SIMULIZI FUPI : NJOZI
Jua lilikwisha zama lakini bado nyuma liliacha mikia yake ya uchengu wa mwangaza uliopinganisha rangi tofautitofauti kama ishara ya heri njema kwa wote walioipenda siku hiyo.Hadi kufikia wakati huo, bado tulikuwa baharini tukikamilisha shughuli zetu za uvuvi. Kweli ilikuwa siku njema. Tulibahatika kuwavua samaki wengi mno. Pengine kwa sababu unyavu wetu ulikuwa ungali mpya. Tulifurahia na kuchangamkia jambo hili hata tukawa tunapiga soga kwa ucheshi mwingi tukiisukuma mashua yetu kufelekea ukingoni mwa ziwa kwani kilicho na mwanzo kina mwisho.
Mara kwa ghafla bin vuu, upepo mkali ukaanza kuvuma kwa nguvu kama za tembo. Mawimbi yakawa yameanza kujitunga tayari ziwani. Yalionekana yakijibeba, yakijiinua na kujibwaga tena kwa nguvu. Mawingu mazito tena meusi ti yakuogofya na kutisha yalikuwa yamekusanyika angani. Dalili ya mvua ni mawingu.
Kuona vile,sote tuliingiwa na wasiwasi kama wa kuku mgeni. Mambo yalikuwa yakitambarika kila muda ulipozidi kuyoyoma. Ndiyo sasa tulikuwa tumefika katikati ya ziwahilo. Kwa utaratibu, mashua yetu ilianza kuongeza uzito hadi ikawa nzito kama nanga.isitoshe, Samaki tuliokuwa tumewavua pia walichangia uzito kuongezeka.
Liloogofya zaidi ni kuwa hapakuwa na wavuvi wengine ziwani. Wote walikuwa washatoweka, wakatokomea na kuvogomea katika peo za macho yetu. Walikuwa wamerudi viamboni mwao kujiunga na jamaa zao. Nyoyo zetu zilitututa kwa nguvu kwa hofu. Upepo mkali ukaanza na kwa umbali tuliona miti zikiinama kusalimu amri. Lililonijia akilini ni tukio lililomkumba Yesu na wafuasi wake kama nilivyopata kuona kwenye sinema awali. Yesu alionekana kuunyosha mkono wake na kuamuru mawimbi kutulia na ghafla yakapoa. Nami bila kusita niliunyosha mkono wangu kama Yesu na kuyaamuru kutulia, jambo lililowafanya Nguviu na Suluhu kuangua vicheko licha ya hali iliyotawala. Lakini hakuna kilichobadilika. Pengine hatukuwa na imani dhabiti katika Bwana.
Badala yake, mashua yetu ikaanza kuingia na kuzama majini. Tulijaribu kupunguza kiimo cha mashua yetu kama hatua ya kwanza. Ungeona namna walivyoruka, kuogelea na kupotelea majini kwa furaha, ungedhani ni wafungwa wameachiliwa huru baada ya hukumu ya kifo. Uzani ukapungua kidogo na tukarejelewa na cheche za matumaini.sote watatu tukawa tunasukuma mashua yetu kwa furaha. Tukaamua kufanya chapuchapu kuiondoa mashua yetu humo ziwani kwani giza lilikuw limeanza kutawazwa angani. Tena tulitaka kuondoka kabla mvua kuanza kunyesha. Wahenga huonya eti tahadhari kabla ya hatari.
Sikuona wala kujua namna Suluhu alivyorudisha unyavu majini. Alitugutusha alipoanza kucheka na kuitana tumpe usaidizi wa kuuvuta unyavu huo kwani ulikuwa na windo nono. Nani asingefurahi? Tena umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu na aidha kidole kimoja hakivunji chawa. Sote tukauangana na kuanza kuburura hadi hapakuwa na dalili zozote za wavu kusonga.
Sululu alisonga mbele zaidi na kuburura kwa nguvu zake zote na lo! Samaki mkubwa alijitokeza kwa rabsha,fujo, vurumai na kishindo na kisha kuzama ghafla na kufanya mashua yetu kutingizika. Kumbe mkia wake ulikuwa katika sehemu ya chini ya mashua yetu ndani ya maji. Hili tuligundua kwa namna mashua yetu ilivyorushwa. Tukawa majini tukipigania maisha yetu. Kwa mara ya kwanza nikakutana na kifo ana kwa ana. Tulianza kupiga mayowe kutaka usaidizi lakini vilio vyetu viliambulia patupu.
Ikawa kila mtu na mzigo wake kwani mvua kubwa ilikuwa ishaanza kunyesha. Ngurumo za radi zilisikika na nguo zetu zikaloa chepechepe. Tukawa sasa ni kuogelea, haswa mimi niliyesalia na wiki moja tu kukalia mtihani wangu wa kitaifa wa kidato cha nne. Mashua yetu ilisombwa na maji na kuenda mbali mno. Potelea pote! Heri uzima kuliko mashua. Tulikuwa tumeogelea na hata kukaribia sana ukingoni.
Lakini kila mara maji yalituzidi nguvu. Kumbe tulijiingiza katika ziwa bila mbinu toisha za kuogelea. Susulu alichelewa kupiga mayowe kwani tulipomsikia akifanya hivyo, tayari alikuwa akisukumwa na maji. Alikazana kutufikia na kutupa mkono wake lakini nguvu zilionekana kumwisha hadi akwa anapelekwa tu kama gogo. Tulijaribu kadri ya uwezo wetu kumfuata lakini wapi! Alikuwa keshakwenda zake. Msomaji, hisia zetu baada ya hapo zilikuwa hazielezeki.
Tulipokuwa mita chache tu karibu na ukingo wa ziwa, Nguviu naye alilalama eti mguu wake ulikuwa umekamatwa na kitu kisichojulikana. Nikainua kichwa zaidi juu ya maji na kutamka kwa shida nikimwarifu kujikaza kufika ukingoni ili suluhisho lipatikane. Huo haukuwa wakati wa kusema mengi kwani maji yaliingia kinywani. Lakini aliendela kunung’unika zaidi.
Nilionekana kujua kuogelea zaidi. Nikamwambia aushikilie mguu wangu mmoja nami niogelee hadi mwisho kisha nimvute. Japo ilikuwa ngumu kuogelea katika hali hiyo, nilijaribu na kufika ukingoni salama. ‘Mungu hamwachi mja wake.’ Nilisema kwa sauti. Mimi ndiye nilitangulia na kuona kipande cha gogo. Nikafurahi na tabasamu hafifu ikaonekana usoni mwangu.
Bila kukawia, nililipanda gogo lenyewe na nikawa sasa namshawishi Nguviu kuunyosha mkono wake niukamate, kasha nimvute pia. Cheche za matumaini zilizotoweka awali zikarejea tena. Nguviu aliukaribia mkono wangu kwa utaratibu. Akaunyosha wake, nikaukamata na kuanza kumvuta.
Mara tu aliponipa mkono wake wa pili, alivutwa ghafla na mara hii akazama zii. Nilikuwa tu nimeanza kupiga mayowe wakati lile gogo nililopanda lilizama pia na kunitumbukiza majini. Kumbe alikuwa ni mamba niliyemkanyaga kwa wakati huo wote! Kila kitu kikawa giza totoro kwangu.Nilipiga usiahi mkali na kujaribu kufungua macho. Ndipo nikagutuka kutoka usingizini. Nilikuta darasa zima linanizomea huku Susulu na Nguviu wakifa kwa vicheko vilivyopenya angani kana kwamba walikuwa na fununu ya kile nilichoota. Nduru ndiyo ilimfanya mwalimu wa Bayolojia kugundua kuwa nilikuwa nikilala darasani wakati wote tangu alipoanza kufunza alasiri hiyo. Nilijua kilichonisubiri baada ya kipindi kukamilika.
0 comments:
Post a Comment