alicheka hadi gego la mwisho likaonekana.



Ni kweli umebadilika,” mkewe alimwambia.



“Yeah, kwa kweli sasa najisikia kuwa tofauti na wakati ule. Nilikuwa nusu mfu!”



**********



MIEZI mitatu baadaye tayari Matanuzi alikuwa amerejea katika hali yake ya zamani. Afya yake iliboreka kwa kiwango kikubwa. Hata ile nuru katika macho yake na mwili wote kwa ujumla vilirejea.



Jioni moja Siamini, Matanuzi na Festo walikwenda mjini Kigoma kutembea.

Huko wakaamua kupunga hewa na kujiliwaza katika ufukwe wa Ziwa Tanganyika. Walikuwa na amani mioyoni, furaha nyusoni. Walizungumza mengi, hoja hii na ile zikivitawala vinywa vyao.



Hatimaye Matanuzi alisema, “Kweli ujinga hauna mwenyewe.”



Festo na dada yake walishangaa, wakamtazama. Muda mfupi tu uliopita walikuwa wakizungumzia utamu wa dagaa wa ziwa hilo. Sasa hii kauli imeingiaje?



“Una maana gani?” Siamini aliuliza.



“Unajua kuwa pamoja na elimu yangu, pamoja na shahada zangu almanusura nijiue mwenyewe kabla ya siku zangu?”



“Ujiue?” Festo alimdaka. “Ujiue kwa nini, shemeji?”



Matanuzi alimtazama kidogo Festo. Kisha kwa sauti ya unyonge akasema, “Acha tu shemeji. We acha tu.”



Siamini alikuwa ameshamwelewa. Hakusema kitu.



“Nakwambia shemeji, acha tu,” Matanuzi alisema tena, safari hii sauti yake ikiwa ni ya chini zaidi. Akaendelea, “UKIMWI! UKIMWI! Ningejiua kwa hofu tu ya kupata UKIMWI! Kweli mficha maradhi kifo humuumbua.”



Siamini alitikisa kichwa kwa masikitiko. Akamtazama kwa huruma. Kisha akasema, “Ni kweli. Na ni muhimu kwa serikali na taasisi zake kuhakikisha kuwa elimu, hasa elimu ya lishe inamfikia kila mtu. Kwa mtazamo wangu, lishe ni tiba ya kwanza kabla ya dawa nyingine. Na kwa tatizo hili la UKIMWI, elimu juu ya lishe inahitajika zaidi.”



Matanuzi alitikisa kichwa akionyesha kuafikiana na maneno hayo ya Siamini. Naye akasema, “Ninaamini kuwa kama hizo dawa za kuimarisha kinga ya mwili zingemfikia kila mmoja, kwa muda mwafaka, na mtumiaji akazitumia sanjari na lishe bora kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu, vifo vitokanavyo na UKIMWI vingepungua kwa kiasi kikubwa.”



“Uko sahihi,” Siamini aliitika. “Tatizo ni kwamba, waathirika wengi katika nchi za Kiafrika ambazo ni maskini, wana matatizo makubwa ya mapato. Kipato cha mtu ni kidogo kiasi cha kumfanya hata asiwe na hakika ya kupata mlo mmoja wa siku. Itakuwa rahisi kupata mkusanyiko wa lishe stahiki inayoweza kupambana na VVU?”



“Hilo ndilo tatizo,” Matanuzi alisema kwa unyonge.



“Naam, ndilo tatizo linalotukabili,” Siamini alimuunga mkono. “Ni tatizo linalopaswa kutatuliwa kwa misaada ya jumuia za kimataifa.”



Wakati wote huo Festo alikuwa kimya, akiwasikiliza kwa makini.





*****HUU NDIO MWISHO WA SIMULIZI HII FUPI. TUNAAMINI KUWA KWA NAMNA MOJA AU NYINGINE UNAWEZA KUWA UMEPATA ELIMU YA KUPAMBANA NA GONJWA HILI HATARI DUNIANI. TOA MAONI YAKO.*****



MWISHO

0 comments:

Post a Comment

BLOG